Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

HABARI MPYA YA LIYUMBA NA SAKATA LA SIMU GEREZANI

 

 
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Amatus Liyumba (pichani), amedai mahakamani kwamba tuhuma za kukutwa na simu ya mkononi gerezani isivyo halali, siyo za kweli bali zilikuwa ni njama za kumfanya aozee gerezani.

Kadhalika, amedai kuwa mtiririko mzima wa kesi hiyo ni wa kupikwa kwa sababu maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), walikwenda gerezani Ukonga mara mbili tofauti wakitaka kumhoji, lakini alikataa na kwamba alijua wana nia ya kumbambikia kesi.

Liyumba alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi wa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando, aliyepangiwa kuisikiliza kesi hiyo.

Akiongozwa na wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, alidai kuwa Julai 27, mwaka 2011, mchana, akiwa kwenye chumba chake Gereza la Ukonga, alikuwa akibadilishana na mawazo na mtu mmoja raia wa Kenya, mara aliingia askari magereza aliyemtaja kwa jina la Patrick akiwa na simu mkononi na kudai kuwa amemkuta nayo.



“Nilishangaa sana kwani simu alikuwa ameishika yeye askari magereza na mimi kabla ya kuingia gerezani nilipohukumiwa kutumikia miaka miwili, nilivua nguo zote na kupekuliwa kama utaratibu wa magereza unavyoelekeza. Hiyo simu niliipata wapi kama siyo kunibambikia kesi bila sababu,?” Alihoji na kuongeza:

”Mheshimiwa, hizi tuhuma siyo za kweli wamenibambikia kwa lengo la kutaka niozee gerezani na kama kweli nilikutwa na simu nikiwa gerezani, hakuna ushahidi uliosema kwamba laini iliyokuwa kwenye simu hiyo imesajiliwa kwa jina langu na niliwezaje kuingia na simu wakati nilikaguliwa na kupekuliwa?.”

Alidai kuwa alikataa kuhojiwa na maofisa wa Takukuru kwa masharti ya kuhojiwa mbele ya wakili wake kwa sababu alihisi kuna kesi nyingine wanataka kumbambikia.

“Takukuru walikuja kunihoji miezi miwili kabla sijamaliza kifungo changu na baada ya kubaki mwezi mmoja na nusu likatokea hili la kunituhumu kwamba wamenikuta na simu, nilistushwa sana na hata sielewi nini kilitokea kuhusu tuhuma hizi,” alidai Liyumba.

Aidha, alidai kuwa kwa mujibu wa taratibu za magereza, mfungwa anapofanya tukio lolote la utovu wa nidhamu, hushtakiwa kwa Mkuu wa Magereza ambaye husikiliza na kutoa maamuzi ikiwamo adhabu mbalimbali.

“Kabla ya kutuhumiwa kukutwa na simu, nilikaa gerezani nikitumikia kifungo cha matumizi mabaya ya madaraka kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu na kwamba katika kipindi chote sijawahi kukutwa na kosa la utovu wa nidhamu wala kushtakiwa kwa Mkuu wa Gereza  ama kuonywa kwa tuhuma yoyote.

Naiomba mahakama hii iniachie huru na kuifuta kesi inayonikabili kwa sababu tuhuma siyo za kweli,” alidai Liyumba.

Hakimu Mmbando alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, watawasilisha hoja za kama mshtakiwa ana hatia au la, Desemba 30, mwaka huu na hukumu itasomwa Januari 15, mwaka 2014.

Septemba 8, mwaka 2011, Liyumba Alifikishwa mahakamani hapo akishtakiwa kwa kosa la kukutwa na simu wakati akiwa gerezani akitumikia kifungo cha miaka miwili kwa kutokana na kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Katika kesi hiyo, ilidaiwa kuwa, Julai 27, mwaka 2011, kinyume cha Sheria ya Magereza, Liyumba alikutwa na simu ya mkononi aina ya Nokia 1280 katika chumba chake cha magereza bila kuwa na kibali.
 
CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top