Serikali ya Afrika Kusini imesema kiongozi huyo
ambaye atazikwa Desemba 15, imeandaa mazishi ya kihistoria
yanayosemekana yatazidi yale ya Papa John 11.
Matukio ya shughuli mbalimbali zinazohusu mipango
ya maziko ya kiongozi huyo maarufu yanatarajiwa kushuhudiwa sehemu
mbalimbali duniani, tofauti na tukio jingine lililowahi kutokea barani
Afrika mbali na kombe la dunia.
Rais Jacob Zuma alisema jana kwamba “Mpendwa wetu
Madiba atazikwa kwa heshima zote za Serikali. Nimeagiza bendera zote za
Afrika Kusini zipepee nusu mlingoti na hiyo itaendelea hivyo hadi
tutakapokamilisha mazishi yake.
Mazishi ya Mandela yanalinganishwa na yale ya Papa
John Paul II mwaka 2005, ambayo yalihudhuriwa na wafalme watano, malkia
sita wa falme mbalimbali na marais wapatao 70 na mawaziri kadhaa,
wakiwamo wafuasi wake zaidi ya milioni mbili. Yanakadiriwa pia kulingana
na maziko ya Winston Churchil aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwaka
1965.
Marais wote wa Marekani walio hai wanatarajiwa
kuhudhuria mazishi hayo iwapo afya zao zitawaruhusu kusafiri, pamoja na
Prince Charles wa Uingereza na hata Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Pia
watu maarufu wenye urafiki wa karibu na Mandela akiwamo msanii Oprah
Winfrey wameshathibitisha kuhudhuria.
Changamoto la kiusalama
Kutokana na idadi kubwa ya wakuu wa nchi na watu
maarufu duniani wanaotarajiwa kufika Afrika Kusini, suala la usalama
limeelezewa kuwa changamoto mpya kwa vyombo vya usalama nchini humo.
Afrika Kusini imekuwa moja ya nchi zinazokabiliwa
na matukio ya uporaji na mauaji yanayotokana na idadi kubwa ya wahalifu,
wengi wao wakidaiwa kuwa wahamiaji haramu.
“Huyu ni shujaa wa dunia. Tutafanya mipango ya
mazishi makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa. Nadhani kila nchi itakuwa
imeandaa utaratibu wake wa namna ya kushiriki,” alisema mmoja wa
wanadiplomasia wa Afrika Kusini ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Siku 11 za maombolezo
Serikali ya Afrika Kusini, kwa mujibu wa gazeti la
The Guardian tayari imeweka wazi ratiba ya siku 11 za maombolezo tangu
alipofariki dunia juzi jioni. Japokuwa ratiba hiyo ilishaandaliwa karibu
mwaka mmoja uliopita na kupitiwa na kufanyiwa maboresho katika baadhi
ya maeneo, inaonyesha namna maofisa wa Serikali ya Afrika Kusini
walivyolipa uzito suala hilo na kulifanya kuwa tukio la kukumbukwa
katika historia.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment