Mkaguzi
wa Jeshi la Polisi toka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoani Arusha
Honorina Msoka akitoa zawadi kwa mmoja wa wagonjwa waliokuwa wamelazwa
katika wodi ya Watoto na akina mama katika hospitali ya Mkoa ya Mount
Meru iliyopo mkoani hapa ikiwa ni hatua ya Jeshi hilo kuungana na Wadau
wengine duniani kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia.(Picha na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mkuu
wa kitengo cha Dawati na Jinsia Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi (SSP) Mary Lugola akimkabidhi moja ya zawadi kwa Msimamizi wa
Kituo cha Faraja Bi. Martina Siara ambacho kinahudumia watoto wa mitaani
na wanawake waliojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na mazingira
magumu. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi toka Dawati la Jinsia na Watoto Maria Maswa akiwa
anaongea na wanawake waliojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na
mazingira magumu ambao wanalelewa na Kituo cha Faraja kilichopo jijini
hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jumla
ya kesi 507 zinazohusiana na matukio ya ukatili na unyanyasaji wa
Kijinsia zimeripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto la Mkoa wa
Arusha ambapoTakwimu hizo ni toka Novemba 2012 hadi Novemba 2013 mwaka
huu.
Hayo
yalielezwa na Mkuu wa kitengo hicho Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP)
Mary Lugola wakati watendaji wa ofisi hiyo walipoungana na wadau
mbalimbali duniani kuadhimisha siku 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji
wa Kijinsia walipotembelea Shirika lisilo la Kiserikali la Faraja
centre linaloshughulika na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira
magumu na wasichana waliojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na
wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Akitoa
ufafanuzi kuhusiana na kesi hizo alisema kwamba, idadi hiyo imeongezeka
kwa asilimia 14.7 ikilinganishwa na Novemba 2011 hadi Novemba 2012
ambapo kesi 442 ziliripotiwa. Alisema ongezeko hilo linatokana na elimu
inayotolewa mara kwa mara na Ofisi hiyo kwa wananchi kupitia mikutano na
vyombo vya habari hali iliyowafanya wananchi wahamasike kupinga vitendo
vya ukatili na unyanyasaji kwa kutoa taarifa katika Ofisi hiyo.
Alisema
kati ya kesi hizo, kesi zilizokuwa zinawahusu wanawake ni 280 wakati
wanaumeni 120 huku watoto ni 107. Miongoni mwa kesi hizo tayari kesi 132
zimekwishafikishwa mahakamani huku kesi 375 zinaendelea kupelelezwa.
Mkuu
huyo wa Dawati la Jinsia na Watoto (SSP) Mary Lugola alisema kwamba
miongoni mwa kesi zinazoripotiwa katika ofisi hiyo ni pamoja na ubakaji,
kulawiti, ukatili dhidi ya mtoto, migogoro katika ndoa na kadhalika.
Akizungumza
wakati anawatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu na
wasichana waliojifungua wakiwa na umri mdogo ambao wanalelewa na
Shirikalisilo la Kiserikali la Faraja na wagonjwa waliolazwa katika Wodi
ya Watoto hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, (SSP) Mary Lugola alisema
kwamba katika kuonyesha kujali kitengo cha Dawati kimeamua kuungana nao
kwa kuwatembelea na kutoa zawadi mbalimbali kwa makundi hayo.
Kwa
upande wake msimamizi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Faraja Young
Women Development Organization Bi. Martina Siara alilishukuru jeshi la
Polisi mkoani hapa kitengo cha Dawati kwa jinsi linalovyoshirikiana na
kituo hicho cha Faraja katika katika suala zima la ulinzi pamoja na
utoaji wa elimu na ushauri kwa wanafunzi waliopo kituoni hapo hivyo
kuwapa mwanga kuhusiana na haki zao.
Jeshi
la Polisi kupitia kitengo cha Dawati Mkoani hapa limeadhimisha siku 16
za kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa kutembelea kituo cha
Faraja na wodi ya watoto katika hospitali ya Mount Meru kwa kutoa zawadi
mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho pamoja na wagonjwa waliolazwa
hospitalini hapo huku likiwa na kauli mbiu ya jeshi hilo nchini isemayo
“Zinduka tumia Dawati la Jinsia na Watoto kukemea Ukatili wa Jinsia na
Watoto”.
Post a Comment