Kaimu kamanda wa kikosi cha polisi cha Tazara,
(SSP) Inocent Mgaya (katikati) akiwa na OCD wa kituo hicho SP, Bakari
Makuka (kushoto) na SP, Shaaban Hussein wakionesha meno ya tembo kwa
waandishi wa habari.
Meno hayo yalikamatwa Alhamisi wiki hii, ikiwa ni siku chache baada
ya mawaziri wanne kuondolewa madarakani kutokana na kutosimamia vizuri
zoezi la 'Operesheni tokomeza majangili '.
Akizungumza jana, Kaimu kamanda wa kikosi cha polisi cha Tazara,
(SSP) Inocent Mgaya, alisema katika tukio hilo alikamatwa Ally Juma
(26), maarufu Ngagari, fundi seremala na mkazi wa Kisaki.
Kamanda Mgaya, alisema walipata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa
kuna mtu amebeba meno ya tembo ndani ya treni hiyo iliyokuwa ikitokea
Zambia kwenda jijini Dar es Salaam.
Alisema baada ya kufanya upekuzi katika behewa namba M2,
walifanikiwa kumkamata mtu huyo akiwa na mabegi mawili yakiwa
yamehifadhiwa pembe 14 za tembo na kipande kimoja cha jino la kiboko.
"Tulipomkamata na kumfanyia upekuzi tuligundua begi la kwanza
lilikuwa na vipande vinane vya pembe nane na la pili aliweka vipande
saba," alisema Kamanda Mgaya.
Alisema kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na
Utalii, walibaini vipande hivyo vya pembe za tembo vina uzito wa kilo
29 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 1950 (Sh. 25,520,000).
Jino la kiboko lilikutwa na uzito wa gramu 900 lenye thamani ya Sh. milioni 2.5.
"Nataka kuweka wazi kwamba usafiri wa treni ni kwa ajili ya watu
kupata usafiri wa uhakika na sio vinginevyo, polisi wapo makini
kuhakikisha hakuna mtu anayetumia chombo hiki kwa uhalifu," alisema.
Aidha, kwenye tukio hilo polisi walikamata mifuko miwili ikiwa imepakiwa madawa ya kulevya aina ya bangi.
Hata hivyo, hakuna mtu aliyekamatwa kuhisika na mifuko hiyo yenye uzito wa kilo 19.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment