IMEELEZWA
kuwa Ismail Aden Rage (pichani) ndiye Mwenyekiti halali wa Simba ambapo
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imemtaka kuitisha Mkutano Mkuu
kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.
Kamati
imebaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya
Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha
Mwenyekiti wao. Upungufu huo ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya
Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha
Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.
Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.
Hivyo,
agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe
mkutano lipo palepale. Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa
kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.
Katika
mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya
Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa
na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya
Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.
TFF
inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na
klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji
wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.
Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.
Kuhusu
mchezaji Emmanuel Okwi ambaye aliuzwa nchini Tunisia, TFF inafahamu
kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa na itasaidia kufuatilia FIFA fedha
za mauzo ya mchezaji huyo.
Post a Comment