Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hali
ya kuendelea kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei nchini.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO,Dar es salaam.
OFISI
ya Taifa ya Takwimu imesema Tanzania inapiga hatua nzuri katika
maendeleo ya uchumi kutokana na hali ya mfumuko wa bei nchini kuendelea
kudhibitiwa hali inayoleta unafuu wa maisha kwa mlaji.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu
za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa
mfumuko wa bei wa Taifa kwa Mwezi Novemba 2013 umepungua hadi kufikia
asilimia 6.2 kutoka 6.3 za mwezi Oktoba 2013 kutokana na kupungua kwa
bei za bidhaa na huduma.
Amesema
kuwa hali hiyo imesababishwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa bidhaa
za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa mwezi Novemba ikilinganishwa
na mwezi Oktoba na kuongeza kuwa kumekua na ongezeko dogo la mfumuko wa
bei wa bidhaa za nyumbani na migahawani hadi kufikia asilimia 7.6
kutoka 7.3 za mwezi Oktoba.
Kwa
upande wa bidhaa zisizo za vyakula Kwesigabo ameeleza kuwa kasi ya
ongezeko la bei imepungua hadi asilimia 5.7 kwa Mwezi Novemba 2013
kutoka asilimia 6.1 za mwezi Oktoba.
Aidha
amefafanua kuwa taarifa za matokeo ya mfumuko wa bei unaopimwa kwa
kipimo cha mwezi unaonyesha kubaki kuwa asilimia 0.6 kama ilivyokuwa
mwezi Oktoba huku fahirisi za bei zikiongezeka hadi kufikia 142.23 mwezi
Novemba kutoka 141.39 za mwezi Oktoba
Amezitaja
baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kwa kuongezeka kwa fahirisi
za bei kuwa ni pamoja na mahindi kwa asilimia 2.4, vitafunwa ailimia
4.0, unga wa Muhogo kwa silimia 2.5, nyama kwa asilimia 1.1, kuku kwa
asilimia 3.7, samaki waliokaushwa kwa mafuta kwa asilimia 5.2, nazi
asilimia 5.7.
Bidhaa
nyingine ni pamoja na dagaa kwa asilimia 2.5, mbogamboga kwa asilimia
3.0, nyanya asilimia 6.0, Maharage 4.5, karoti kwa asilimia 5.8 na viazi
mviringo asilimia 4.6.
Ameongeza
kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula hasa mchele kwa mwezi
Novemba 2013 umeonyesha kupungua kwa asilimia 26.0 ikilinganishwa na
mwezi Novemba mwaka 2012, bidhaa nyingine zilizopungua ni mahindi kwa
asilimia 9.4, unga wa mahindi 5.7, viazi mviringo 7.6 na karanga kwa
asilimia 9.7.
Kuhusu
mchango wa bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko
wa bei kwa kipimo cha mwezi Novemba 2013 ni pamoja na mitandao kwa
asilimia 4.7, radio asilimia 4.3 na vifaa vya kielectroniki kama luninga
kwa asilimia 2.7.
Hata
hivyo kufuatia hali hiyo ya mfumuko wa bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa
uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za
jamii kwa mwezi Novemba umeonyesha kuwa imara kwa kufikia shilingi 70 na
senti 31.
“Napenda
niwahakikishie kuwa fahirisi za bei za Taifa zimeonyesha kuwa na
mwelekeo imara kwa kipindi chote, kwa hiyo uwezo wa shilingi 100 ya
Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeonyesha kuwa na mwelekeo
imara kwa kufikia shilingi 70 na senti 31 ” amesema.
Kuhusu
ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko
wa bei nchini Kenya umefikia asilimia 7.36 kwa mwezi Novemba kutoka
asilimia 7.36 za mwezi Oktoba, huku nchini wa Uganda Ukifikia asilimia
6.8 kwa mwezi Novemba kutoka asilimia 8.1 za mwezi Oktoba.
Post a Comment