SIRI
mbalimbali zimeanza kufichuka kuhusiana na ‘madudu’ yaliyokuwa
yakifanyika, katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, iliyowang’oa
madarakani mawaziri wanne.
Siri
hizo zimeanza kuvuja baada ya kubainika kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
aliandikiwa barua mara mbili na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi juu ya ‘madudu’ hayo, lakini hakuweza kuchukua hatua.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA Jumamosi limezipata zilisema kutokana
na Pinda kushindwa kuchukua hatua, kulisababisha Dk. Nchimbi kugoma
kujiuzulu pale alipotakiwa kufanya hivyo.
Chanzo chetu cha habari kilisema kuwa Nchimbi aligoma katika kikao
kilichoitishwa na Pinda, wakati akizungumza na mawaziri wanne waliotajwa
katika ripoti ya Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira,
akiwashawishi waachie ngazi.
Chanzo chetu kilieleza kuwa katika kikao hicho, Dk. Nchimbi alimkumbusha
Pinda namna alivyokuwa akimpatia taarifa juu ya malalamiko ya wananchi,
lakini alijibiwa kuwa hiyo ni kazi maalumu ya Serikali.
Mbali na Dk. Nchimbi, mawaziri wengine walioitwa na Pinda ni Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo.
“Katika kikao kile, Dk. Nchimbi alimkumbusha waziri mkuu juu ya barua
mbili alizomwandikia, akimlalamikia jinsi operesheni ilivyoendeshwa.
Katika barua hizo, alimweleza mbona watuhumiwa wanaokamatwa hawapelekwi
katika mahabusu za polisi na badala yake wanafungwa katika nguzo za
umeme?
“Hakuishia hapo, Nchimbi akamweleza tena waziri mkuu kwamba, wakuu wa
mikoa na wilaya nao wanalalamika kwamba mikoa yao imevamiwa, watu
wanateswa, hiyo Task Force inaingia bila kamati za ulinzi na usalama za
mikoa yao kuwa na taarifa?
“Waziri mkuu alimjibu akisema kuwa ile ilikuwa ni Task Force (kikosi
kazi) na kwa msingi huo, Dk. Nchimbi aligoma katakata kuwajibika,”
kilisema chanzo chetu cha habari.
MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta, Dk. Nchimbi kupitia simu yake ya
kiganjani lakini simu hiyo ilikuwa ikiita bila kupokewa na baadaye
ilizimwa.
Mawaziri wote waliong’olewa kwa nyakati tofauti wameelezea hatua hiyo na wengi wakionesha wazi ni kama vile wameonewa.
Dk. Nchimbi aliweka wazi kile kilicho moyoni mwake kupitia mtandao wa
Facebook, akielezea alivyoguswa na namna atakavyoendelea kuwa na upendo
kwa wanadamu wenzake.
Balozi Kagasheki yeye alipata wasaa wa kuzungumza muda mfupi kabla ya
Waziri Mkuu kutangaza bungeni uamuzi wa Rais Kikwete, akikubali
kuwajibika kutokana na kilichojiri katika ripoti iliyosomwa na
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, James Lembeli.
Dk. Mathayo naye alipata fursa kama ya Kagasheki kuzungumza bungeni
akisema tuhuma zilizomo kwenye taarifa ya Operesheni Tokomeza
hazijamgusa.
Nahodha naye alihusisha kilichomtokea kuwa ni sawa na mitihani inayompata mwanadamu duniani na hivyo anapaswa kukabiliana nayo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
nchini, Isaya Mungulu amesema ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na
Mazingira iko upande mmoja kwa kutoangalia pande mbili zilizoathirika na
Operesheni Tokomeza Ujangili.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi ofisini kwake jana, Mungulu alisema
hata wabunge waliochangia mjadala wa ripoti ya Kamati ya Lembeli, nao
waliangalia upande mmoja wa waathirika.
“Katika operesheni ile askari polisi mmoja aliuawa, lakini wabunge
hawakuona huo umuhimu wa kuwazungumzia, lakini inategemea na hadidu za
rejea walizopewa,” alisema Mungulu.
Hata hivyo, Mungulu alisema Operesheni Tokomeza iko kwa maandishi na haikuagiza askari wakaue wananchi.
Naye, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alizungumza na MTANZANIA Jumamosi
alikiri ripoti ya Lembeli kuonyesha upungufu kwa kutoeleza bayana namna
majangili walivyoua askari waliokuwa wakipambana na ujangili.
Lugola alisema katika operesheni hiyo, ndugu yake wa kike ambaye ni
askari alikufa baada ya kupigwa risasi na majangili na kufa papo hapo.
“Ripoti ingeenda ndani zaidi tuone namna askari walivyokuwa
wakikabiliana na mazingira magumu wakati wakipambana na majangili na
wengine waliofariki.
“Lakini hii hoja ya watu kuteswa ni ya muda mrefu na haya yaliyotokea
imekuwa sawa na moshi tu uliowekwa kwenye mzinga wa nyuki,” alisema
Lugola.
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment