Meneja wa Mawasiliano wa Tanesco,Badra Masoud
*****
MacDonald Live Line Technology ilipeleka malalamiko yake kwa msuluhishi huyo Wakili Mtango Jonathan Lukwalo, baada ya Tanesco kusitisha mkataba kwa kampuni hiyo kwa madai kuwa ilichelewa kutekeleza kazi ya ukarabati wa njia za umeme mkoani Arusha.
Tanesco na kampuni hiyo ambayo hufanyakazi ya kutengeneza umeme bila kuzima umeme waliingia katika mkataba Machi mwaka 2010 wa kufanya ukarabati wa njia ya umeme njia ya Kilimanjaro-Arusha kwa kutafuta nguzo, kuzisafirisha hadi eneo la kazi.
Kazi hiyo ilitakiwa kukamilika ndani ya wiki 32 kuanzia Julai 2010, 28 hadi Machi 9, 2011.
Katika uamuzi wake, Wakili Jonathan aliiamuru MacDonald Live Line Technology kuilipa Tanesco Sh. milioni 700 kwa kuchelewesha kazi na kulisababishia hasara shirika.
Mkurugenzi wa MacDonald Live Line Technology, MacDonald Mwakamele, amesema kuwa hakuridhishwa na maamuzi ya msuluhishi kwa kuwa hakutilia maanani hoja alizoziwasilisha na kwamba wiki hii kampuni yake itafungua kesi katika Mahakama Kuu kuyapinga.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuchelewa kwa kazi hiyo kulitokana na muda kuwa mfupi kwa kuwa zinapoagizwa nguzo Sao Hill inahitajika miezi mitano au sita ili zikauke pamoja na muda wa kuzisafirisha hadi eneo la mradi.
Alisema Tanesco ilimpa Sh. milioni 400 wakati kazi ya kupata nguzo 700 na kuzisafirisha ilihitaji zaidi ya Sh. bilioni moja.
Pia alisema kuwa licha ya Tanesco kuvunja mkataba haikuwahi kumtambulisha kwa aliyekuwa meneja wa mradi huo ambaye pia alisema hakuwahi kufika eneo la mradi.
“Pamoja na kunitambulisha kwa meneja mradi katika mkataba, hakuwahi kukanyaga eneo la site,” alisema Mwakamele.
Mwakamele alisema kuwa alishangaa jinsi mkataba wake ulivyositishwa kwamba aliandikiwa barua mbili kwa terehe tofauti ya kwanza ya Desemba Mosi, 2010 ambayo ilimtambulisha kwa meneja wa mradi na kufuatiwa na ya Desemba 2, 2010 ambayo ilimpa karipio la kusitisha mkataba.
Alikanusa madai kuwa alipewa kazi hiyo na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, akisema kuwa akisema alipata mkataba huo mwaka 2004 kabla Mhando hajashika nafasi hiyo.
Alisema Tanesco inapaswa kufanya mambo ya msingi ili kuwapunguzia adha ya umeme Watanzania na kuliingiza taifa katika hasara ya kulipa Sh. bilioni tatu kila ziku za kununua mafuta ya mitambo ya kuzalisha umeme, badala ya kuzungumzia mambo yasiyo na tija ya nani kampa nani mkataba.
Alisema shirika halina mhandisi hata mmoja mwenye utaalamu wa kufanya matengenezo ya umeme bila kuuzima, na kusema kuwa yuko tayari kutoa Sh. milioni 10 kwa atakayejitokeza.
Wakili Lukalo jana hakupatikana kuzungumzia kampuni hiyo kutokubaliana na maamuzi yake.
Meneja wa Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, alipoulizwa kama wamepata taaarifa kuwa uamuzi huo utapingwa mahakamani, alisema Mwakamele ameshashindwa kesi na anapaswa kuwalipa.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment