Familia ya Waingereza, Kirstie Trup na
Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18, waliomwagiwa tindikali huko
Zanzibar, wameiomba Serikali ya Uingereza kuishinikiza Tanzania
kuharakisha kuwawajibisha waliohusika na tukio hilo.
Waingereza hao ambao walikuwa walimu
wa kujitolea katika shule ya St Monica, Tomondo, Zanzibar, walimwagiwa
tindikali na watu wawili wasiojulikana wakati walipokuwa kwenye
matembezi ya jioni katika eneo la Mji Mkongwe Agosti 7, mwaka huu.
Baada ya tukio hilo lililowajeruhi
kiasi kikubwa katika maeneo ya kifua na mikononi, walipewa matibabu
katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, kisha wakarudishwa kwao kwa
matibabu zaidi.
Alipowatembea wasichana hao
hospitalini, Rais Jakaya Kikwete alisema tukio hilo limetia aibu kwa
mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha linawakamata na
kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.
Taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao
wa habari wa Polisi wa Kimataifa (Interpol) Kanda ya Tanzania, inaeleza
kuwa familia ya wasichana hao hairidhishwi na namna Serikali ya Tanzania
inavyolishughulikia suala hilo kwa kuwa hadi sasa imeshindwa kuwatambua
wahusika.
Mtandao huo umemnukuu baba yake Trup,
Marc alipokuwa akizungumza na Redio 4 ya BBC, kuwa kuna wingu zito
lililotanda kuhusu kesi hiyo, kwa kuwa hadi sasa Serikali ya Zanzibar
imeshindwa kuonyesha picha za wahusika ili zitambuliwe na wasichana hao,
ingawa imekwisha kuwahoji watu kadhaa.
"Picha haziwezi kutumwa katika muundo
bora unaokubaliwa na Interpol au Mamlaka za Uingereza, kutokana na
sababu hizo hakuna hata mmoja ameshaziona hizo picha," alisema Marc.
Naye baba mlezi wa Gee, Doug Morris,
alisema: "Kama Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Jumuiya ya Madola wako
makini kusaidia watu hao kufikishwa mbele ya sheria kwa niaba ya raia
wa Uingereza, tulitegemea wafanye kila linalowezekana, lakini hakuna
dalili zozote zinazoonekana za kutaka kuharakisha jambo hili."
Aliongeza:"Kama wanamaanisha
wanachokisema na ni muhimu kwao kuwatafuta waliotekeleza kitendo hicho
ili wawafikishe kwenye vyombo vya sheria, basi watusaidie kwa kila njia
ambayo wanaweza.
"Kila mtu ameanza kufikiri kuwa
wanatuchezea, kila wiki tunakatishwa tamaa. Huu ni uharibifu ambao
hauwezi kupita tu bila mtu kuadhibiwa kwa manufaa ya wasichana wale au
mtu mwingine yeyote.
"Aina gani ya ujumbe unaoletwa, kwamba unaweza kufanya jambo baya halafu usifanywe kitu chochote?"
Alisema kuwa wangependa suala hilo lifike mwisho haraka iwezekanavyo ili haki itendeke.
Familia hiyo inasema kuwa hadi sasa
haijafahamu sababu ya wasichana hao kushambuliwa kwa tindikali, kwa kuwa
muda wote walipokuwa Zanzibar walionyesha tabia njema na kuvaa mavazi
ya heshima.
Mzazi huyo wa Trup aliongeza kuwa:
"Ninadhani mamlaka za Tanzania haziyachukulii masuala ya mambo ya nje ya
nchi kwa umakini unaotakiwa, tunataka ifanye kazi.
"Wasichana wanataka kujua kama tukio lile lilitokana na rangi yao au dini kwasababu hawajui ni kwa nini lilitokea."
Akizungumzia maendeleo ya afya ya
binti yake, alisema kuwa Kirstie anaendelea vizuri na kwamba amesharudi
chuoni kuendelea na masomo yake, ingawa bado anakwenda hospitali kupata
matibabu.
"Anavaa vazi maalumu la kufunika
makovu aliyoyapata, atafanya hivyo saa 23 kwa mwaka mzima. Ingawa
anaendelea vizuri kimwili na kiakili, bado anapita katika kipindi
kigumu," alisema.
Akielezea maendeleo ya kiafya ya
Katie, Morris alisema kuwa naye anaendelea na matibabu na kwamba hali
yake inaendelea kuimarika.
Danadana za Polisi
Alipoulizwa maendeleo ya kesi hiyo,
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema kuwa jalada la tukio
hilo lipo Zanzibar, hivyo mwandishi awasiliane na Kamishna wa Jeshi la
Polisi Zanzibar kupata ufafanuzi.
Hata hivyo, alipopigiwa Kamishna wa
Polisi Zanzibar, CP Mussa Ali Mussa simu zake zote mbili ziliita bila
kupokewa. Alipotafutwa Ofisa Habari Mkuu Jeshi la Polisi Zanzibar, INSP
Mohammed Mhina alisema kuwa kuna kesi nyingi za matukio ya watu
kumwagiwa tindikali yaliyotokea Zanzibar ambayo yatatolewa ufafanuzi
yote kwa wakati mmoja.
"Matukio ya kumwagiwa tindikali yapo
mengi, hata hilo unalolizungumzia ninalikumbuka, ni vyema hayo yote
yakazungumzwa kwa wakati mmoja," alisema na kuongeza kuwa apigiwe simu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, kwa
kuwa ndiye anayelijua vizuri jambo hilo.
Kwa upande wake, Mkadam alisema suala hilo halipo tena mikononi mwake kwa kuwa lilishapelekwa kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Mwananchi lilimtafuta Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Yusuf Ilembo, lakini simu zake ziliita bila majibu.
Kauli ya Dk Shein
Akihutubia Baraza la Idd Fitr mwaka
huu mjini Zanzibar, Rais wa visiwa hivyo, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema
serikali yake itahakikisha inawasaka na kuwafikisha mahakamani
waliopanga na kufanya shambulio hilo.
Chanzo:Mwananchi


Post a Comment