Majeruhi wakiwa kwenye gari la wagonjwa kwenye mapokezi ya Hospitali ya
Rufani ya KCMC Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kupata ajali ya basi la
Osaka kwenye Kijiji cha Kirinjiku, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro
jana. Picha na Dionis NyatoKilimanjaro na Manyara.Watu
saba wamefariki dunia na wengine 71 kujeruhiwa kwenye ajali ya
iliyohusisha mabasi ya abiria mikoa ya Kilimanjaro na Manyara.
Ajali iliyotokea Mkoa wa Manyara, basi la abiria
maarufu Polepole liligongana na trekta na bajaji eneo la Makatanini,
Wilaya ya Babati. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Mussa Marambo
alisema ajali hiyo ilitokea Desemba 7, mwaka huu saa 2:00 usiku wakati
basi hilo likitokea mkoani Arusha.
Marambo alisema chanzo cha ajali hiyo ni trekta
kuegeshwa katikati ya barabara bila alama yoyote ya tahadhari. Basi la
abiria aina ya Fusso, mali ya Issack Polepole liligongana na trekta hiyo
ambayo haikuwa na namba za usajili aina ya Swaraj, lilikuwa
likiendeshwa na Clement Tuji.
Alitaja waliokufa kuwa ni Shaibu Olae (25),
Nicodemu Mofuru (27) mkazi wa Majengo Mapya na Mwalimu wa Sekondari ya
Aldersgate, Charles Exaud na mwanamke ambaye hakufahamika.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro, watu watatu wamefariki
dunia papohapo na wengine 39 kujeruhiwa, baada ya basi walilokuwa
wakisafiria kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam kupoteza mwelekeo kabla
ya kuacha njia na kupinduka.
Ajali hiyo iliyotokea jana saa 3:30 asubuhi eneo
la Kirinjiko, Wilaya ya Same, ilihusisha basi la abiria mali ya Kampuni
ya Osaka Coach.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Naye Katibu wa Hospitali ya Wilaya ya Same,
Mwajuma Nyika alisema hali za baadhi ya majeruhi wanaopata ni mbaya na
kwamba uongozi wa wilaya umetoa magari manne ya dharura kwa ajili ya
kuokoa roho za majeruhi wa ajali hiyo.
Post a Comment