WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amelipongeza Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha kwa
kubuni na kuunda Umoja wa Madhehebu ya Kikristu katika mkoa wa Arusha
kama njia ya kuleta amani na mshikamano kwa waumini wake.
Ametoa
pongezi hizo leo mchana (Jumapili, Desemba 29, 2013) wakati akitoa
salamu za Serikali kwenye ibada ya kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya
Jimbo Kuu Katoliki la Arusha iliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Kuu
la Mt. Theresia wa Mtoto Yesu jijini Arusha.
Waziri
Mkuu ambaye alishiriki ibada hiyo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete,
alisema uamuzi uliofanywa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la
Arusha, Mhashamu Josaphat Lebulu ni wa kuigwa na viongozi wa mikoa
mingine kwani unasaidia kuwaunganisha viongozi wote bila kujali tofauti
zao.
“Kwa
kweli ninampongeza Baba Askofu Lebulu kwa ubunifu wake wa kuunda umoja
huu, yeye kama Mwenyekiti ni kiunganishi kikubwa katika kukuza ukristu
bila kujali tofauti zao. Sisi kama Serikali umetusaidia sana.
Tutawahimiza viongozi wengine waige mfano wako badala kuwa wanapigana
vikumbo kila kukicha,” alisema.
Alisema
kazi inayofanywa na Kanisa ya kubadilisha mwelekeo wa watu mbalimbali
na kupata waumini wenye hofu ya Mungu kwa kiasi kikubwa inaisaidia
Serikali kwani nayo pia inakuwa imepata raia wema.
Aliwasihi
viongozi wa dini wa mkoa huo waimarishe umoja wao na ikibidi watoke nje
ili kuwavuta watu wa dini nyingine kwenye umoja wao huku akisisitiza
umuhimu wa kuilinda amani ambayo alisema ni tunu ya Taifa.
Mapema,
akitoa salamu za pongezi kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa
Madhehebu ya Kikristu mkoani humo, Askofu Hotay wa Kanisa la Anglikana,
Askofu Oral Sosy wa Kanisa la TAG Arusha ambaye pia ni Katibu wa Umoja
huo, alisema umoja huo umeundwa na makanisa yaliyo chini ya Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Kikristu Tanzania (CCT) na
Umoja wa Makanisa ya Pentekoste.
Alisema
umoja huo unakazi kubwa tatu ambazo ni kuhubiri amani, kuombea Serikali
pamoja na nchi ya Tanzania na kuangalia masuala ya kijamii. “Sisi
tunafanya kwa uaminifu kazi ya kuiombea nchi na viongozi wake kwa sababu
tumeagizwa katika maandiko.”
Kuhusu
masuala ya kijamii, Askofu Sosy alisema wanafuatilia kwa makini suala
la Katiba mpya na kuna mambo ambayo hawangependa yawemo kwenye Katiba
mpya. Aliyataja mambo hayo kuwa ni ndoa za jinsia moja, utoaji mimba na
masuala ya dini au dhehebu kuingizwa kwenye Katiba.
Kwa
mujibu wa Katibu Mtendaji wa TEC, Padre Raymond Saba ibada hiyo ambayo
iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama
Polycarp Kardinali Pengo ilihudhuriwa na Maaskofu 17 na mapdri zaidi ya
80.
Naye Mwakilishi
wa Baba Mtakatifu hapa nchini, Askofu Mkuu Fransisco Padilia alisema
udugu ni msingi wa njia ya amani na msingi huo unapaswa kuanzia katika
kanisa. Alisema siasa na uchumi visiishie kwenye ujenzi wa kiteknolojia
uliotelekeza tunu na hatma ya kazi za kibinadamu bali viwe mwanga wa
kuondoa chuki na husuda na badala yake vilete upendo.
Aliwataka
waumini waliohudhuria ibada hiyo wazidi kuwa na upendo na umoja.
“Jubilei hii iwe kichocheo cha udugu… isaidie kujenga amani na kuleta
haki. Ninawasihi mbaki mkiwa wamoja, muheshimu mawazo ya wengine,
muwasaidie zaidi wengine, muonyeshe upendo zaidi, msamaha zaidi na
ushirikiano zaidi,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 29, 2013
Post a Comment