Aliyoandika. Dr.Kitila Mkumbo kwenye gazeti la Raia mwema.
********************
Tunahitaji mbadala wa CCM, CHADEMA
Kitila Mkumbo
Toleo la 334
15 Jan 2014
ITACHUKUA muda kuelewa nini hasa
kilichokikumba Chama Kikuu cha
Upinzani nchini (CHADEMA) hadi
kikashindwa kutatua mgogoro wa
uongozi na hatimaye kuingiza nchi
katika kizungumkuti cha kisiasa
tunachokishuhudia leo. Binafsi, kama
mmoja ya wahusika wakubwa katika
mgogoro huu nimepokea pole, lawama,
na kwa kiasi fulani hongera kwa
kumudu kuhimili mikikimikiki
iliyonikumba. Nimepokea pole
kutokana na misukosuko
niliyokumbana nayo katika sakata hili
hadi kufikia kufukuzwa uanachama.
Hili si jambo dogo katika maisha ya
binadamu. Kufukuzwa katika ushirika
wowote ni jambo linalosababisha
mfadhaiko na ninazipokea pole
nilizopewa kwa unyenyekevu.
Ninashukuru pia kwa wale walionitia
moyo kwamba hii ni ajali katika safari
na nisikate tamaa katika kutoa
mchango wangu katika harakati za
mabadiliko ya kisiasa nchini. Nami
nawaahidi kwamba bado nipo imara na
nitaendelea kushiriki kikamilifu katika
harakati za kuleta mabadiliko ya
kisiasa hapa nchini, ndani na nje ya
vyama vya siasa.
Walionipa lawama ni wale
waliokubaliana mia kwa mia na
viongozi wa CHADEMA waliotujengea
taswira ya usaliti na uhaini kwa chama
kwa uamuzi wetu wa kuandaa mkakati
wa kushinda uchaguzi ndani ya
CHADEMA; mkakati ambao ulikuja
kutafsiriwa kama mkakati wa
mapinduzi ya uongozi halali ndani ya
chama. Na kwa kuwa viongozi
waliongea sana na kulirudia jambo hili
mara kwa mara, na kwa kuwa jamii
yetu imejengwa katika kuamini uongozi
zaidi kuliko mtu mwingine yeyote,
wapo watu wengi ambao wameafikiana
na tafsiri ya uongozi kwamba waraka
ule ulikuwa ni mkakati wa mapinduzi
na haukuwa na nia njema.
Wapo pia wananchi walionilaumu kama
sehemu ya uongozi wa chama kwa
kushindwa kuyamaliza mambo yetu
ndani ya chama. Na wengine
wamenilaumu kwa kutokuwa na moyo
wa kubali yaishe, kwamba ningekubali
kosa, hata kama siamini kwamba ni
kosa, ili niombe msamaha yaishe,
tusonge mbele. Natamani ingekuwa
rahisi hivi na kwamba kungekuwa na
nia njema kwa pande zote mbili,
pengine neno samahani lingetosha
kumaliza mgogoro huu.
Kwa sababu hii nazipokea lawama zote
kwa unyenyekevu pia na ninakubali
kwamba nimeshiriki, bila kutarajia,
kusababisha usumbufu na kutatiza
tamanio na tumaini la mamilioni ya
Watanzania katika kuitoa CCM
madarakani. Hata hivyo, taswira ya
mgogoro huu ni pana kuliko
inavyoonekana na pengine tutapata
nafasi nzuri zaidi mbele kueleza vizuri
kilichotokea katika maandishi ili watu
waelewe na waielewe CHADEMA na
viongozi wake vizuri, na kuweka
kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.
Sitarajii katika makala haya kukidhi kiu
ya watu wengi wanaotamani kujua
ukweli wa mgogoro ndani ya
CHADEMA na pengine mimi siye mtu
sahihi kueleza jambo hili kwa kuwa
nina maslahi ya moja kwa moja.
Ninatoa changamoto kwa watafiti wa
sayansi ya siasa kulifanyia utafiti
jambo hili na kuliweka bayana, ili watu
wapate kujifunza na kulijua vizuri.
Nieleze tu kwamba mgogoro huu
unatukumbusha kuwa, pamoja na
kwamba tupo katika mfumo wa vyama
vingi, bado tumeendelea kuukumbatia
utamaduni wa chama kimoja. Kwa hiyo
tuna vyama vingi vya siasa, lakini
vyama hivi bado vinakumbatia
utamaduni wa chama kimoja.
Utamaduni wa chama kimoja ni
utamaduni hodhi na wa kiimla. Uongozi
katika utamaduni wa chama kimoja
unapatikana kwa njia za uteule,
ukiwahusisha watu wachache wateule.
Utamaduni wa chama kimoja unakataa
ushindani wa wazi. Katika utamaduni
wa chama kimoja kutamani cheo fulani
ndani ya chama na katika serikali ni
ulafi na uroho wa madaraka. Ndio
maana vyama vyetu vyote vikubwa
hapa nchini vinakataza na kukemea
wanachama wao kutamani na
kutangaza nia ya kuwania madaraka
makubwa kama vile urais au uenyeviti
wa vyama.
Kutamani madaraka peke yake
kunakatazwa, achilia mbali kuandaa
mkakati wa kushinda nafasi
unayoitamani. Na hili ndilo kosa
tulilolifanya. Tulikuwa wajinga sana
kudhani kwamba tupo katika mfumo na
utamaduni wa vyama vingi ambapo
mtu yupo huru kutamani cheo
chochote katika chama chake cha
siasa, na kutengeneza mikakati ya
kushinda cheo hicho katika uchaguzi
huru ndani ya chama. Tulikuwa wajinga
kwa kujaribu kuachana na utamaduni
wa kuvizia cheo na kujifanya hutaki
wakati unataka.
‘Msaliti’ mwenzetu Zitto Kabwe alianza
siku nyingi mwaka 2009 kwa uamuzi
wake wa kugombea uenyekiti wa
chama bila kupata ridhaa ya wazee wa
chama. Alikuwa mjinga kudhani
kwamba uongozi katika mfumo wa
chama kimoja unapatikana kwa kujaza
fomu na kuomba kura. Nami nilikuwa
mjinga nisiyeelewa kwa kumuunga
mkono na kumtaka asonge mbele
katika nia yake hiyo. Hakuishia hapo,
Zitto Kabwe akafanya ujinga mwingine
kwa kutamani na hatimaye kutangaza
kugombea urais kupitia chama chake.
Huu nao ulikuwa ni usaliti kwa
utamaduni wetu wa chama kimoja, kwa
sababu katika utamaduni huu nafasi
kama hii ni ya kiteule na wateule na
wateuaji wapo.
Ninapokubali kupokea lawama katika
kushiriki kusababisha mgogoro
unaoendelea ndani ya CHADEMA,
naomba nami niwarushie lawama tele
wanachama na mashabiki wa chama
hiki, na wapenda mabadiliko kwa
ujumla. Nawarushia lawama
wanachama na washabiki wa
CHADEMA kwa kuwashabikia viongozi
wa chama chao katika kukinyonga
chama. Viongozi wa chama hiki
wamefanya makosa mengi na
makubwa hadi kusababisha mgogoro
ufike ulipofika, lakini wanachama na
mashabiki wa chama wamekuwa
wakishwashangilia katika kila hatua
walioifanya. Kwa hiyo lawama ya
kwanza kwa wanachama na mashabiki
ni pale walipokubali kugeuzwa kuwa
mashabiki wa viongozi ndani ya chama
badala ya kuwa mashabiki wa chama.
Na kwa kuwa ushabiki hupofusha
macho na akili, mashabiki wa viongozi
hawatofautishi kati ya uongozi na
chama. Ni kama vile wamedanganywa
na viongozi waliopo na wakakubali
kudanganyika, kwamba uongozi wa
chama ndio chama, na chama ndio
uongozi!
Ni kwa sababu ya ushabiki kwa
viongozi, ndio maana ilifika mahala
wanachama na mashabiki wa
CHADEMA wakagawanyika katika
makundi ya washabikia viongozi, na
chama kikakosa watu wa kukishabikia
na hapo kikajikuta hakina mlinzi.
Makosa yaliyofanywa na uongozi na
wanachama wa CHADEMA unafanana
sana na makosa yaliyofanywa na
viongozi na wanachama wa NCCR
Mageuzi miaka ya tisini. Kama
inavyotokea kwa CHADEMA leo,
wanachama wa NCCR Mageuzi
waligeuka kuwa mashabiki wa
viongozi, kundi moja likimshabikia
Mrema na kundi jingine likiwashabikia
akina Marando. Kwa kudhani kwamba
chama kilikuwa imara sana, kundi la
akina Marando likaamua kumfukuza
Mrema likiamini kwamba alikuwa hana
madhara yoyote kwa sababu chama
kilishaimarika mno, wakisahau
kwamba msingi wa ufuasi ulijengwa
kwa viongozi na sio kwa chama.
Mrema alipotimka, akatimka na
mashabiki wake. Hicho ndicho
kinachoendelea ndani ya CHADEMA.
Kuna watu wenye mtazamo finyu
wanaamini kwamba chama hiki ni
imara sana kwa sasa kiasi kwamba
hata wakimfukuza Zitto kitaendelea
kubaki imara. Wamesahau kwamba
wamejenga ufuasi kwa viongozi, na
hivyo watakapomfukuza Zitto atatimka
na wafuasi wake na chama kitayumba.
Wangekuwa na mtazamo mpana wa
kimantiki, na kama wangekuwa ni watu
wa kujifunza, viongozi wa CHADEMA
wangelimaliza sakata la Zitto ambalo
sasa lipo mahakamani kwa njia ya
usuluhishi kimya kimya kama
walivyofanya NCCR kwa Kafulila. Lakini
kwa sababu ya upofu unaoendelea
unaotokana na kugubikwa na ulevi wa
utamaduni wa chama kimoja kwa
upande mmoja, na ulevi wa umaarufu
kwa upande mwingine, hawatakubali
yaishe nje ya Mahakama, na hatimaye
watamfukuza Zitto. Wakishakumfukuza
Zitto atatimka na mashabiki wake,
chama kitayumba na kutoa unafuu kwa
CCM. Katika mazingira haya tunahitaji
sana mbadala wa CCM na CHADEMA.
Itaendelea wiki ijayo..
********************
Tunahitaji mbadala wa CCM, CHADEMA
Kitila Mkumbo
Toleo la 334
15 Jan 2014
ITACHUKUA muda kuelewa nini hasa
kilichokikumba Chama Kikuu cha
Upinzani nchini (CHADEMA) hadi
kikashindwa kutatua mgogoro wa
uongozi na hatimaye kuingiza nchi
katika kizungumkuti cha kisiasa
tunachokishuhudia leo. Binafsi, kama
mmoja ya wahusika wakubwa katika
mgogoro huu nimepokea pole, lawama,
na kwa kiasi fulani hongera kwa
kumudu kuhimili mikikimikiki
iliyonikumba. Nimepokea pole
kutokana na misukosuko
niliyokumbana nayo katika sakata hili
hadi kufikia kufukuzwa uanachama.
Hili si jambo dogo katika maisha ya
binadamu. Kufukuzwa katika ushirika
wowote ni jambo linalosababisha
mfadhaiko na ninazipokea pole
nilizopewa kwa unyenyekevu.
Ninashukuru pia kwa wale walionitia
moyo kwamba hii ni ajali katika safari
na nisikate tamaa katika kutoa
mchango wangu katika harakati za
mabadiliko ya kisiasa nchini. Nami
nawaahidi kwamba bado nipo imara na
nitaendelea kushiriki kikamilifu katika
harakati za kuleta mabadiliko ya
kisiasa hapa nchini, ndani na nje ya
vyama vya siasa.
Walionipa lawama ni wale
waliokubaliana mia kwa mia na
viongozi wa CHADEMA waliotujengea
taswira ya usaliti na uhaini kwa chama
kwa uamuzi wetu wa kuandaa mkakati
wa kushinda uchaguzi ndani ya
CHADEMA; mkakati ambao ulikuja
kutafsiriwa kama mkakati wa
mapinduzi ya uongozi halali ndani ya
chama. Na kwa kuwa viongozi
waliongea sana na kulirudia jambo hili
mara kwa mara, na kwa kuwa jamii
yetu imejengwa katika kuamini uongozi
zaidi kuliko mtu mwingine yeyote,
wapo watu wengi ambao wameafikiana
na tafsiri ya uongozi kwamba waraka
ule ulikuwa ni mkakati wa mapinduzi
na haukuwa na nia njema.
Wapo pia wananchi walionilaumu kama
sehemu ya uongozi wa chama kwa
kushindwa kuyamaliza mambo yetu
ndani ya chama. Na wengine
wamenilaumu kwa kutokuwa na moyo
wa kubali yaishe, kwamba ningekubali
kosa, hata kama siamini kwamba ni
kosa, ili niombe msamaha yaishe,
tusonge mbele. Natamani ingekuwa
rahisi hivi na kwamba kungekuwa na
nia njema kwa pande zote mbili,
pengine neno samahani lingetosha
kumaliza mgogoro huu.
Kwa sababu hii nazipokea lawama zote
kwa unyenyekevu pia na ninakubali
kwamba nimeshiriki, bila kutarajia,
kusababisha usumbufu na kutatiza
tamanio na tumaini la mamilioni ya
Watanzania katika kuitoa CCM
madarakani. Hata hivyo, taswira ya
mgogoro huu ni pana kuliko
inavyoonekana na pengine tutapata
nafasi nzuri zaidi mbele kueleza vizuri
kilichotokea katika maandishi ili watu
waelewe na waielewe CHADEMA na
viongozi wake vizuri, na kuweka
kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.
Sitarajii katika makala haya kukidhi kiu
ya watu wengi wanaotamani kujua
ukweli wa mgogoro ndani ya
CHADEMA na pengine mimi siye mtu
sahihi kueleza jambo hili kwa kuwa
nina maslahi ya moja kwa moja.
Ninatoa changamoto kwa watafiti wa
sayansi ya siasa kulifanyia utafiti
jambo hili na kuliweka bayana, ili watu
wapate kujifunza na kulijua vizuri.
Nieleze tu kwamba mgogoro huu
unatukumbusha kuwa, pamoja na
kwamba tupo katika mfumo wa vyama
vingi, bado tumeendelea kuukumbatia
utamaduni wa chama kimoja. Kwa hiyo
tuna vyama vingi vya siasa, lakini
vyama hivi bado vinakumbatia
utamaduni wa chama kimoja.
Utamaduni wa chama kimoja ni
utamaduni hodhi na wa kiimla. Uongozi
katika utamaduni wa chama kimoja
unapatikana kwa njia za uteule,
ukiwahusisha watu wachache wateule.
Utamaduni wa chama kimoja unakataa
ushindani wa wazi. Katika utamaduni
wa chama kimoja kutamani cheo fulani
ndani ya chama na katika serikali ni
ulafi na uroho wa madaraka. Ndio
maana vyama vyetu vyote vikubwa
hapa nchini vinakataza na kukemea
wanachama wao kutamani na
kutangaza nia ya kuwania madaraka
makubwa kama vile urais au uenyeviti
wa vyama.
Kutamani madaraka peke yake
kunakatazwa, achilia mbali kuandaa
mkakati wa kushinda nafasi
unayoitamani. Na hili ndilo kosa
tulilolifanya. Tulikuwa wajinga sana
kudhani kwamba tupo katika mfumo na
utamaduni wa vyama vingi ambapo
mtu yupo huru kutamani cheo
chochote katika chama chake cha
siasa, na kutengeneza mikakati ya
kushinda cheo hicho katika uchaguzi
huru ndani ya chama. Tulikuwa wajinga
kwa kujaribu kuachana na utamaduni
wa kuvizia cheo na kujifanya hutaki
wakati unataka.
‘Msaliti’ mwenzetu Zitto Kabwe alianza
siku nyingi mwaka 2009 kwa uamuzi
wake wa kugombea uenyekiti wa
chama bila kupata ridhaa ya wazee wa
chama. Alikuwa mjinga kudhani
kwamba uongozi katika mfumo wa
chama kimoja unapatikana kwa kujaza
fomu na kuomba kura. Nami nilikuwa
mjinga nisiyeelewa kwa kumuunga
mkono na kumtaka asonge mbele
katika nia yake hiyo. Hakuishia hapo,
Zitto Kabwe akafanya ujinga mwingine
kwa kutamani na hatimaye kutangaza
kugombea urais kupitia chama chake.
Huu nao ulikuwa ni usaliti kwa
utamaduni wetu wa chama kimoja, kwa
sababu katika utamaduni huu nafasi
kama hii ni ya kiteule na wateule na
wateuaji wapo.
Ninapokubali kupokea lawama katika
kushiriki kusababisha mgogoro
unaoendelea ndani ya CHADEMA,
naomba nami niwarushie lawama tele
wanachama na mashabiki wa chama
hiki, na wapenda mabadiliko kwa
ujumla. Nawarushia lawama
wanachama na washabiki wa
CHADEMA kwa kuwashabikia viongozi
wa chama chao katika kukinyonga
chama. Viongozi wa chama hiki
wamefanya makosa mengi na
makubwa hadi kusababisha mgogoro
ufike ulipofika, lakini wanachama na
mashabiki wa chama wamekuwa
wakishwashangilia katika kila hatua
walioifanya. Kwa hiyo lawama ya
kwanza kwa wanachama na mashabiki
ni pale walipokubali kugeuzwa kuwa
mashabiki wa viongozi ndani ya chama
badala ya kuwa mashabiki wa chama.
Na kwa kuwa ushabiki hupofusha
macho na akili, mashabiki wa viongozi
hawatofautishi kati ya uongozi na
chama. Ni kama vile wamedanganywa
na viongozi waliopo na wakakubali
kudanganyika, kwamba uongozi wa
chama ndio chama, na chama ndio
uongozi!
Ni kwa sababu ya ushabiki kwa
viongozi, ndio maana ilifika mahala
wanachama na mashabiki wa
CHADEMA wakagawanyika katika
makundi ya washabikia viongozi, na
chama kikakosa watu wa kukishabikia
na hapo kikajikuta hakina mlinzi.
Makosa yaliyofanywa na uongozi na
wanachama wa CHADEMA unafanana
sana na makosa yaliyofanywa na
viongozi na wanachama wa NCCR
Mageuzi miaka ya tisini. Kama
inavyotokea kwa CHADEMA leo,
wanachama wa NCCR Mageuzi
waligeuka kuwa mashabiki wa
viongozi, kundi moja likimshabikia
Mrema na kundi jingine likiwashabikia
akina Marando. Kwa kudhani kwamba
chama kilikuwa imara sana, kundi la
akina Marando likaamua kumfukuza
Mrema likiamini kwamba alikuwa hana
madhara yoyote kwa sababu chama
kilishaimarika mno, wakisahau
kwamba msingi wa ufuasi ulijengwa
kwa viongozi na sio kwa chama.
Mrema alipotimka, akatimka na
mashabiki wake. Hicho ndicho
kinachoendelea ndani ya CHADEMA.
Kuna watu wenye mtazamo finyu
wanaamini kwamba chama hiki ni
imara sana kwa sasa kiasi kwamba
hata wakimfukuza Zitto kitaendelea
kubaki imara. Wamesahau kwamba
wamejenga ufuasi kwa viongozi, na
hivyo watakapomfukuza Zitto atatimka
na wafuasi wake na chama kitayumba.
Wangekuwa na mtazamo mpana wa
kimantiki, na kama wangekuwa ni watu
wa kujifunza, viongozi wa CHADEMA
wangelimaliza sakata la Zitto ambalo
sasa lipo mahakamani kwa njia ya
usuluhishi kimya kimya kama
walivyofanya NCCR kwa Kafulila. Lakini
kwa sababu ya upofu unaoendelea
unaotokana na kugubikwa na ulevi wa
utamaduni wa chama kimoja kwa
upande mmoja, na ulevi wa umaarufu
kwa upande mwingine, hawatakubali
yaishe nje ya Mahakama, na hatimaye
watamfukuza Zitto. Wakishakumfukuza
Zitto atatimka na mashabiki wake,
chama kitayumba na kutoa unafuu kwa
CCM. Katika mazingira haya tunahitaji
sana mbadala wa CCM na CHADEMA.
Itaendelea wiki ijayo..
Post a Comment