Bahati
(katikati) akiwa hospitalini na baadhi ya wajeruhiwa wa mgogoro baina
ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kiteto.Picha na Musa Juma
*******
Kiteto:Bahati
ni kweli ana bahati kama jina lake lilivyo Bahati. Katika mapigano,
yaliyotokea hivi Karibuni, mtoto, Bahati Juma alikuwa ni mmoja wa watu
waliojikuta wako katikati ya mapigano hayo.
Mtoto
huyu anasema alikamatwa na kundi la wafugaji wa Kimasai, akiwa ndani ya
nyumba yao iliyochomwa moto. Katika tukio hilo, Bahati alinusurika kufa
ingawa tayari sime ilikuwa imeanza kukata shingo yake.
Hivi sasa
Bahati amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara,
akiuguza jeraha la kukatwa na sime na ameshonwa nyuzi nane huku akiwa na
majeraha ya fimbo mgongoni na mikononi.
Ndugu
zake watatu ambao ni wakulima wote kutoka mkoani Dodoma, wameuawa ambao
ni Juma Mlangwa (47) na Yohana Hivo (33) waliuawa papohapo na Mussa
Juma alifariki akiwa hospitali.
Katika
mapigano hayo yaliyotokea Desemba 21 Kijiji cha Olpopong, wakulima
wengine wanane walijeruhiwa, mmoja alikuwa mahututi. Mussa Juma ambaye
alichomwa mkuki wa mbavu, alihamishiwa hospitali ya Mkoa ya Dodoma,
alifariki baadaye.
Wengine
waliolazwa hospitali ya wilaya ya Kiteto ni Emanuel Mathias (26), Hoti
Damas (38), Mwajuma Hamis (20), Habiba Ally(16 ) na Mwajuma Martin(33).
Daktari azungumza
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Kiteto, Thomas Ndalio anasema, hali za majeruhi hao saba zinaendelea vizuri.
“Mussa
ndio hali yake ilikuwa mbaya sana na ndio sababu alihamishiwa Hospitali
ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi, kwa bahati mbaya
alifariki,”anasema Dk Ndalio.
Bahati asimulia alivyonusurika kifo
Anasema, anakumbuka Desemba 21 alikuwa nyumbani na ndugu zake, wakiwa wamepumzika baada ya kutoka shamba kulima.
Siku hiyo
anakumbuka kulikuwa kumezuka mgogoro katika eneo la malisho kati ya
wakulima na wafugaji wa jamii ya Kimasai. Wafugaji hao walikuwa
wameingiza katika mashamba yao, mifugo na walifanikiwa kuwafukuza.
Hata hivyo, anasema ilionekana wafugaji hao, walikasirishwa na kufukuzwa lakini waliondoka na hasira.
“Sasa
mimi nikiwa ndani ghafla nilisikia nje watu wakisema kuna vita! kuna
vita!. Nilipotaka kutoka, tayari nyumba yetu ilikuwa imeshika moto,”
anasema Bahati.
Anasema
aliamua kutoka mbio ili kujiokoa, lakini alijikuta yuko mikononi mwa
wafugaji wa kimasai, walimkamata na kuanza kumkata na sime huku wengine
wakimchapa.
“Wakati
wanaendelea kutaka kunichinja ndugu zangu wengine walijitokeza, ugomvi
ulikuwa mkubwa na hapo niliona wenzangu wawili wakiuawa kwa kuchomwa
mikuki na kukatwa sime”anasema Bahati.
Anasema baada ya tukio hilo, wafugaji waliendelea kuchoma nyumba zao, baadaye wakaondoka huku wakionya wasisumbuliwe.
“Wakati
huo mimi nilikuwa chini nalia, damu zilikuwa zinanivuja, baadaye
nilichukuliwa na kuletwa hapa hospitalini,”anasema Bahati huku
akisisitiza kuwa Serikali ikomeshe haraka mgogoro huo.
Aomba Serikali kumaliza mgogoro
Bahati
anaomba Serikali, kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo, kwani
hali ya usalama sio nzuri katika kijiji cha Olpopong wanachoishi.
“Tunaomba tu watusaidie tukae kwa amani na hawa wafugaji,“anasema Bahati kwa uchungu.
Anasema
kama amani ikipatikana katika eneo lao, atarejea kuishi, lakini kwa sasa
bado ana hofu kwani bado hajui ndugu zake wengine wamekimbilia wapi.
Chanzo cha mapigano
Saitoti
Kalanga, ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Olpopong kilichotokea mapigano
baina ya wakulima na wafugaji na kusababisha vifo vya watu wawili,
anasema chanzo cha mapigano hayo ni watu kuvamia ardhi ya kijiji bila
kufuata mpango wa matumizi bora ya ardhi na kila wanapotakiwa kuondoka
wamegoma.
Anasema
watu hao wakiwemo wakulima wamejianzishia vitongoji batili ndani ya
kijiji. Katika maeneo wanayolima wamekuwa wakikamata mifugo inayopita na
kuikatakata kwa mapanga jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwa zaidi ya
miaka miwili sasa.
“Wakulima
ni wavamizi, hawatambui Serikali ya kijiji, wameingia tu kwa nguvu na
wanalima kwa kukata miti ovyo jambo ambalo limewaudhi wafugaji,”anasema
Kalanga.
Kalanga
anasema kijiji hicho, kilichosajiliwa mwaka 1993, kina mpango wa
matumizi ya ardhi, uliopitishwa na halmashauri tangu mwaka 2010, lakini
umekuwa haufuatwi baada ya wakulima kuvamia.
Mwenyekiti
huyo anaonyesha ramani ya mpango wa matumizi ya ardhi katika kijiji
hicho; ekari 2880 zilitengwa kwa kilimo, hekari 1, 450 kwa makazi, ekari
9184 kwa malisho na ekari 9805 hifadhi ya jamii.
“Hivi
sasa ardhi ya malisho na hifadhi imevamiwa na wakulima kutoka Mkoa wa
Dodoma, ndiyo sababu kumeibuka mapigano,”anasema Kalanga.
Naye
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Eseriani, ambacho mapigano yametokea, Mariam
Ijumaa, anasema kumekuwepo na uvamizi wa wakulima katika kitongoji
chake, anaamini suluhu ni kuwagawia ardhi.
“Uvamizi
unaongezeka na hawa wanaokuja hawataki hata kutambua Serikali ya kijiji,
wameanzisha vitongoji vyao porini,”anasema Ijumaa.
Waeleza suluhu ya mgogoro huo
Saitoti
Kalanga, Mariam Ijumaa na Alaisi Nangoro, wakazi wa eneo hilo wanasema
suluhu ya mgogoro ulioibuka katika kijiji hicho ni kufuatwa mpango wa
matumizi bora ya ardhi.
Nangoro
anasema kwa kuwa tayari kijiji hicho kilipimwa, ni busara Serikali
ikasaidia kufuatwa mpango halali; kama kuna wakazi wasio na ardhi
wapewe.
“Tunapaswa
kuishi kwa amani, mapigano yaliyozuka hapa yasitokee tena, ni muhimu
kuheshimu mamlaka za vijiji kwa wale wanaotaka ardhi,”anasema Nangoro.
na mkazi wa kijiji hicho,
Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara
Mkuu wa
Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo, anaeleza Serikali kusikitishwa na hali
ya mapigano ya ardhi katika wilaya ya Kiteto na hadi kufikia watu watatu
kufariki ndani ya wiki moja na wengine wanane kujeruhiwa.
Mbwilo
anaagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kusaidia vijiji kuondokana na
mapigano ikiwamo kupanga matumizi bora ya ardhi na kuwaondoa wavamizi.
“Haiwezekani watu wavamie tu ardhi kama hakuna viongozi, ni lazima
tufuate sheria,” anasema.
Chanzo;Mwananchi
Post a Comment