Balozi
wa Tanzania Nchini Marekani na Canada Balozi Liberata Mula mula
akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kwa mazungumzo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi
wa Tanzania Nchini Marekani na Canada Balozi Liberata Mula mula hapo
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Mula mula
akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR)
******
Na Othman Ame OMPR.
Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imepongezwa kwa hatua iliyochukuwa ya kusherehekea miaka
50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kwa mafanikio makubwa na ya
kupigia mfano.
Pongezi hizo
zimetolewa na Balozi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Nchini Marekani na Canada Balozi Liberata Mulamula wakati akizungumza na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini
kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Liberata Mula
mula alisema maadhimisho hayo yaliyofikia nusu Karne yameijengea
Historia kubwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika muelekeo wa
maendeleo ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.
Alisema Mataifa mbali
mbali duniani yameendelea kushuhudia hatua kubwa zilizofikiwa na
Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo akiitaja baadhi yake imo
katika sekta ya Afya, Maji, Mawasiliano ambayo tayari imeshajengewa
miundo mbinu imara.
“ Huu ni mwaka wa
Kihistoria kwa Zanzibar na Tanzania katika kuadhimisha miaka 50 ya
Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964. Sasa kinachowapaswa
wananchi na viongozi wote kuhakikisha historia hii inaendelezwa zaidi
katika misingi ile ile ya amani na utulivu “. Alisema Balozi Liberata
Mula mula.
Balozi Mula mula
alielezea kwamba katika muelekeo wa kujiandaa na sherehe za maadhimisho
ya kutimia miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Uongozi wa
Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani na Canada tayari uko
mbioni kujiandaa na tamasha kubwa litakalolenga kutangaza maendeleo
yaliyofikiwa na Tanzania katika kipindi hicho.
Alisema Ofisi yake
iko wazi na huru wakati wote kujumuisha pamoja na taasisi mbali mbali
ziwe za Serikali au Binafsi katika kuchangia na hatimae kufanikisha
Tamasha hilo muhimu katika kuitangaza Tanzania kiuwekezaji.
Akizungumzia kuhusu
ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Mjini Seattle
Nchini Marekani mwishoni mwa Mwaka jana Balozi Liberata Mula mula
alisema yapo mafanikio makubwa yaliyojitokeza kufuatia ziara hiyo ambayo
yanatarajiwa kuinufaisha kiuchumi Zanzibar.
Balozi Mula mula
alisema kilichopo hivi sasa ni kuhakikisha taasisi zinazohusika na ziara
hiyo kuendelea kufuatilia mazungumzo au makubaliano iliyofikia ili
lengo la ziara hiyo liweze kufanikiwa vyema.
Akitoa shukrani zake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar
ina mategemeo makubwa ya kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji katika
sekta ya utalii kutokana na miundo mbinu mbali mbali iliyowekwa.
Balozi Seif aliuomba
Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani na Canada kuhakikisha kwamba
unaendelea kuitangaza Zanzibar kiuwekezaji ili washirika na taasisi za
maendeleo wapate nafasi ya kuitumia fursa hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar aliwapongeza watendaji wote wa Ofisi za Kibalozi za
Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani kwa kufanya kazi za
kizalendo licha ya kukabiliwa na mazingira magumu ya kikazi.
Chanzo: Zanzinews
Post a Comment