Rais Jakaya Kikwete
*****
RAIS Jakaya
Kikwete anatarajia kuipanga upya safu ya Baraza lake la Mawaziri wakati
wowote, huku baadhi ya wabunge na mawaziri wakitakiwa kusitisha
mapumziko yao ya mwisho wa mwaka na kurejea jijini Dar es Salaam haraka.
Miongoni mwa wabunge waliositisha mapumziko yao na kurejea nchini ni
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa nchini
Afrika Kusini na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki, aliyekuwa Uswisi.
Wabunge hao walipoteza nafasi zao za uwaziri baada ya ripoti ya
Kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, kuwagusa
mawaziri hao kwamba walishindwa kuwajibika katika utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza Ujangili.
Dk. Nchimbi anapewa nafasi ya kurejea kwenye Baraza la Mawaziri
kutokana na kushiriki kwake kuipinga operesheni hiyo, ambayo kwa kiwango
kikubwa ilikuwa chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na
kwamba alishawahi kumuandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
akiipinga.
Kwa upande wake Kagasheki, anatajwa kurudi kwenye Baraza la Mawaziri
kutokana na kubainika kwamba hakuwa na kosa na kwamba operesheni hiyo
ilitekelezwa zaidi kijeshi na haikuwa chini ya wizara yake moja kwa
moja.
Aidha Kagasheki anatajwa kuwa mmoja wa waliokuwa mawaziri hodari
kutokana na uwezo wake wa kufuatilia mambo, ambapo akiwa ndani ya Wizara
ya Maliasili na Utalii, alianza harakati za kukomesha biashara haramu
ya pembe za ndovu.
Wakati Kagasheki na Dk. Nchimbi wakipewa nafasi ya kurejea kwenye
Baraza la Mawaziri, pia zipo taarifa kwamba wapo baadhi ya wabunge
wataingia kwa mara ya kwanza kwenye baraza hilo, huku wengine
wakirudishwa kwa mara ya pili.
Taarifa za uhakika kutoka kwa watu wa karibu wa baadhi ya wabunge,
zimebainisha kwamba jana Rais Kikwete aliwaita Ikulu wabunge wawili
vijana, hata hivyo haikujulikana waliitwa kwa sababu gani.
Baadhi ya wabunge wanaotajwa kujumuishwa kwa mara ya kwanza kwenye
baraza hilo ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, Mbunge wa Iramba
Magharibi, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Kahama, James Lembeli, sambamba
na mmoja wa wabunge vijana kutoka mikoa ya Iringa na Njombe.
Wakati wabunge hao wakiitwa Ikulu, zipo taarifa za uhakika kwamba
mawaziri wote wametakiwa kusitisha mapumziko yao ya mwisho wa mwaka na
kurejea Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya kutajwa kwa baadhi ya wabunge kuingia kwenye Baraza la
Mawaziri imewatia hofu baadhi ya mawaziri, hasa wale walionyooshewa
vidole na chama chao kwamba ni mawaziri mizigo.
Mawaziri waliotajwa na CCM kuwa ni mizigo wamekuwa hawana matumaini
ya kurejea kwenye baraza hilo na kwamba wanaamini wao ndio watakuwa wa
kwanza kutemwa.
Wakati baadhi ya mawaziri wakiwa na hofu, zipo taarifa kwamba mmoja
wa wabunge wanaotoka Mkoa wa Mbeya ameshaanza kufanya sherehe, akiamini
kwamba amejumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Aidha imebainika kwamba wapo baadhi ya manaibu waziri wameshaanza kujipigia debe ili kupandishwa na kuwa mawaziri kamili.
Mchakato huo wa kujipigia debe unachagizwa na utaratibu wa Rais
Kikwete wa kuwapandisha hadhi manaibu waziri kuwa mawaziri kamili.
Tayari baadhi ya Manaibu Waziri kama Amos Makala, Lazaro Nyalandu na
January Makamba, Aggrey Mwanri na Angela Kairuki, wameshaanza kutajwa
kuwa wanastahili kuwa mawaziri kamili.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, anatajwa
kuwa miongoni mwa Manaibu Waziri wanaoweza kusalia kwenye Baraza la
Mawaziri, kutokana na utendaji wake, lakini hawezi kupandishwa hadhi
kutokana na makosa madogo aliyowahi kuyafanya, kama vile kushindwa
kutofautisha nchi ya Zambia na kisiwa cha Zanzibar, hali iliyoonesha
kuishushia hadhi Serikali ya Rais Kikwete, kwa kuwa na kiongozi asiyejua
historia na jiografia ya nchi yake.
Utamaduni wa kupandisha manaibu waziri
Dhana ya manaibu waziri hao kupandishwa inatokana na hatua ya Rais
Kikwete kuwahi kuwapandisha Dk. Nchimbi, aliyekuwa Naibu Waziri wa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Naibu Waziri wa Wizara
ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Aidha Ezekiel Maige kabla ya kupandishwa kuwa Waziri wa Maliasili na
Utalii, alikuwa naibu waziri wa wizara hiyo, wakati huo ikiwa chini ya
Shamsa Mwangunga.
Balozi Kagasheki kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na
Utalii, alikuwa naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mara baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani, mwaka 2006
alimpandisha aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Mifugo wakati wa Serikali
ya Awamu ya Tatu, Anthony Diallo, kuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya
Mifugo.
William Ngeleja, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
alipandishwa hadhi na kuwa waziri kamili wa wizara hiyo, kabla ya
kutemwa kwenye mabadiliko ya mawaziri yaliyofanyika Mei, mwaka 2013.
Aidha Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, awali alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.
Dk. Cyril Chami, ambaye ameanza kupigiwa chapuo la kurejea kwenye
baraza jipya, kabla ya kupandishwa hadi kuwa Waziri wa Wizara ya Viwanda
na Biashara na kutemwa mwaka 2012, alianzia kwenye unaibu waziri kwenye
wizara hiyo.
Mawaziri wengine ambao walianzia kwenye nafasi ya unaibu waziri ni
Celina Kombani, ambaye kabla ya kuwa waziri kamili wa Wizara ya Nchi,
Ofisi ya Rais (Utumishi), alikuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo,
Dk Mathayo, kabla ya kupewa nafasi hiyo alianzia kwenye nafasi ya Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Historia hiyo ya Rais kuwapa hadhi manaibu waziri kuwa mawaziri
inatoa nafasi kwa manaibu wengi kuamini kuwa huenda wakapandishwa, hata
hivyo hali ni tofauti kwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro
Mahanga, ambaye amekosa bahati ya kupandishwa kuwa waziri kamili, ingawa
ni mmoja wa manaibu waziri wa muda mrefu waliozunguka kwenye wizara
mbalimbali.
Dk. Migiro na uwaziri
Kwa upande wake, Dk. Asha-Rose Migiro anapewa nafasi kubwa ya kuwemo
kwenye Baraza la Mawaziri, kutokana na historia ya Rais Kikwete ya kutoa
nafasi ya uwaziri kwa watu anaowateua kuwa wabunge, ambapo kwenye idadi
ya wateule wake nane, tayari watano amewapa nafasi ya uwaziri.
Wabunge hao ni Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa akiongoza Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Makame Mbarawa, anayeshikilia
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Wateule wengine wa Rais kwenye ubunge ambao wameteuliwa kuwa mawaziri
ni Profesa Sospeter Muhongo, anayeshikilia Wizara ya Nishati na Madini,
Saada Mkuya na Janet Mbene, ambao ni manaibu waziri wa Wizara ya Fedha.
Wakati Dk. Migiro na wabunge wengine wakipewa nafasi ya kuwemo kwenye
Baraza la Mawaziri, joto linabaki kwenye nani atakwenda wizara gani.
Wizara zinazoonekana kuwa ni mtihani kwa Rais Kikwete kumpa mtu
sahihi ni Wizara ya Fedha, ambayo inashikiliwa na Dk. William Mgimwa,
ambaye kwa sasa ni mgonjwa.
Hata hivyo, Dk. Abdallah Kigoda, anayeshikilia Wizara ya Viwanda na
Biashara kwa sasa, anatajwa kuweza kuimudu wizara hiyo, huku Zakia
Meghji akitajwa kuwa na nafasi kubwa ya kurudi kwenye Baraza la
Mawaziri, ili kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dk. Migiro anapewa nafasi ya kurejea kwenye wizara yake ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Bernad Membe, anayeshikilia wizara
hiyo, akipewa nafasi ya kurudishwa Wizara ya Mambo ya Ndani,
aliyoihudumia kwa kipindi kifupi akiwa naibu waziri wa wizara hiyo.
Uteuzi wa nafasi ya uwaziri kimikoa
Kama Rais Kikwete ataendeleza utaratibu wake wa kuchagua mawaziri
kulingana na mikoa yao na kuamua kutomrejesha Nchimbi kwenye Baraza la
Mawaziri, anaweza kuteua mmoja kati ya wabunge hawa, Mbunge wa Viti
Maalumu, Mhandisi Stella Manyanya, Jenister Mhagama (Peramiho), Vita
Kawawa (Namtumbo) au Mhandisi Ramo Makani (Tunduru Kaskazini) ili kujaza
nafasi ya Nchimbi.
Endapo Kagasheki hatarejea, ni wazi turufu ya kuwemo kwenye Baraza la
Mawaziri inaweza kumuangukia Jason Rweikiza (Bukoba Vijijini), Charles
Mwijage (Muleba Kaskazini), Deogratius Ntukamazina (Ngara) au Asumpta
Mshama (Nkenge).
Nafasi ya Dk. David Mathayo, huenda ikawa kaa la moto kwa Rais
Kikwete kufanya maamuzi ya kumpata mtu sahihi, kwani idadi ya wabunge wa
Mkoa wa Kilimanjaro ni ndogo na kwamba wengi wao wameshashikilia
wizara, ukimuondoa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela,
ambaye wachambuzi wa masuala ya siasa hawampi nafasi sana ya kuingia
kwenye Baraza la Mawaziri.
Kauli ya Ikulu
MTANZANIA Jumatano lilimtafuta Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Premi Kibanga, ili kujua ukweli wa habari hizo, lakini alisema hajui
chochote.
“Mimi niko Tanga, sijui kinachoendelea,” alisema Kibanga kwa kifupi, alipozungumza kwa simu na gazeti hili.
Post a Comment