Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Wanamichezo wa Vikundi vya Mazoezi ya Viungo katika Bonanza la 5,Vikundi vya mazoezi ya Viungo,lililofanyika katika Uwanja wa Amaan,Wilaya ya Mjini Unguja,katika shamra shamra za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amewataka wananchi kujenga na kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi
ili kuimarisha afya zao pamoja na kujikinga na maradhi yanayoweza
kuepukika.
Dk. Shein
ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa
klabu za mazoezi na vyama vya michezo katika Bonanza Maalum la Mazoezi
ya Viungo lililofanyika katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Kabla ya
kuzungumza na wanamichezo hao Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi akiwa amefuatana na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif
Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na
viongozi wengine walishiriki matembezi ikiwa ni sehemu ya Bonanza hilo
yaliyoanzia Michenzani mjini Unguja hadi Uwanjani hapo.
Dk. Shein
aliwaeleza washiriki kuwa ni jambo lililo dhahiri kuwa kufanya mazoezi
ni jambo la msingi sana katika kuimarisha afya ya mwili na kuchangamsha
akili hivyo Serikali ina kila sababu ya kuziunga mkono jitihada
walizozianzisha za kuunda vikundi vya mazoezi.
Alifafanua
kuwa hivi sasa kumekuwepo na maradhi mengi ambayo hapa kwetu yanaelezwa
kusababishwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha na kuyataja maradhi hayo
kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, kisukari na kuongezeka unene
ambayo yanaweza kupunguza kwa kufanya mazoezi.
Hata
hivyo pamoja na ukweli huo alibainisha kuwa kuimarika kwa huduma za afya
na huduma hizo kusogezwa karibu na wananchi kumerahisisha wananchi
kugundua maradhi mengi kuliko iliyokuwa huko nyuma.
Dk. Shein
aliwahakikishia wanamichezo nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Saba
itaendelea jitihada zilizoanzishwa na Serikali za awamu zilizopita
kuimarisha michezo ikiwemo kuweka mazingira na miundombinu bora ya
michezo.
Kwa hiyo
aliwapongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa
kutekeleza maagizo yake kikamilifu ya kubadili haiba ya uwanja wa
michezo vya Amaan Unguja kwa wakati pamoja na kualika timu za nje katika
mashindano ya kikombe cha Mapinduzi mwaka huu.
Aliongeza
katika kuimarisha michezo Serikali imeuwekea pia nyasi bandia uwanja wa
Michezo wa Gombani Pemba na huduma nyingine ili kukidhi viwango vya
kimataifa. Kuhusu uwanja wa Mao Dk. Shein alisema tayari Serikali
imeshatiliana saini makubaliano na Serikali ya China kuujenga upya
uwanja huo.
Sambamba
na pongezi hizo alieleza kufurahishwa na Wizara hiyo kuhamasisha michezo
mijini na vijijini huku akitolea mfano ushiriki wa vikundi kutoka
sehemu zote za Zanzibar pamoja na Tanzania Bara katika Bonanza la mwaka
huu.
Wakati
huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein ameunga mkono tamko la Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii
na Michezo la kuifanya siku ya tarehe 01 Januari kila mwaka kuwa siku
ya mazoezi kitaifa na ametaka maandalizi ya Bonanza hilo ambalo litakuwa
la Sita yafanyike kwa umakini mkubwa.
Akizungumza
kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo Said Ali Mbarouk alisema Bonanza hilo ni sehemu ya utekelezaji
wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi la kuitaka Wizara hiyo kurejesha hamasa ya wananchi kupenda
nchini.
Kufuatia
agizo hilo alibainisha Waziri huyo wa Michezo kuwa Serikali imeamua siku
ya tarehe 01 Januari ya kila mwaka iwe siku ya mazoezi kitaifa ambapo
kila mwananchi popote alipo nchini atashiriki mazoezi.
Aliongeza
kuwa Bonanza hilo la Tano la Mazoezi ambalo limejumuisha vikundi vya
mazoezi 65 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara badala ya 50
vilivyapangwa awali ni ishara ya wananchi kuitikia wito wa kufanya
mazoezi pamoja na kuimarika uongozi wa ZABESA.
Kwa hiyo
aliahidi kushirikisha vikundi kutoka sehemu nyingi zaidi ya nchi katika
bonanza lijalo kuongeza hamasa na pia kuimarisha vikundi vya mazoezi.
Kwa
uapande wake Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Sharifa Khamis
alieleza kuwa Bonanza hilo ni uzinduzi wa Vuguvugu la Miaka 50 ya
Mapinduzi kwa wanamichezo ambalo litaendelea hadi tarehe 13 Januari
mashindano hayo yatakapofikia fainali.
Amewashukuru
wadau mbalimbali waliofanikisha Bonanza hilo pamoja na michezo
itakayofanyika wakati wa maadhimisho hayo. Amezitaja nchi za nje
zilizoleta timu kuwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Zambia, Sudan Kusini na
Ghana.
Katika
risala yao iliyosomwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha
Wafanya Mazoezi ya Viungo Zanzibar- ZABESA bibi Hawa Abdalla Mandred
wanamazoezi hao waliiomba Serikali ifanye tathmini ya kiafya kwa
wanamazoezi hao na Serikali kufanyia kazi matokeo ya tathmini yake kwa
faida ya wanamazoezi na kwa Taifa kwa jumla.
Risala
hiyo ilizidi kueleza kuwa wanamazoezi hivi sasa wanazidi kuhamasisha
wananchi wengine zaidi kujiunga na vyama vya mazoezi na takwimu za kila
mwaka zimekuwa zikionesha kuwa idadi ya vikundi na wanachama wa vyama
vya hivyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka.
Sambamba
na ongezeko hilo jambo muhimu la kutia moyo alisema Bi Hawa ni kuona
kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wanamazoezi wanawake tofauti na miaka
mitano iliyopita lilipoanzishwa bonanza hilo.
Alisema
ZABESA inaamini kuwa kazi hiyo ya kuhamasisha mazoezi inalisaidia Taifa
kwa kuwa mazoezi hayo yanasaidia kuepusha maradhi yasiyo ya lazima na
pia hata kutibu baadhi ya mardhi bila ya mwananchi kupaswa kweda
hospitali hivyo kulipunguzia Taifa gharama za matibabu.
Post a Comment