Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
Nape Nnauye akizungumza na waandihi wa habari katika Ukumbi wa
Sekretarieti ,Makao Makuu ya CCM Ofisi Ndogo Lumumba.
……………………………………………………………………….
Mara baada ya kuundwa kwa
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu
Ndg. Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka mwaka jana, Sekretarieti hiyo
imejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mikoani kukutana na wananchi
kusikiliza kero zao,kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na
kuimarisha Chama mikoani. Utaratibu huu ni agizo la mkutano mkuu wa
Taifa wa nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma. Nanukuu
azimio hilo;
“ Chama Cha Mapinduzi lazima
kiwe karibu na wananchi, kisikilize changamoto zao na kiwasemee wananchi
na hasa wanyonge” Moja ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM 2012.
Kwa hiyo msingi wa kwanza wa
ziara hizo ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambacho ndicho kikao
cha juu kabisa cha Chama. Msingi wa pili ni ukweli kuwa CCM ndio
iliyopewa dhamana na kuingia mkataba na wananchi kupitia ilani ya
uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015, hivyo inayowajibu wa kukagua
utekelezaji wa ilani hiyo.
Na bila shaka wote tumeshuhudia
jinsi ziara hizo zilivyoinua uhai wa Chama nchi nzima na kuongeza kasi
ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kutatua kero mbalimbali za
wananchi kwenye maeneo yao, kiasi cha kuongeza imani ya wananchi kwa
CCM.
Tumeshuhudia makundi mbalimbali
ndani ya jamii yakija kueleza changamoto zao ndani ya Chama. Makundi
hayo ni pamoja na makundi ya wakulima, wafugaji, wafanyabiashara,
wanafunzi na wafanyakazi hasa walimu. Huu ni uthibitisho wa kuongezeka
kwa imani yao kwa CCM.
Katika mwendelezo wa ziara hizo
mwishoni mwa mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM na baadhi ya wajumbe wa
Sekretarieti walifanya ziara ya siku 26 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na
Njombe. Pamoja na mambo mengine wananchi walilalamikia baadhi ya
watendaji wa serikali hasa baadhi ya mawaziri wakiamini kuwa yapo
mapungufu kadhaa yanayotokea kwenye wizara zao.
CCM kama lilivyo agizo la
Mkutano mkuu la kuwasemea wananchi tulisikiliza kilio chao na kwa
kufuata utaratibu, baadhi ya mawaziri hao waliitwa na kuhojiwa kwenye
Kamati Kuu ya CCM mwezi Disemba 2013.
Utaratibu wa watendaji wa
serikali kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye
vikao vya Chama sio mgeni na wala haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa
kwenye wilaya, wakuu wa mikoa hutoa mikoani kwao,hivyo sio utaratibu
mpya.
Baada ya mahojiano hayo Kamati
Kuu ya CCM ilitoa ushauri kwa serikali wa namna ya kurekebisha mapungufu
yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye
mamlaka na mawaziri ni Rais mwenyewe, CCM ililiacha suala hili kwake
aangalie njia ipi bora ya kuondoa mapungufu tuliyoyaeleza.
Na kwenye taarifa yetu kwa
vyombo vya habari baada ya kikao hicho tulisisitiza kuwa sio lazima
awafukuze mawaziri husika isipokuwa wanaweza kufanya mabadiliko katika
mfumo,sheria nk ili mradi kuwepo na mabadiliko katika kushughulikia
mambo yaliyolalamikiwa na wananchi.
Hivi karibuni Rais amefanya
mabadiliko kidogo kwenye baraza lake la mawaziri na kuwarudisha baadhi
ya mawaziri waliolalamikiwa na wananchi na wabunge, ambao malalamiko
hayo yaliungwa mkono na CCM. Ni kupitia malalamiko hayo ndipo
lilipozaliwa jina la mawaziri mizigo. Baada ya uteuzi huo kukaibuka
mjadala mkubwa nchini wakihoji kulikoni Rais kaamua kutowatimua mawaziri
hao.
Kwanza haikua hoja ya CCM
kuwafukuza mawaziri hao bali kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu
husika. Kufukuza inaweza kuwa ni njia ya kutatua tatizo lakini sio njia
pekee. Hivyo basi CCM tunaamini kuwa kurudishwa kwao wamepewa fursa ya
kurekebisha mapungufu tuliyoyasema kwa niaba ya wananchi. Tunaamini
mawaziri wote hawatabweteka bali watatimiza wajibu wao na kuhakikisha
wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa serikali.
Ifahamike kuwa Chama Cha
Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji
wengine watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na watakaoshindwa kutimiza
wajibu wao vizuri. Wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni
hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM, CCM haitavumilia usaliti huo. Kukaa
kimya kwa CCM itakua ni kujinyonga yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu
kabisa.
Tunajua wapo baadhi ya watendaji
wa serikali wasiopenda kuhojiwa utendaji wao, tunawasihi kwa moyo safi
wasiotaka kuulizwa juu ya utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani
CCM tutakuwa wakali sana kwenye mapungufu,kwani tukikaa kimya tutakua
tunajihujumu wenyewe.
Tutatumia vizuri wingi wa
wabunge wetu bungeni na wingi wa madiwani wetu kwenye halmashauri
kuisimamia vizuri serikali. Hivyo kuanzia sasa kasi ya CCM kuisimamia
serikali, kuisifu itakapofanya vizuri na kukosoa itakapofanya vibaya
itaongezeka mara dufu kwa kila ngazi.
Tunawaomba watanzania kwa ujumla
tuwape muda wateule hawa wa Rais watimize wajibu wao, lakini tusisite
kusema pale tutakapoona mambo hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji
wa kweli ndio msingi wa mafanikio na maendeleo yetu.
CCM inawatakia kila lakheri
kwenye kutimiza wajibu wao. Tuna matumaini makubwa kuwa wote kwa pamoja
hawataisaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba hawatayaangusha
matumaini ya wananchi kwa serikali yao.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
23/01/2014
Post a Comment