2. WATOTO WAFANYIWA UKATILI WA KUTISHA
Watoto Hassan Yusuf, Hussein Yusuf na Rehema Said baada ya kuokolewa na majirani.
Na Makongoro Oging'
“TUNAJUA
shangazi anatutesa kwa sababu baba na mama wapo mbali, kama wangekuwepo
hapa tusingeteswa hivi. Tunamuomba baba, tunamuomba mama kama watasoma
habari hii waje watuchukue turudi nyumbani, shangazi anatutesa sana,
wala hatukutegemea,” ndivyo alivyoanza kusema mtoto Hassan Yusuf (5)
ambaye ni mkubwa kwa wenzake, Hussein Yusuf (5) na Rehema Said (5).
Hassan na Hussein baada ya kuokolewa.
Ikifika
mahali mtoto mdogo anasema anawakumbuka wazazi wake kwa sababu ya mateso
anayoyapata ugenini ujue ni zaidi ya ukatili, tena ni ukatili wa
kutisha.
Watoto hao, kwa sasa wanaishi Nzasa ‘A’, Kata ya Charambe,
Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na ndiko walikopatia mateso yote.
MAMBO YALIPOANZA KUTIBUKA
Wiki
iliyopita, watoto hao waliokolewa na majirani katika kifungo cha miezi
sita ndani huku afya zao zikiwa zimedhoofu kwa kukosa chakula.
Banda walimokuwa wakiishi watoto hao.
Ilidaiwa
kwamba, watoto hao Hassan na Hussein ambao ni mapacha na Rehema,
walifungiwa katika banda la shangazi yao aitwaye Asia Bora ambalo ujenzi
wake haujakamilika. Wamekuwa wakiishi humo kwa kula mabaki ya vyakula
jalalani.
USHUHUDA WA MAJIRANI
Wakizungumza
na gazeti hili hivi karibuni, majirani wa nyumba hiyo walimweleza
mwandishi wetu kuwa watoto hao wamekuwa wakionekana nje ya nyumba hiyo
mara chache sana wakiwa wanagombania mabaki ya vyakula kwenye jalala.
Mtoto Rehema akiwa huru baada ya kuokolewa na majirani.
“Tumekuwa
tukiwaona nje mara chache kwenye jalala. Unajua, Asia (shangazi yao)
aliwachukua kwa kaka yake, Kijiji cha Namakongoro Kata ya Lihimalyao
huko Kilwa mkoani Lindi.
“Tukasikia lengo lake aje kuishi nao kwa
vile yeye Mungu hamkujalia kupata watoto. Lakini maisha hapo kwake
yakawa siyo mazuri kwa kipato kwa mama huyo.
Mmoja wa majirani hao aliyejitambulisha kwa jina la Aisha Ramadhan yeye alikwenda mbele zaidi kwa kusema:
“Hapo
awali tulikuwa tukiwaona wakitoka nje na kucheza na watoto wetu huku
wakiwa na afya nzuri. Asia akatueleza kuwa ni watoto wa nduguye,
amewachukua huko kijijini.
Ndani ya banda walimokuwa wakiishi watoto hao.
“Baada ya
muda fulani tukawa hatuwaoni, tulidhani amawarudisha kwao, lakini kadiri
siku zilivyokuwa zinakwenda mbele tukawa tunawaona mara chache wakiwa
jalalani wanapigania mabaki ya chakula.
“Kuna siku mimi niliwakamata
wakiwa wamebeba mfuko wa rambo wenye kinyesi, walikuwa wanakuja kutupa
katika maeneo yetu, nikawarudisha nao kwa shangazi yao. Kumbe nyumba
wanayoishi haina choo ndiyo maana wamekuwa wakijisaidia kwenye rambo.
“Siku moja
walipotoka nje kutafuta chakula jalalani, mimi na majirani wenzangu
tuliwauliza wanaishije? Wakatuambia hawapewi chakula na shangazi yao
akitoka asubuhi harudi mapema, akirudi inakuwa ni usiku sana wao wakiwa
wameshalala.
“Inasikitisha
sana kuwaona watoto hawa wanaachwa peke yao kutwa nzima bila mtu wa
kukaa nao na wamekuwa wakifungiwa ndani kwa muda mrefu sasa, ila huwa
wanakiuka masharti na kutoka kwa ajili ya kutafuta mabaki ya chakula.
Jirani huyo
akaendelea kuanika mateso ya watoto hao: “Kwa kuwaonea huruma tumekuwa
tukilazimika kuwapa chakula, lakini Asia anaporudi na kugundua hilo
anawapiga, kwa hiyo wakawa waoga kuja kuchukua chakula. Mimi niliumia
hadi machozi.”
Jirani:
“Baadaye wakawa hawaonekani, lakini cha ajabu mara nyingi tukiamka
asubuhi tunakuta mifuko ya rambo yenye vinyesi imetapakaa, tukimweleza
Asia inakuwa ugomvi.
“Siku moja baada ya shangazi yao kuondoka,
nilikwenda kuwachungulia ndani, nikawaona wamekonda sana, wamepauka na
wamevaa nguo zilizochakaa.
“Nilitokwa
machozi, nililazimika kuwaita wenzangu nao walipofika hakuna aliyejizuia
kulia. Tukasema hawa watoto watakufa, ndiyo tukaamua kuwaokoa kwa
kupeleka taarifa kwa mzee Dadi Salum ambaye ni polisi jamii wa hapa.
POLISI JAMII NAYE ALIA
“Mzee
Dadi naye alipofika na kuwaona kwa macho alilia, watu wakaanza
kukusanyika, tukawatoa nje watoto, kila mmoja aliwaonea huruma.
Tuliwachukua hadi Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Nzasa A.
SHANGAZI MTU ANUSURUKA KIPIGO
“Hatujui
ni nani aliyempigia simu Asia, kwani muda mfupi tu tukasikia yupo
nyumbani kwake. Uongozi wa mtaa ulimfuata, walipofika, wanawake wenzake
hasa wale anaochukua nao mkopo wa fedha benki walitaka kumpiga
wakimuuliza pesa anapeleka wapi.
“Hata hivyo
aliokolewa na polisi jamii ambao walimchukua na kumweka katika Bajaj na
kumpeleka Kituo cha Polisi Mbagala kwenye Dawati la Jinsia na Watoto,
watoto nao pia walipelekwa huko.”
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa
wa Nzasa A, Mrisho Salum alikiri kuwapokea watoto hao wakiwa katika
hali mbaya kiafya, wakapelekwa polisi. Akawataka wananchi kutokaa kimya
mara wanapoona vitendo kama hivyo.
Mwandishi
alifika hadi kituo cha polisi na kuambiwa na askari mmoja kuwa mapacha
walichukuliwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Othman Mbwana
aliyedai ni babu yao.
Mbwana alidai kwamba ameamua kuwachukua watoto hao wakaishi nyumbani kwake wakati akifanya mawasiliano na wazazi wao.
“Kwanza
nitawapeleka hospitali wakatazamwe afya zao, ila nimesikitishwa sana na
hali hii, sijajua ni kwa nini watoto hawa wamefikia hatua hii,” alisema
Mbwana.
Rehema yeye alichukuliwa na mjomba wake aitwaye Sood Ismail
ambaye alidai anakwenda kukaa naye hadi hapo atakapofanya mawasiliano na
wazazi wa huyo mtoto, akisema kitendo cha Asia kimeidhalilisha familia.
RPC TEMEKE ATUPIA NENO
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo amewataka wananchi kufichua
vitendo viovu ndani ya jamii na amewapongeza vijana wake wa ulinzi
shirikishi kuokoa maisha ya hao watoto.
Post a Comment