Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Jaji Warioba aonywa

 

Jaji mstaafu Joseph Warioba
******
Taasisi ya Kitaaluma na Siasa inayojihusisha na Kukuza Maendeleo ya Wananchi nchini (Aford), pamoja na wadau wa Katiba, imemtahadharisha Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, kuacha kuyachambua na kuyatolea ufafanuzi baadhi ya mambo yaliyomo katika rasimu ya pili ya Katiba mpya ili kuepuka maslahi binafsi yanayoweza kuvuruga mchakato huo.


Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Seneta Julius Misely, akizungumza na waandishi wa habari jiji Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, alisema kitendo cha Jaji Warioba kuendelea kuzungumza mambo ambayo tayari yamekwisha kuchukuliwa maamuzi, kunaleta taswira ya mgonano wa maslahi, jambo ambalo linaweza kuvuruga mchakato.

"Tume ya Mabadiliko ya Katiba imemaliza kazi yake baada ya kuwasilisha rasimu ya Katiba mpya. Kwanini aendelee kuzungumzia tena mambo yaliyomo katika rasimu hiyo, tafsiri yake ni nini? Hapa kuna jambo limejificha," alisema.

Misely alisema Jaji Warioba kuendelea kuzungumzia rasimu ya pili ya Katiba, inawafanya wadau wa Katiba mpya waamini kuwa rasimu hiyo ni dhaifu kiasi cha kuhifadhi mchango mwingine zaidi ya uliopo na hivyo kutawaondolea imani Watanzania.

Aliongeza kuwa Jaji Warioba kama kiongozi aliyekula kiapo, amehusika kwa nguvu kuyaongeza mawazo yake na ya watu wengine waliochangia kwenye rasimu ya pili ya Katiba, hivyo anapaswa kunyamaza kimya ili kuruhusu mchakato uchukue hatua inayofuata kwenye Bunge Maalum la Katiba.

Naye kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mtangazaji wa zamani wa TBC, Enock Ngombale- Mwiru, alisema Jaji Warioba amefanya kazi nzuri kwenye suala la Katiba lakini sasa anaanza kutibua kwa kuanza kujadili baadhi ya mambo yaliyomo katika rasimu hiyo, jambo linaloonyesha upendeleo wa mambo hayo.

Alisema Jaji Warioba ni mwanachama wa CCM ambaye chama chake kimeshatoa msimamo wa serikali mbili, hivyo anapoendelea kulichambua suala la serikali tatu, ni matokeo ya malumbano ndani ya chama chake na suala hilo linaharibu mchakato wa Katiba mpya unaondelea.

"Jaji Warioba anyamaze kimya ili wananchi wawe huru kwenye Bunge Maalum la Katiba, kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilishakwisha tangu Desemba 31, mwaka jana," alisema.

Januari 2, mwaka huu, ikiwa ni siku mbili baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukabidhi rasmi kwa Rais Kikwete, alizungumza na vyombo vya habari na kueleza kuwa watu wanaodai kuwa mapendekezo ya kuanzishwa muundo wa Muungano wa serikali tatu ni kumgeuka Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye enzi za uhai wake aliukataa.

Pia alisema suala la gharama haliwezi kuwa tatizo kwa kuwapo muundo wa Muungano wa serikali tatu.

Jaji Warioba alisema hayo katika mkutano kati yake na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri (TEF) kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Jaji Warioba alisema watu wanaotoa madai hayo wana upeo finyu wa kufikiri, hasa kuhusu hali aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere kimawazo.
“Wanafikiri Mwalimu (Nyerere) angekuwa na mawazo mgando wakati wote, asingebadilika,” alisema Jaji Warioba.

Alisema enzi za uhai wa Mwalimu Nyerere kuna mambo kadhaa yalibadilika, ukiwamo mfumo wa demokrasia ya chama kimoja cha siasa, ambao yeye alikuwa kinara wake mkubwa.

Hata hivyo, alisema Tume ya Jaji Francis Nyalali, ilipokuja na ripoti iliyopendekeza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, Watanzania wengi waliupinga.

“Lakini Mwalimu (Nyerere) akasema tumefika mahali hatuwezi kwenda na chama kimoja. Dunia imebadilika. Hata ukuta wa Berlin umevunjika,” alisema Jaji Warioba akimnukuu Mwalimu Nyerere.

GHARAMA HAZIEPUKIKI
Aidha, aliwashangaa wanaoshikilia kwamba serikali tatu zitatumia gharama kubwa katika kuziendesha huku wakisahau kuwa wakati Watanganyika walipoanza kujitawala, walianza na mikoa, wilaya, tarafa na vijiji vichache, lakini leo vimeongezwa na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji wake.

“Hizi ni gharama lakini ni za kimaendeleo,” alisema Jaji Warioba.
Hata hivyo, alisema njia pekee ya kupunguza gharama kubwa katika uendeshaji wa serikali za muundo wowote wa Muungano, ni kuondoa matatizo yanayousibu Muungano. 

CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright 2025 EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG | Designed By Code Nirvana