| PICHA: MAKTABA |
Vurugu kubwa zimetokea katika eneo la Mgodi wa Stamico uliopo
Nyarugusu wilayani Geita, baada ya walinzi kumuua kwa kumpiga risasi mtu
mmoja, hatua iliyowalazimisha wananchi kuvamia majengo ya Stamico na
kuyachoma moto.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Leonard Paul,
amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba yeye na maofisa wake
sasa wamefika katika eneo la tukio kwa ajili ya kudhibiti vurugu.
Alisema mpango huo utahusisha pia kuwasaka wanaojihusisha na vurugu.
Kwa mujibu wa shuhuda vurugu hizo, chanzo ni mmoja
wa wachimbaji wadogo kupigwa kwa risasi na kuuawa wakati akiwa katika
eneo la Mgodi wa Stamico.
Habari zilisema mgodi huo uko jirani na mgodi
binafsi wa Buziba na kwamba hatua iliwafanya wachimbaji wadogo kupiga
kelele na kuvamia eneo hilo na kisha kuchoma moto majengo ya mgodi huo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu,
Alphonce Malingira, alisema baada ya wachimbaji wadogo kubaini kuwa
mwenzao amekufa, walianza vurugu na kuvamia mgodi na kisha kuchoma moto
majengo.
Pia walipora baadhi ya vitu zikiwemo kompyuta.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Simiyu, Leonard Paul, alikiri kutokea kwa tukio hilo na
kubainisha kuwa amelazimika kwenda katika eneo la tukio, kufuatilia kwa
kina vurugu hizo.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote niko eneo la
tukio na kazi ya uchunguzi imeanza ikiwa ni pamoja na kuwasaka
waliohusika na vurugu, hivyo nitatoa taarifa baadaye,” alieleza.
Matukio ya polisi kuua wachimbaji yamekuwa yakitokea mara kwa mara migodini mkoani Geita.
MWANANCHI


Post a Comment