********
Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, imeelekeza kipindi cha mpito
ambacho pamoja na mambo mengine, kitaandaa mazingira ya Katiba hiyo
kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa
2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka
2014 na kufanya maandalizi ya mambo yote muhimu kwa ajili ya utekelezaji
bora wa masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya Mwaka 2014,” inasema sehemu ya rasimu hiyo.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia imependekeza
kipindi cha mpito cha miaka minne kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa
Katiba Mpya ili sheria zilizopo ziweze kubadilishwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba alisema jana kwamba katika kipindi hicho cha mpito
utakuwa ni muda wa kutungwa kwa Katiba ya Tanganyika. Warioba alisema
pia katika kipindi hicho, utakuwa ni muda wa mgawanyo wa rasilimali
baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za nchi washirika.
“Katika kipindi hicho pia utakuwa ni muda wa
kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa
kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2014,”
alisema.
Warioba alisema katika kipindi hicho, Katiba ya
Zanzibar itafanyiwa marekebisho ili kuwiana na masharti ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2014.
Maoni ya Muungano kutengeneza Katiba ya Tanganyika
Sehemu ya Rasimu ya Katiba ya Muungano,
imependekeza kuwa maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
yanaweza kutumika kutengeneza Katiba ya Tanganyika.
Raymond Kaminyoge, Elias Msuya na Fredy Azzah
MWANANCHI
Post a Comment