Mwandishi
wa Thehabari.com, Joachim Mushi (katikati mwenye jaketi) akizungumza na
baadhi ya wanakijiji wa Lunyala, wilayani Nkasi, Rukwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lunyala, Alfred Ndenje akizungumza na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani)
Nkasi, Rukwa.
KILA
kabila nchini Tanzania lina mila na desturi zake. Baadhi ya mila na
desturi hizi zimekuwa zikienziwa vizazi na vizazi kwa baadhi ya makabila
huku nyingine zikipigwa vita kutokana na kukiuka ama haki za kibinadamu
na pengine kuonekana hatarishi na zimepitwa na wakati. Ukitembelea
jamii za makabila anuai utalibaini hili.
Kimsingi
nakubaliana na utaratibu wa kuendelea kuzipiga vita kwa nguvu zote
baadhi ya mila hizi, ikiwemo hii ya jamii ya wafugaji wa kisukuma ambao
wao hadi leo bado wanaozesha mabinti wadogo hata ambao hawajitambui.
Mtoto
mdogo wa kike jamii ya wafugaji wa kisukuma baadhi ya vijiji wilayani
Nkasi anaolewa tena kwa mahari na mume asiyemjua. Mazungumzo hufanyika
kati ya wazazi wenyewe na kukubaliana mahari kisha kukabidhiana na binti
kuchukuliwa akiwa mdogo hivyo hivyo.
Bi.
Scholastica Milambo (40) ni mkazi wa Kijiji cha Lunyala wilayani Nkasi,
ikiwa ni miongoni mwa vijiji vilivyozungukwa na familia za wafugaji
toka makabila ya kisukuma. Anasema katika kijiji hicho jamii za wasukuma
wao ni jambo la kawaida kuwaozesha mabinti wao wakiwa kingali watoto.
Anasema
wakati mwingine mabinti hao huolewa na wazee kabila bila ya wao kujua,
kwa kuwa hulipiwa mali na kuchukuliwa wakiwa wadogo hata hawajitambui.
Kinachofanyika ni wazazi wa familia ya muoaji au muoaji mwenyewe
kuzungumza na wazazi wa binti kwamba wamempenda binti yake na kisha
kupangiwa mahari (idadi ya ng’ombe).
Anasema
baada ya hapo waoaji uleta ng’ombe kwa familia ya binti kama
walivyopangiwa na kumchukua binti huyo, hata kama ni mtoto wa miaka 7 au
chini ya hapo. Bi. Magreth Nkana (32) anasema wasukuma hawa jamii ya
kifugaji huweza kuilipia mahari hata mimba (yaani mtoto akiwa tumboni)
kwa makubaliano.
“…Hawa
watu mila zao ni za ajabu sana maana muoaji anaweza kuzungumza na
familia (ya mzazi mjamzito) na kukubaliana kuwa akizaa binti basi
atakuwa ni mke wa mtoa mahari, na hii hufanyika hasa familia inapokuwa
inazaa mabinti weupe…,” anasema Bi. Nkana akizungumza na mwandishi wa
makala haya.
Anasema
wanapooa binti mdogo; muoaji humchukua binti huyo na kwenda kumuhifadhi
kwa mama yake mzazi. Pale atakaa pamoja na watoto wengine wa mama wa
muoaji hadi anapotimiza miaka 15 ndipo kijana hupewa na kuanza
kumchombeza (kuishi naye kinyumba). Jamii hii ya wasukuma wafugaji
haioni kabisa umuhimu wa kumwacha binti huyu asome shule.
Naye
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lunyala, Edger Nkoswe anasema matukio ya
jamii ya wafugaji kuoza wa toto ni kitu cha kawaida kwao. Anasema ni
vigumu kuyadhibiti wao kwa kuwa wapo mbali na vijiji yaani pembezoni
(mashambani).
Hata
hivyo anasema wao huyafanya kwa siri kati ya familia ya muoaji na
muolewaji jambo ambalo mtu wan je ni vigumu kubaini. “…Utakuta binti
huyo mdogo akisha olewa mume amchukui moja kwa moja na kwenda kuishi
naye, humpeleka kwa mama yake mzazi na kusubiri hadi anapovunja ungo na
kuwenza kuingiliwa, ndipo mwenye mke hubeba na kuanza kuishi naye kama
mke,” anasema Mtendaji wa Kijiji cha Lunyala.
“…Ni
kweli huku kwetu wasukuma wanaoa watoto wadogo, wakati mwingine
wanaweza kuchumbia binti akiwa na miaka 12 na anapolipa mahari humchukua
na kwenda kumuweka kwa mama yake mzazi na anapotimiza miaka 15 na 16
humchukua na kuanza kuishi naye, jamii hii haina mpango na shule kabisa
hata ukiangalia wanapoishi ni mbali sana (porini) na huduma za kijamii,”
anasema Nkoswe.
Oscar
Mdenye ni Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,
katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anakiri uwepo wa ndoa za
utotoni kwa jamii hiyo na wenyeji wenyewe. Anabainisha kuwa tatizo la
ndoa za utotoni lipo kwa kiasi kikubwa na si kwa jamii za wafugaji
pekee, lakini hata kwa wenyeji hapa (wafipa) wanafanya vitendo hivyo.
“…Unajua
ndoa katika umri mdogo zipo na matukio ni mengi yanafanywa na kuungwa
mkono na jamii inayowazunguka, kwa maana nyingine sehemu kubwa vijijini
wanafanya vitendo hivyo…wakati mwingine unashindwa nani wa kumuwajibisha
kwa kuwa kila mmoja anafanya. Unakuta mtoto kaoa mtoto, wamezaa mtoto
na wote wanalia…,” anasema Mdenye.
Anasema
Ofisi ya Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto
wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu juu ya madhara ya ndoa katika umri
mdogo pamoja na haki za watoto ili jamii ibadilike na kuzingatia sheria
za nchi, japokuwa bado ni changamoto.
“…Tunajitahidi
kuelimisha jamii kupitia mikutano, matamasha ya pamoja na nafasi
nyingine tunapozipata, tumezunguka na kuelimisha sana juu ya haki za
watoto ili kila mmoja azijue labda itakuwa rahisi kuwabainisha
wanaozipuuza,” anasema.
Pamoja
na hayo anasema bado kuna changamoto kubwa ya jamii kutoa taarifa pindi
inapoona kuna ukiukwaji wa haki hizo. Anaongeza kuwa wengi hawaripoti
matukio hayo kwenye vyombo vya sheria ili viweze kuchukua hatua.
Lakini
pamoja na matukio hayo ya kuwanyima haki ya msingi ya kupata elimu
mabinti hawa kwa kuolewa moja kwa moja wakiwa wadogo, bado vitendo vya
uhalifu kwa watoto hawa vinafanyika pia hata kwa wale waliopo shuleni.
Wapo
wanaowafuata mabinti hawa shuleni na kuwarubuni na hatimaye kuwakatiza
masomo yao kwa kuwatia mimba. Ofisa Elimu Msingi, Wilaya ya Nkasi, Bw.
Misana Kwangura akizungumzia matukio ya mimba kwa ujumla kwa wanafunzi
eneo hilo, anasema japokuwa matukio hayo bado yanaendelea lakini kwa
sasa yameanza kupungua.
Anabainisha
kuwa hiyo ni kutokana na matukio hayo kupungua kwa sasa ukilinganisha
na hapo awali. Anatolea mfano tangu mwezi Januari hadi Novemba 2013
jumla ya wanafunzi 9 wametiwa ujauzito na kukatizwa masomo yao, idadi
ambayo ni ndogo ukilinganisha na mwaka 2012 ambapo wanafunzi 11 walitiwa
mimba.
Aidha
aliongeza kuwa kwa mwaka 2011 jumla ya wanafunzi 16 wa shule za msingi
walitiwa mimba na kukatizwa masomo yao. “…Kimsingi naweza kusema
matukio haya kwa sasa yanapungua ukilinganisha na hapo nyuma, na hii
inatokana na elimu ambayo tunaitoa kwa kuzunguka kwenye shule mbalimbali
kwa kutumia ofisi ya Ofisa Elimu Sayansi Kimu,” anasema Kwangura.
Kwa
upande wake Msimamizi wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi,
Cpl- Anna Kisimba anasema matukio ya ukatili kwa watoto ikiwemo
kuozeshwa yamekuwa yakiripotiwa kwenye dawati hilo na kuyafanyia kazi
ikiwemo kuwafikisha watuhumiwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Anatolea
mfano kwa mwaka 2013 hadi mwezi Desemba jumla ya matukio hayo 25
yaliripotiwa kwenye Dawati la Jinsia na watoto na utekelezaji wake upo
katika hatua mbalimbali. Anasema kwa matukio ambayo upelelezi wake
ulikamilika wameyafikisha mahakamani ili kutoa mwanya sheria kuchukua
mkondo wake kwa wahusika.
Post a Comment