Na Joseph Ngilisho,Arusha
BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya jiji la Arusha,limemtimua
Mkurugenzi wa jiji hilo, Nd. Sipora Liana na wakuu wake wa idara, katika kikao cha madiwani baada ya kumpigia
kura,wakidai Mkurugenzi huyo amezidi kuwadharau na kuwakejeli.
Hali hiyo ilijiri mapema jana wakati madiwani hao walipochachamaa
ndani ya kikao wakidai hawawezi kujadili mada yoyote hadi wapate ufafanuzi juu
ya dharau wanazodai zinafanywa na Mkurugenzi huyo kwa madiwani.
Naibu Meya, Nd. Prosper Msofe, aliyekuwa akiongoza kikao hicho
aliamuru kupigwa kura za kumjadili Mkurugenzi baada ya kutolewa hoja kutoka kwa
diwani wa Sekei, Nd. Crisipin Tarimo, kutaka baraza hilo lijigeuze kamati
kumjadili Mkurugenzi.
Hoja hiyo ilipokewa na Mwenyekiti wa kikao hicho na aliamuru baraza
hilo kujigeuza kamati baada ya nusu ya wajumbe kuunga mkono hoja hiyo ambapo
kwa pamoja walimtaka Mkurugenizi na wakuu wake wa idara watoke nje ya
ukumbi.Madiwani hao wakiwa kama kamati walianza kumjadili Mkurugeninzi huyo
huku kila mmoja akitupa lawama juu yake wakidai wamechoshwa kudharauliwa
ikiwemo kutofanyiwa kazi kwa maazimio wanayoyapitisha.
Awali diwani wa viti maalumu kupitia
CCM, Nd. Belinda Kabuje alisema hawataweza kufanya kazi na Mkurugenzi
mwenye dharau dhidi ya madiwani na kwamba madiwani palei wanapomfuata ofisini
kwa ajili ya kueleza kero zao anawajibu kwa nyodo na dharau kubwa.
“Huyu Mkurugenzi ana dharau sana, ni mwanamke kama mimi lakini amekuwa
na dharau utazani si mwanamke ,hatuwezi kukubali kufanya kazi na mtu wa namna
hii,” alisema.
Baada ya kamati hiyo kumalizika, Naibu Meya alisema kikao hicho
kilikuwa kizito na kwamba makubaliano yaliyotoka katika kamati hiyo ni kwamba
madiwani wataandika maoni dhidi ya tuhuma za Mkurugenzi na yatapelekwa kwa mkuu
wa mkoa kwa ajili ya kuitisha kikao na kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.
Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi, Nd. Sipora Liana aliwashangaa
madiwani hao kwa kujigeuza kamati kwa lengo la kumjadili na kueleza
kwamba,madiwani hao hawana ubavu wa kumjadili yeye.
Post a Comment