Leo tunaanza mwaka mpya, huku tukiwa na kumbukumbu ya mambo
yaliyotikisa anga za siasa hapa nchini katika mwaka 2013 kama yafuatayo:
1. Rasimu mbili za Katiba
Miongoni mwa matukio makubwa kwa mwaka uliopita ni
kuzinduliwa kwa Rasimu mbili za Katiba. Ya kwanza ikiwekwa hadharani
Juni 3, 2013 na ya pili juzi Desemba 30, 2013.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba alikabidhi rasimu hizo kwa Serikali kuamsha mjadala
kuhusu mwelekeo wa nchi, baada ya rasimu hizo kubainisha uwezekano wa
kutokea mabadiliko makubwa katika mfumo wa uongozi wa nchi.
Mambo makuu yaliyoibua mjadala mzito ni suala zima
la kuwapo kwa serikali tatu – ya Muungano (shirikisho), Tanzania bara
na Zanzibar.
2. Mawaziri wanne wang’olewa
Tukio kubwa la kufungia mwaka limetokea Desemba 20
baada ya mawaziri wanne kufutwa kazi baada ya ripoti ya madhila
yaliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili kuwasilishwa bungeni.
Mawaziri hao ni Balozi Khamis Kagasheki aliyekuwa
Maliasili na Utalii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha
na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
3. Kifo cha Nelson Mandela
Pengine tukio ambalo halijasahaulika vichwani ni
kicho cha Nelson Mandela, aliyekuwa rais wa kwanza mzalengo wa Afrika
Kusini hapo Desemba 5, 2013.
Kutokana na msiba huo wa dunia, viongozi zaidi ya
100 wakiwamo wakuu wa nchi na Serikali walishiriki hatua mbalimbali za
safari ya mwisho ya mzee huyo maarufu kama Madiba.
Mandela alizikwa Jumapili, Desemba 15, 2013 katika Kijiji cha
Qunu alikokulia, mazishi ambayo Rais Jakaya Kikwete alipata fursa ya
kuhutubia na kueleza nafasi ya Tanzania ilivyoshiriki katika harakati za
ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.
4. Kikwete ahutubia Bunge
Mwezi Novemba Rais Jakaya Kikwete alihutubia Bunge
lengo kubwa likiwa ni kufafanua kuhusu kuzorota kwa Jumuia ya Afrika
Mashariki (EAC). Pia aligusia ushindi wa majeshi ya Umoja wa Mataifa
yakijumuisha askari kutoka Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo), Katiba Mpya, na Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo baadaye
imekuja kusababisha mawaziri wake wane wafukuzwe kazi.
5. Chadema uamuzi mgumu
Vilevile Novemba 22, Chadema kilimvua madaraka
yote Zitto Kabwe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Naibu
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mjumbe wa Kamati Kuu na
Baraza Kuu kwa maelezo kuwa anakwenda kinyume na taratibu za chama
hicho.
Pamoja na Zitto wengine waliovuliwa nyadhifa zao
ni Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha na Mjumbe wa
Kamati Kuu na Baraza Kuu, Dk Kitila Mkumbo.
Viongozi hao wamepinga uamuzi huo wa Kamati Kuu na
kukata rufaa kwenye vikao vya juu, uamuzi unayotarajiwa kutoka mapema
mwezi huu.
6. Malumbano, matusi bungeni
Mwaka uliopita Bunge lilitawaliwa na matukio
makubwa na mijadala mizito iliyoibua hisia kali, malumbano na wakati
mwingine matusi yaliyowaacha wananchi midomo wazi.
Mojawapo ya mijadala hiyo ni ule wa Aprili 15,
ambapo Ezekiel Wenje (Nyamagana) alitoa kauli za kukituhumu chama cha
CUF kuwa na uhusiano na vyama vya kiliberali vinavyosapoti ushoga, hali
iliyoibua majibu mazito kutoka kwa wabunge wa CUF kwamba Chadema “ni
wehu, wahuni, wazushi na wameidhalilisha CUF”.
Katika hatua nyingine wabunge wakichangia hotuba
ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), Juma Nkamia alijibizana
na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini-Chadema), alisema kuwa yeye “haongei na
mbwa bali mwenye mbwa.” Naye Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde
alitoa kauli ya iliyotafsiriwa kuwa ya kuudhi kuwa kuna “wabunge bungeni
wenye mimba zisizitarajiwa.” Kauli nyingine iliyochoma masikio ya
wabunge na wananchi ilikuwa ya Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini-
Chadema) ya “akili ndogo kutawala akili kubwa” na wakati mwingine
kutumia kifungu cha Biblia katika Kitabu cha Mithali 27:22, kinachosema
kuwa; ‘Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu pamoja na ngano, upumbavu
wake hautamtoka.
7. Makonde bungeni
Ukiacha zile kauli zilizolalamikiwa kuwa ni za kuudhi, mwaka
2013 ilifika wakati Bunge likawa kama sinema wakati maofisa usalama
walipolazimika kumbeba mzobemzobe Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
(Sugu).
Katika tukio hilo, ambalo maofisa usalama
walitakiwa kumtoa nje Kiongozi wa Kambi Rasimu ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe huku wabunge wa kambi hiyo wakipinga kutolewa nje.
Ilidaiwa kuwa Sugu alimrushia ngumi mmoja wa askari.
8. Lema ashinda rufaa ya ubunge
Mwezi Aprili 2013 Mbunge wa Arusha Mjini
(Chadema), Godbless Lema aliyekuwa nje ya Bunge baada ya ubunge wake
kutenguliwa na Mahakama Kuu alishinda rufani baada ya Mahakama ya Rufaa
kutupilia mbali maombi ya marejeo na kuamua arudi bungeni.
Maombi ya marejeo yalikuwa yamewasilishwa
mahakamani hapo na makada watatu wa CCM mkoani Arusha, kupitia kwa
mawakili wao Alute Mughway na Modest Akida wakiiomba Mahakama ya Rufani
ifanye marejeo ya hukumu yake hiyo kwa madai kuwa hukumu ya Mahakama ya
Rufaa iliyomrejeshea ubunge wake haikuwa sahihi.
9. Kicheko Aeshi Hilary
Furaha ya kurudi bungeni haikuishia kwa Lema, Mei
6, kicheko kilihamia kwa Aeshy Hilary baada ya Mahakama ya Rufani,
kumthibitisha kuwa ni mbunge halali wa Sumbawanga Mjini baada ya
kushinda rufaa aliyokata kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya
Sumbawanga, iliyomvua ubunge.
Hilaly alivuliwa ubunge na aliyekuwa Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Bethuel Mmila Aprili 30, 2012,
kutokana na kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho
katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 kupitia Chadema, Nobert Yamsebo.
10. Dk Kafumu kidedea Igunga
Ilipotimu Mei 9, msimu wa furaha ukahamia Igunga
pale Dk Dalali Kafumu wa CCM, ambaye ushindi wake uliokuwa umebatilishwa
na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, alirejeshewa ubunge wake na Mahakama
ya Rufaa.
Dk Kafumu katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi
iliyoachwa na Rostam Aziz aliyejiuzulu, alimshinda Joseph Kashindye wa
Chadema. Kashindye alipinga ushindi huo kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi na ubunge huo kutenguliwa.
Sakata la gesi Mtwara
Ingawa suala hili lilianza katika mwaka uliotangulia wa 2012,
mwaka 2013 umeshuhudia maandamano makubwa, hasira za baadhi ya wananchi
waliojichukulia hatua mkononi na kuchoma majengo na magari, pia hatua za
Serikali katika kutuliza vurugu hizo za kupinga gesi kusafirishwa kwa
bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Hali hiyo ilitulizwa na sasa ujenzi wa bomba
unaendelea na hivyo kuweka matumaini kuwa ugunduzi wa gesi nyingi hapa
nchini unaweza sasa kuwa wa manufaa badala ya kuwa mkosi kama ambavyo
ilikuwa imeanza kuonekana.MWANANCH
Post a Comment