Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MKUU WA WILAYA YA MULEBA AMTIA NDANI DIWANI


Mkuu wa Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, Lembris Kipuyo.
*****
MKUU wa Wilaya (DC) ya Muleba, mkoani Kagera, Lembris Kipuyo, amedaiwa kutumia vibaya mamlaka yake na kuwalazimisha polisi kumkamata Diwani wa Kata ya Magatakalutanga, Geofrey Ezekiel (CCM), kwa madai ya kumtishia maisha na kutaka kummwagia tindikali.
Habari kutoka Muleba zilisema kuwa  Kipuyo amekuwa akitoa tuhuma mbalimbali dhidi ya diwani huyo na kufikia hatua ya kumshitaki katika vikao vya CCM vilivyoketi Januari 5 na 6 mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari hizo, diwani huyo alilazimika kuandika barua kwa uongozi wa wilaya wa CCM na kumshitaki mkuu huyo wa wilaya.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa kutokana na hatua hiyo Kipuyo alikimbilia polisi na kudai kuwa diwani amemtishia maisha na kutaka kummwagia tindikali, jambo lililolilazimu Jeshi la Polisi kumkamata na kumweka chini ya ulinzi.

“Hivi ninavyokwambia diwani huyo ameelekea nyumbani kwake na polisi kwa ajili ya kwenda kufanya upekuzi,” alisema mtoa habari wetu.
Habari zaidi zinasema kuwa mgogoro huo unatokana na Kipuyo kuingia katika vikao viwili vya CCM na  cha Kamati ya Siasa ya wilaya, akimtuhumu diwani huyo kuwa ni mla rushwa na amekuwa akitumia nafasi yake ya uenyekiti kushirikiana na makandarasi kula fedha za miradi.

Chanzo hicho kilisema kuwa hata katika kikao cha Januari 6 cha Kamati Kuu ya wilaya bado mkuu wa wilaya hiyo aliendelea kushusha tuhuma hizo huku diwani huyo akiwa si miongoni mwa wajumbe waliohudhuria kikao.

“Hatua hiyo ndiyo ilimsababishia diwani huyo kulazimika kuandika barua kwa uongozi wa wilaya kulalamikia kitendo hicho na Kipuyo alivyobaini hilo akaamua kumbadilishia tuhuma na kufungua hiyo ya kumwagiwa tindikali na kutishiwa maisha,” alisema.

Hata hivyo gazeti hili lililazimika kumtafuta Kipuyo ambaye alipigiwa simu na kushindwa kupokea, badala yake alituma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi na kudai kuwa yupo kikaoni, huku akitaka kujua aliyempigia simu.

Akithibitisha kukamatwa kwa diwani huyo, mmoja wa askari wa jeshi hilo (jina limehifadhiwa) kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo, alikiri kukamatwa kwa diwani huyo na kuwa bado wanamshikilia kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top