Rais Kikwete alitengua uteuzi wa Mawaziri hao kutokana na shinikizo la
wabunge baada ya kuipitia Ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoundwa
kuchunguza athari zilizotokana na utekelezwaji wa "Operesheni Tokomeza
Ujangili".
Mawaziri ambao uteuzi wao ulitenguliwa ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mifugo na Uvuvi, Dkt. David
Mathayo, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Shamsi Vuai Nahodha
pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Nafasi nyingine ambayo iko wazi ni ile ya Waziri wa Fedha, ambayo
aliyekuwa Waziri wake, Dkt. William Mgimwa, alifariki dunia Januari mosi
mwaka huu.
Macho na masikio ya Watanzania yapo kwa Rais Kikwete wakiamini kiongozi
huyo, ana kazi ngumu ya kufanya uteuzi makini ambao utarudisha heshima
ya Serikali hasa kwa wananchi walioathirika na operesheni hiyo.
Wakizungumza na Majira ili kutoa maoni yao kwa sharti la kutotajwa
majina yao gazetini, baadhi ya mawaziri ambao hawakuguswa na rungu hilo,
walisema kuchelewa kwa Rais Kikwete kufanya uteuzi huo ni dalili nzuri
ya kuteua mawaziri wenye sifa na uwezo wa kumsaidia katika wizara
husika.
Alisema suala la uteuzi wa nafasi nyeti za uwaziri, si kazi ndogo ndio
maana amekaa kimya muda mrefu ili kuangalia nani anayeweza kutekeleza
majukumu atakayompa ili kuleta matokeo mazuri kwa wananchi, Taifa kwa
ujumla.
Waliongeza kuwa, kazi kubwa ipo kwenye uteuzi wa Waziri wa Fedha ambaye
uwezo wake utafanana na ule wa marehemu Dkt. Mgimwa kwani kifo chake ni
pigo kubwa kwa Serikali iliyotambua uwezo wake na kumpa dhamana.
"Dkt. Mgimwa alikuwa na uwezo mkubwa katika masuala ya fedha, aliweza
kufanya mambo mengi ambayo kimsingi yameiletea sifa kubwa Serikali yetu
ndani na nje ya nchi.
"Imani yangu ni kwamba, Rais Kikwete ana washauri wazuri ambao watafanya
kazi nzuri ambayo itakubalika na wananchi wote... tusubiri uteuzi
wake," alisema mmoja wa Mawaziri wakati akitoa maoni yake.
Kwa upande wao, baadhi ya wa n a n c h i wa l i o z u n g umz a na
Majira, wamemshauri Rais Kikwete asikilize kilio cha wabunge ambao
walishauri kuwajibishwa kwa mawaziri wengine ambao uwajibikaji wao si
mzuri katika
Serikali yake.
Walisema mbali na mawaziri ambao ametengua uteuzi wao, wapo watendaji
katika wizara hizo ambao nao wanapaswa kuwajibishwa kwa kuondolewa
katika nafasi hizo kwani kama wataendelea kuwepo, bado wataendelea kuwa
kikwazo kwa mawaziri wapya watakaoteuliwa.
"Mimi naamini CCM bado ina watendaji wazuri ambao wanaweza kupewa nafasi
za uongozi na wakafanya kazi waliyopewa kwa ufanisi mkubwa.
"Ni fursa nzuri kwa Rais Kikwete na wasaidizi wake, kukaa chini na
kuteua viongozi ambao uteuzi wao utapokewa vizuri na wananchi... kati ya
mawaziri ambao alitengua uteuzi wao, wapo ambao anaweza kuwarudisha ila
si wote kwani ajali iliyowakuta, imechangiwa na wasaidizi wao," alisema
Bw. Suleiman Sadif ambaye kitaaluma na mchumi.
Akizungumzia suala la mawaziri ambao Kamati Kuu ya CCM iliwaita na
kuwahoji, mjini Dodoma, Bw. Sadif alisema dhamira ya chama hicho si
kutaka wafukuzwe kazi bali lengo ni kuwakumbusha viongozi hao watekeleze
wajibu wao.
Alimpongeza Rais Kikwete, kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kutengua uteuzi
wa Mawaziri wake kwani hiyo ndiyo demokrasia na uamuzi huo umeepusha
malalamiko ambayo yangeweza kutolewa kwa Serikali kwani matokeo ya
Operesheni Ujangili hayakuwa mazuri kwa Taifa.
Uchunguzi uliofanywa na Majira umebaini kuwa, wananchi wengi wana hamu
kubwa ya kuona Rais Kikwete akiteua Mawaziri vijana ambao utendajikazi
wao umeonekana katika majimbo yao, Kamati za Bunge na kwenye mijadala
mbalimbali yenye masilahi kwa Taifa.
Post a Comment