Serikali ya Tanzania, Mfuko wa Maendeleo ya Watoto wa Umoja wa Mataifa ,
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) Tanzania, Shirika kimataifa la Save the
Children (SCI) na Shirika la Plan International (PLAN) leo wamezindua
mpango wa pamoja wa kukomesha ukatili dhidi ya watoto Tanzania.
UNICEF, Plan
International (PLAN) na Save the Children International (SCI)
watatekeleza mpango huu uliopata ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) wa
kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 4 (€1.8 milioni), katika wilaya
za Kisarawe, Kibaha na Shinyanga vijijini, kwa upande wa Tanzania Bara,
na wilaya ya Kaskazini ya Zanzibar. SCI, PLAN, kwa ushirikiano na
serikali za mitaa na mashirika ya kiraia wataongoza mpango huu katika
ngazi ya serikali za mitaa. UNICEF watasimamia katika ngazi ya kitaifa
pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania Bara na Wizara ya
Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Zanzibar.
“Ushirikiano
huu ni hatua muhimu ya kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto
ilikukabiliana na ukatili dhidi ya watoto nchini, pamoja na kutoa fursa
ya kuimarisha muungano kwaajili ya maendeleo ya watoto katika ya Umoja
wa Ulaya, Serikali husika na mashirika yanayofanya kazi kwa ukaribu na
watoto – UNICEF, PLAN International, na Save the Children”, amesema Dkt. Jama Gulaid, Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania
“Kulinda haki na
ustawi wa watoto sio tu adili muhimu, bali pia ni lengo la msingi la
maendeleo. Umoja wa Ulaya kwa taadhima umechangia katika mpango huu wa
pamoja wa wadau mbali mbali utakao fika mbali katika kutoa huduma za
kina na jumuishi kupambana na ukatili dhidi ya watoto” amesema Eric
Beaume, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano, Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini
Tanzania.
Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kufanya utafiti wa kina juu ya viwango vya unyanyasaji wa kijinsia, kimwili na hisia dhidi ya wasichana na wavulana. Ripoti ya Utafiti wa Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania,
uliotolewa na Serikali na UNICEF mwaka 2011, umedhihirisha kwamba
msichana mmoja kati ya watatu na mvulana mmoja kati ya saba nchini
Tanzania hukumbwa na manyanyaso ya kijinsia kabla ya kufikisha umri wa
miaka kumi nane. Pia, viwango vya unyanyasaji wa kimwili viko juu sana,
kwani karibu wasichana na wavulana watatu kati ya wanne wamepigwa ngumi,
kuchapwa au kupigwa mateke wakati utoto wao, huku robo ya watoto wote
wamefanyiwa ukatili wa kihisia. Watoto wengi hawashtaki matukio hayo,
wachache hutafuta huduma stahiki, na wachache zaidi hupatiwa huduma,
matibabu au msaada. Mpango huu wa pamoja ni mwandamo wa Utafiti wa Ukatili Dhidi ya Watoto uliofanyika mwaka 2009 ambao utasaidia nchi kutoka kwenye hatua ya utafiti kwenda hatua ya utekelezaji.
Mradi wa kumlinda motto umejenga mahusiano mahususi na hatua na mifumo iliyopo sasa nchini. Mradi
unasaidia Mpango Mkakati wa Taifa katika Kuzuia na Kukabiliana na
Ukatili Dhidi ya Watoto (2013-2016) pamoja na Mpango Mkakati wa Taifa wa
kwaajili ya Watoto Wanaoishi Katika Mazingira Hatarishi (2013-2017).
Katika Mpango wa pili, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wameahidi
kuongeza wigo wa mifumo ya ulinzi wa mtoto kufikia wilaya 30 ifikapo
mwaka 2016. Msaada kutoka Umoja wa Ulaya (EU) ni mchango muhimu wa
kutimiza lengo hili.
Mpango huu
utasaidia uanzishwaji wa mifumo ya kumlinda mtoto ili kwa ufanisi uweze
kutambua, kudhibiti na kukabiliana na kila aina ya ukatili dhidi ya
watoto, hasa watoto wa kike. Katika ngazi ndogo wa kitaifa, hatua hii
itasaidia utekelezaji wa mipango iliyopo ya kupambana na ajira kwa
watoto na kuanzisha shule salama Zanzibar, kwa pamoja na SCI, na
kuongeza nguvu katika mifumo ya kijamii iliyopo chini ya Programu ya
Maji na Usafi wa Mazingira, Kisarawe ya Plan International, zote
zikitekelezwa kwa msaada wa Umoja wa Ulaya (EU)
Mradi huu
utasaidia mamlaka za kitaifa kujenga mifumo ya kumlinda mtoto katika
ngazi za wilaya na kukabiliana na kila aina ya ukatili dhidi ya watoto,
hasa watoto wa kike. Utajikita kusaidia watoto na familia zao,
kuimarisha ulinzi katika mazingira ya jamii na shule salama, wakati
ukiwajengea uwezo wenye jukumu la mstari wa mbele. Programu inalenga
kufikia malengo ya muda mrefu, kuwa na mfumo endelevu kwa ajili ya kutambua, kuzuia, kukabiliana na kusaidia watoto
kwa kuujumuisha katika mfumo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na
taratibu za jamii kwa kutumia matokeo yatakayopatikana kuhamasisha mgao
wa mara kwa mara wa bajeti kwaajili ya ulinzi wa mtoto katika ngazi za
wilaya. Katika ngazi za kitaifa, programu itaimarisha uwezo wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Tanzania Bara na Zanzibar kwa kutoa msaada wa kiufundi kwa Halmashauri za Serikali za Mitaa namna ya kuimarisha mfumo wa ulinzi wa mtoto.
Post a Comment