Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini wakisikiliza mada
mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwenye mkutano ulioandaliwa na Kituo
cha Demokrasia Tanzania (TCD), Dar es Salaam jana. Picha na Venance
Nestory
**********
Vyama vya siasa vimekubaliana kutafuta mwafaka wa agenda za Katiba Mpya kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba.
Kutokana na makubaliano hayo, vimekubaliana
kuwasilisha mapendekezo yao kwenye Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD),
ili kuratibiwa kabla ya kuanza kwa Bunge hilo.
Vyama hivyo vimetakiwa kuwasilisha maoni ili
yachambuliwe na kutolewa maoni ya pamoja yatakayotumika kwenye Bunge
Maalumu la Katiba.
Baadhi ya vyama vimeonyesha wazi kutofautiana na
Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Chama tawala, CCM kinatofautiana na vingine juu ya mfumo wa
Muungano kikitaka Serikali mbili wakati vingine vikikubaliana na maoni
ya Tume ya Serikali tatu.
Bunge la Katiba limepangwa kuanza Februari, mwaka
huu na litakuwa na wajumbe 640, huku 42 wakitokea katika vyama hivyo vya
siasa, kila chama kikitoa wajumbe wawili.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa majadiliano ya
viongozi wa vyama hivyo, Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia alisema:
“Tumekubaliana kuwa mpaka Januari 31, mwaka huu kila chama kiwe
kimewasilisha maoni yake kuhusu rasimu ya Katiba.
“Kuanzia Februari 8 hadi 14, mwaka huu Kamati ya
mashauriano itayapitia maoni yote ya vyama ili kama kuna tofauti ziweze
kujadiliwa. Tunataka tuwe na mawazo yanayofanana ndani ya Bunge la
Katiba kwa sababu Katiba Mpya ni muhimu kuliko itikadi za vyama vyetu,
nchi kwanza vyama baadaye.”
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula na
Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana ambao walikuwapo katika mkutano
huo, walikataa kutolea ufafanuzi msimamo wa chama hicho kuhusu
mapendekezo yaliyomo katika rasimu hiyo.
“Kila kitu amezungumza msemaji wetu Mbatia, sasa
mimi mnataka niseme nini siwezi kuzungumza tofauti na makubaliano ya
kikao chetu cha leo (jana),” alisema Mangula.
Katika ufafanuzi wake, Mbatia alisema kama vyama
hivyo vitaingia katika Bunge hilo na kuanza kupingana ni wazi kuwa
vitawachanganya wananchi: “Kuna vyama vinataka Serikali mbili vingine
tatu na vingine moja, nadhani tutakubaliana na hata ikishindikana basi
tuwe na aina ya uwasilishaji ambayo haitaleta mvutano bungeni.”
Mbatia pia aligusia suala la maboresho ya Daftari
la Kudumu la Wapigakura… “Tumeiomba Serikali kuipatia fedha Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili iweze kuliboresha daftari hilo, tunataka
liwe limefanyiwa maboresho katika upigaji wa kura ya maoni Mei mwaka
huu.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema lengo la kukutana ni kutaka kuweka msimamo wa pamoja kwa maslahi ya taifa.
MWANANCHI
Post a Comment