Waziri Mkuu Mizengo Pinda akikagua marekebisho ya ukumbi wa Bunge kwa ajili ya Bunge la Katiba. ******* |
Maandalizi ya Bunge Maalumu la Katiba,
yamefikia hatua nzuri zaidi na wiki ijayo majina 201 ya wajumbe wa
nyongeza wa Bunge hilo, yatatangazwa katika Gazeti la Serikali ili
kukamilisha wajumbe 604.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, ilinukuu
kifungu kidogo cha tatu cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Toleo la 2013, inayomtaka Rais kuchapisha majina hayo katika
Gazeti la Serikali.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakusudia kukamilisha
uteuzi wa wajumbe hao baada ya kushauriana na Rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, mwanzoni mwa wiki ijayo na majina hayo yatachapishwa
kwenye Gazeti la Serikali," ilieleza taarifa hiyo.
Sheria inaendelea kusema kuwa kati ya wajumbe hao 201, theluthi moja sawa na wajumbe 67, lazima watoke Zanzibar.
Mbali na wajumbe watakaoteuliwa wiki ijayo, wengine ni wabunge wote
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao ni 357 na wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar, ambao wako 81.
Sheria hiyo pia inaeleza kuwa baada ya Bunge hilo kuitishwa, wajumbe
hao watachagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Naibu Katibu wa
Bunge.
Kazi ya kuchambua majina ya wajumbe waliopendekezwa na taasisi zao
ilimalizika wiki iliyopita ambapo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue, alisema Ikulu ilipokea majina 2,722 kutoka taasisi 575.
Kwa mujibu wa Balozi Sefue wakati wajumbe wanaotakiwa kuwakilisha
taasisi zisizo za kiserikali ni 20, taasisi hizo 245 zilipeleka majina
1,185.
Taasisi za kidini nazo kisheria zinapaswa kuwa na wawakilishi 20,
lakini kati ya taasisi hizo 77 zilipendekeza majina 277. Vyama vya siasa
vyenye usajili wa kudumu, kisheria vinapaswa kuwa na wawakilishi 42,
lakini vyama hivyo 21, vilipeleka majina 126.
Kwa upande wa taasisi za elimu, zina nafasi 20 za wawakilishi, ambapo
taasisi tisa zilipeleka majina 82. Makundi ya watu wenye ulemavu, yana
nafasi 20 za wawakilishi na 24 yalipeleka majina 70.
Vyama vya wafanyakazi, kisheria vimepewa nafasi 19 za uwakilishi na
vyama 20 vilipendekeza majina 69. Vyama vya wafugaji vina nafasi 10
ambapo vinane, vilipendekeza majina 43.
Wavuvi kupitia vyama vyao, kisheria wana nafasi 10, vyama saba
vilipeleka majina 45. Wakulima wana nafasi 20 kisheria ambapo vyama 22
vya wakulima, vilipendekeza majina 115 na makundi yenye malengo
yanayofanana pia yalipewa nafasi 20 kisheria ambapo makundi 142
yalipendekeza majina 710.
Kesho kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rasimu ya Pili ya Katiba mpya
inatarajiwa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali, kutekeleza kifungu
kidogo cha pili cha kifungu cha 20 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Sura 83, Toleo la 2013.
Sheria hiyo inamtaka Rais kuchapisha Rasimu hiyo kwenye Gazeti hilo
ndani ya siku 30 baada ya kukabidhiwa Rasimu hiyo na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba. Tume hiyo ilimkabidhi Rais Kikwete Rasimu hiyo Desemba 30
mwaka jana.
Post a Comment