Baada
ya kikosi kazi cha Jeshi la Polisi cha Kudhibiti Uharamia Baharini
kukamata kilo 201 za dawa za kulevya aina heroini zilizokuwa zikiingizwa
nchini kutoka Iran. Sasa imefahamika kuwa madawa ya kulevya
yanapitishwa kwenye bahari ya hindi. Hii imethibotishwa kwenye gazeti
la MWANANCHI kutoa maelezo ya kina kuhusu madawa hayo.Polisi
wa kikosi kupambana na dawa za kulevya wakizifungua dawa hizo
zilizokamatwa jana kwenye jahazi liitwalo Kunarak-Iran iliyokutwa katika
bahari ya Hindi eneo la Tanzania ikiwa na Heroin kilo 201, pamoja na
raia wa nane wa Iran na wapakistan wanne.Picha na Michael JamsonGazeti
la mwananchi linaeleza kuwa; wakati vita ya kupambana na biashara ya
dawa za kulevya ikiendelea nchini, wasafirishaji wa dawa hizo wameanza
kutumia fukwe ndogondogo za bahari nchini kuziingiza kutoka Mashariki ya
mbali, gazeti hili limebaini.Januari
10, mwaka huu saa 6:30 usiku, mwandishi wetu alishuhudia mzigo
unaoaminika kuwa ni dawa za kulevya, ukishushwa kutoka kwenye boti, eneo
la Salender Bridge, nyuma ya Kituo cha Polisi kilichopo eneo hilo.Baada
ya boti hiyo kutia nanga, walishuka watu zaidi ya 10; Wazungu wawili,
Waafrika kadhaa na mmoja mwenye asili ya Asia na kuungana na wengine
wanne ambao tayari walikuwa katika eneo hilo wakiwa ndani ya magari
mawili.
Mara moja
walianza kupakua mizigo iliyokuwa imefungwa kwenye maboksi na kupakia
kwenye magari ambayo yalikuwa yameegeshwa mbali kidogo na ufukwe huo.
Kazi hiyo ilichukua muda usiozidi nusu saa na baada ya mizigo kupakiwa,
magari hayo moja likiwa ni Land Cruiser liliondoka na kuelekea upande wa
Morroco na jingine aina ya Nissan liliondoka kwenda uelekeo wa Posta
Mpya.
Wakati
magari hayo yakiondoka kwa mwendokasi, boti iliyokuwa na mzigo huo nayo
iling’oa nanga na kuelekea katikati ya Bahari ya Hindi.
Chanzo chetu kilisema mzigo ulioshushwa ni dawa za kulevya na kwamba boti hizo ndogo hufika eneo hilo hata mara mbili kwa wiki.
Uchunguzi
zaidi ulibaini kuwa dawa hizo huingizwa nchini kwa meli kubwa za
mizigo, hasa zile zinazotoka Iran, Pakistan na Afganistan.
Ukamataji polisi
Mwandishi
wetu aliwasiliana na polisi kuhusu njia hiyo ya kuingiza dawa za
kulevya nchini na jeshi hilo kuahidi kutoa majibu baada ya kufanya
ufuatiliaji. Kabla ya kutoa majibu juu ya ufuatiliaji huo, polisi
ilikamata meli kutoka Iran ikiwa na kilo 201 za heroini katikati ya
Bahari ya Hindi.
Msemaji
wa Polisi, Advera Senso alisema kama taarifa hizo zingeripotiwa katika
vyombo vya habari, ingekuwa vigumu kwa jeshi hilo kufanikisha kukamatwa
kwa wahusika.
Katika
wiki moja iliyopita, kilo 846 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh38
bilioni zimekamatwa kwenye mipaka ya Tanzania iliyoko katika eneo la
Bahari Kuu, kiwango ambacho ni kikubwa katika rekodi ya kukamatwa kwa
dawa za hizo.
Dawa hizo
zilikamatwa kati ya Februari 2 na 5 mwaka huu. Kilo 350 za heroini
zilikamatwa Februari 5 na wadhibiti wa dawa za kulevya wa Australia na
kilo 265 za heroini zilikamatwa na wadhibiti wa kimataifa wa Canada,
zote zikiwa zinaelekea Tanzania.
Dawa
nyingine ni kilo 201 za heroini zilizokamatwa ndani ya mpaka wa Tanzania
na Kikosi cha Polisi cha Wanamaji na kilo 30 zilizokamatwa Zanzibar.
Kamishna
Msaidizi wa Tume ya Kuratibu Dawa za Kulevya, Aida Tesha alisema, kiasi
hicho kikubwa kilikamatwa na wadhibiti wa bahari wa kimataifa
walioshirikiana na wadhibiti wa Tanzania.
“Huu
msimu ni wa wasafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya maji. Ni wakati
ambao wasafirishaji huleta dawa kwa wingi kwa sababu ya hali ya hewa.
Ieleweke kuwa zinazokamatwa ni asilimia 10, tu. Wapo wengi ambao
wanapita bila kubainika,” alisema Tesha.
Tesha
alisema wadhibiti wa kimataifa wanapokamata dawa huziharibu majini ili
kuwapa hasara wauzaji hao kwani wanapowaacha au kuzikabidhi kwa nchi
zilizo mipakani, zinaweza kuwafikia watumiaji. Mkuu wa Interpol, Tawi la
Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alisema hana
taarifa za kina za kukamatwa kwa kiasi hicho cha dawa za kulevya
isipokuwa wenzake wamemtumia taarifa hizo akiwa Algeria.
Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu alisema: “Nina
taarifa za Kilo 201 za heroini, ambazo watuhumiwa wake 12 Raia wa Iran
na Pakistan tayari wameshafikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yao”.
DCI
Mngulu alisema polisi wanaendelea na doria kwenye maeneo ya bahari kwa
kutumia mbinu zote ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua.
Kwa
upande wake, Kamishna wa Kikosi cha Polisi cha Kupambana na Dawa za
Kulevya, Godfrey Nzowa alisema: “Ni kweli hicho ni kiasi kikubwa
kukamatwa kwenye mipaka ya Tanzania na kinaonyesha kuwa watu hawa
wanadharau mipaka yetu, pia kunaonyesha kuwa tunafanya misako mikali.”
Fukwe nyingine
Uchunguzi
ulibaini kuwa fukwe nyingine ndogo za Dar es Salaam zinatumika kushusha
dawa za kulevya bila kugundulika kwa urahisi na kukwepa nguvu nyingi za
udhibiti ambazo zilikuwa zimewekwa katika viwanja vya ndege na mipaka
ya barabara.
Miongoni
mwa fukwe hizo ni Mbezi Jogoo, Dar es Salaam na eneo maarufu la Loliondo
ya Kigamboni ambako pia kunadaiwa kuwa na vitendo vya kutisha vya
ukahaba, biashara ya pombe haramu ya gongo na bangi.
Uchunguzi
umebaini pia kuwa katika eneo la Loliondo, wavuvi hutumika kubeba dawa
hizo kwa kutumia boti kutoka kwenye meli kubwa na kufikisha mizigo
husika nchi kavu ambako hupokewa na watu maalumu na kuanza usambazaji.
Katika
Pwani ya Bagamoyo, kiasi kikubwa cha dawa za kulevya hupitishwa na mara
nyingi huwa zimefungashwa kama makopo ya samaki waliosindikwa.
Mkoani
Mtwara, wasafirishaji hutumia fukwe ndogondogo kama za Mikindani
kuingiza dawa hizo ambazo baadaye husafirishwa kupelekwa Msumbiji.
Katika
Mkoa wa Lindi, maeneo ya Songo Mnara, Kilwa nayo yanatajwa kwamba
yanatumika kuingiza dawa za kulevya kutoka Dar es Salaam na Zanzibar.
Uchunguzi
wetu umebaini baadhi ya mbinu za kusambaza dawa hizo mitaani. Mizigo
hufungwa kwenye khanga au matenga ili isitiliwe shaka na kisha kupelekwa
mitaani kwa miguu na watu kati (middlemen) ambao hulipwa ujira kwa kazi
hiyo.
Katika siku ambazo kuna wasiwasi au hofu ya kukamatwa, mizigo hufukiwa ardhini hadi hali inapotulia.
Kamanda
wa Kikosi cha Wanamaji, ACP Mboje Kanga alisema kwa Tanzania ni kazi
ngumu kusimamia fukwe na uharamia unaofanyika, kwani ina fukwe zenye
urefu wa kilometa 1,424.
Ripoti ya
2013 ya Kitengo cha Uhalifu na Dawa za Kulevya cha Umoja wa Mataifa
(UNODC), inataja Bahari Kuu kuwa njia kuu zinazotumika kusafirisha dawa
za kulevya hadi Tanzania hasa Tanga na Zanzibar, kisha kusafirishwa kwa
boti ndogo kwenda Dar es Salaam na baadaye nchi za Kusini mwa Afrika.
Kadhalika,
taarifa ya 2011 ya kitengo cha dawa za kulevya iliyochapishwa katika
Ripoti ya Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Marekani inaeleza kuwa,
heroini huingia Tanzania kupitia Bahari ya Hindi ikitokea Afghanistan,
Iran na Pakistan kupitia Dubai.
MWANANCHI
Post a Comment