Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepanga ratiba ya Uchaguzi mdogo katika
jimbo la Kalenga katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambapo siku ya
kupiga kura itakuwa Jumapili ya Machi 16, mwaka huu na kampeni zitaanza
wiki ijayo.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi, Julius Mallaba alisema kuwa uteuzi wa wagombea ubunge,
utafanyika Februari 18, ambapo kampeni za uchaguzi zitaanza Februari 19
hadi Machi 15 mwaka huu.
"Tume
ya Taifa ya Uchaguzi imepokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuiarifu uwepo wa nafasi wazi ya
ubunge katika jimbo hilo, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo
hilo, William Mgimwa aliyefariki dunia Januari mosi mwaka huu," alisema.
Alisema
baada ya taarifa hiyo, Tume imepanga ratiba hiyo, ambapo wagombea
wanatakiwa kuwasilisha fomu za uteuzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo
la Kalenga siku ya uteuzi kabla ya saa 10.00 alasiri.
"Tume
inawataarifu wananchi wote pamoja na vyama vya siasa kufuata ratiba
iliyotolewa pamoja na kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi
kuanzia siku ya uteuzi hadi siku ya kupiga kura ili watimize haki yao ya
kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka," alisema.
Aidha,
Tume hiyo imewasisitiza wananchi wote katika maeneo husika, kujitokeza
kukagua taarifa zao wakati wa kuweka wazi Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura ili kuona kama kuna marekebisho madogo yanahitajika kufanyika,
kuwawezesha kupiga kura bila malalamiko yoyote. Mallaba alisisitiza
kwamba hakutakuwa na uandikishaji mpya wa wapiga kura.
Wakati
huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha rasmi Godfrey Mgimwa
(32) kuwa mgombea wa uchaguzi katika Jimbo la Kalenga mkoani Iringa huku
kikivitaka vyama vingine kutanguliza ustaarabu mara kampeni
zitakapoanza.
Akimtambulisha
mgombea huyo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema CCM imejipanga
kuchukua jimbo hilo kwa kishindo, kama ilivyofanya katika uchaguzi mdogo
wa madiwani, uliofanyika hivi karibuni, ambapo chama hicho kimeshinda
viti 24 kati ya 27 vilivyokuwa vikigombaniwa.
Aidha
Nape alisema pia CCM imemteua Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho upande
wa Tanzania Bara, Phillip Mangula kuwa Mratibu wa shughuli zote za
kampeni za chama hicho katika jimbo hilo, lililoachwa wazi kutokana na
kifo cha aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William
Mgimwa.
Nape
alisema wamepanga kamati ya siasa ya Wilaya ya Iringa Vijijini na
kamati ya siasa ya mkoa, kuwa ndizo zitakazosimamia kampeni za mgombea
huyo, zinazotarajiwa kuanza Februari 19 na baadae uchaguzi utakaofanyika
Mach 16 mwaka huu.
"CCM
haitavumilia vurugu za aina yoyote, kama ilivyojitokeza katika
uchaguzi wa madiwani sehemu mbalimbali, matarajio wenzetu watakuja na
ustaarabu wenye lengo la kufanikisha uchaguzi ufanyike salama," alisema
Nape.
Aidha,
alisema CCM itashinda uchaguzi huo kwa asilimia kubwa, kama ilivyofanya
mwaka 2010 iliposhinda kwa asilimia 85 ya kura zote zilizopigwa.
Post a Comment