Hivi punde mtandao huu umepata nafasi ya kufanya mazungumzo na Katibu
mkuu wa shirikisho la soka nchini Celestine Mwesiga ili kujua undani wa
suala la FIFA kumuidhinisha mchezaji Emmanuel Okwi kuichezea klabu ya
Dar Young Africans.
Katika mazungumzo hayo Mwesiga amesema kwamba ni kweli FIFA
wamemruhusu Okwi kuendelea kucheza soka wakati wenyewe wakishughulikia
madai ya vilabu vya Simba SC na Etoile Du Sahel.
"Kwanza ningependa kusema kwamba kazi ya FIFA kwenye hili suala
ilikuwa sio kumruhusu mchezaji kuichezea au kutoichezea Yanga, hilo
suala lipo chini ya shirikisho la soka nchini TFF.
"Kilichotokea ni kwamba kulikuwa na malalamiko ya klabu ya Simba SC,
juu ya uhalali wa uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kutoka SC Villa
kwenda Yanga na pili juu ya deni lao wanaloidai klabu ya Etoile Du
Sahel. FIFA wameridhika na suala la uhamisho wa Okwi kwenda Yanga kwa
maana ulifuata vigezo vyote na walipata ITC.
"Pia kuhusu suala la deni la Simba wanayoidai Etoile, FIFA imeeleza
kwenye email yake kwamba suala lipo pale pale lakini halina uhusiano na
suala la Okwi kusajiliwa Yanga. Sisi kama TFF tutaendelea kulifuatilia
kiundani kuhakikisha Simba wanapata haki yao."
Alipoulizwa kama suala la uhamisho wa Okwi kwenda Yanga halina tatizo
lolote, hivyo Okwi ataruhusiwa kuichezea Yanga, Mwesiga alisema:
"Kilichobaki sasa ni masuala ya ndani ya shirikisho. Tutaangalia kama
mchezaji husika amekidhi vigezo vya kuweza kushiriki kwenye michuano
mbalimbali hapa nchini, ikiwa atakuwa amekidhi basi tutakuwa hatuna
kipingamizi chochote."
Post a Comment