Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kikosi cha wachezaji 22
kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Namibia
(Brave Warriors) itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek,
Namibia.
Wachezaji
walioitwa katika timu hiyo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo
Mapunda (Simba) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki wa pembeni ni Edward
Charles (JKT Ruvu), Erasto Nyoni (Azam), Hassan Mwasapili (Mbeya City)
na Michael Aidan (Ruvu Shooting).
Mabeki
wa kati ni Aggrey Morris (Azam) na Kelvin Yondani (Yanga) wakati viungo
ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), David Luhende (Yanga),
Frank Domayo (Yanga), Jonas Mkude (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Markhiya
Sports Club, Qatar).
Washambuliaji
ni Athanas Mdamu (Alliance Mwanza), Haruna Chanongo (Simba), Khamis
Mcha (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-
DRC), Mrisho Ngasa (Yanga), Ramadhan Singano (Simba) na Thomas
Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaingia kambini
Machi 1 mwaka huu, kwenye hoteli ya Accommondia inatarajiwa kuondoka
Machi 3 mwaka huu kwenda Windhoek.
Wachezaji
ambao timu zao zinacheza mechi za mashindano ya kimataifa na ligi
wikiendi hii wataripoti kambini mara baada ya mechi zao kumalizika.
TAARIFA YA KLABU ZOTE TANZANIA YATAKIWA TFF
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zimewaagiza wanachama wake- vyama vya
mpira wa miguu vya mikoa kuwapatia orodha ya klabu zote za mpira wa
miguu zilizosajiliwa katika mikoa yao.
Orodha
hiyo inatakiwa kujumuisha namba ya usajili wa klabu, viongozi waliopo
madarakani kwa sasa pamoja na mawasiliano yao (namba za simu na anuani
za email) na eneo yalipo makao ya klabu husika.
Kwa
utaratibu huo, vyama vya mikoa vitakusanya taarifa za klabu zinazocheza
ligi ya mikoa, lakini wakati huo vinatakiwa kuwasiliana na wanachama
wake (vyama vya wilaya) kupata taarifa za klabu zinazocheza ligi za
wilaya na baadaye kuziwasilisha TFF.
Klabu
ambazo taarifa zake zitakuwa hazijawasilishwa TFF hadi Agosti mwaka huu
hazitaruhusiwa kushiriki ligi ya msimu wa 2014/2015 katika ngazi yoyote
ile.
RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa
na mkutano na waandishi wa habari juu ya programu ya mpira wa miguu kwa
vijana.
Mkutano
huo utafanyika kesho (Februari 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi
za TFF zilizopo ghorofa ya 3 katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden
na Ohio.
AZAM, ASHANTI UNITED KUKIPIGA VPL
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho
(Februari 26 mwaka huu) kwa mechi moja itakayochezwa Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi
itazikutanisha timu za Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa
ligi hiyo ikiwa na pointi 37 dhidi ya Ashanti United iliyoko nafasi ya
12 kwa pointi zake 14.
Post a Comment