* Asisitiza mfumo wa malezi, tamaa chanzo cha tatizo
Mzee Kingunge akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na blogu hii nyumbani kwake |
WAKATI serikali
ikitokwa povu la mdomo ikijigamba kuwa, itaongeza ukali dhidi ya
wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, japo tatizo hilo
linaloonekana kuzidi kuota mizizi, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge
Ngombale-Mwiru ameibuka na kufichua sababu za biashara hiyo kushindwa
kukomeshwa huku taifa likiendelea kushuhudia vijana ambao ni nguvu kazi
ikiangamia kwa tamaa za utajiri wa watu wachache.
Mwanasiasa huyo amesema ni vigumu biashara
hiyo kukoma nchini kama serikali na vyombo vyake vya dola
havitawashughulikia na kuwakamata 'vigogo' wa biashara hiyo pamoja na
kutengenezwa sheria kali itakayowafanya wahusika wajutie kujihusisha
nayo na kuwatia woga watu wengine wanaoanza au kutamani kuifanya
biashara hiyo.
Pia, amesema ni lazima serikali na jamii
kwa ujumla ishirikiane katika kuwapa malezi na elimu bora watoto na
vijana itakayowafanya wapende kufanya kazi na kujitegemea badala ya kuwa
tegemezi, wavivu na wanaopenda anasa na tamaa ya kutamani vitu ambavyo
hawana uwezo wa kuvipata
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
nyumbani kwake wiki iliyopita, Kingunge alisema tatizo la dawa za
kulevya ni kubwa na linaloliangamiza taifa, na kwamba licha ya kuwepo
kwa juhudi tatizo hilo limeshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa sababu
wanaonaswa ni watu wadogo tu, huku vigogo na wamiliki wakubwa wa mtandao
huo wakiachwa mitaani bila kuguswa.
Kingunge alisema pia hata sheria zilizopo
ni nyepesi na zisizowafanya watuhumiwa na biashara hiyo kuziogopa, japo
alidai asingependa kupona sheria za kuwapiga risasi au kuwanyonga kama
zinazofanywa na mataifa mengine ndizo zitumike nchini, lakini alitaka
sheria ziwe kali na zitakazowafanya wanaonaswa wakijishughulisha na
biashara hiyo kujuta wao na familia zao ambazo zimekuwa zikifahamu
nyendo zao na kunyamaza.
"Juhudi za kudhibiti suala hili zipo, ila
hazizai matunda kwa sababu wanaokamatwa ni watu wadogo, vigogo je kwa
nini hawaguswi? Ni vyema nguvu zikaelekezwa kwa vigogo na kuwekwa sheria
kali ya kuwatisha wanaojihusisha na biashara hiyo. Dawa za kulevya ni
janga na hatari kwa taifa. Ni tatizo la dunia nzima hivyo tunapaswa
kuonyesha ukali katika hili hapo tunaweza kudhibiti, ingawa kukomesha
kabisa ni vigumu," alisema.
Alisema pia kuna haja ya kujipanga upya
katika kuteua watu wa kushughulikia mapambano ya dawa za kulevya kwa
kuhakikisha wanateuliwa watu waaminifu na wasiojihusisha na mtandao wa
biashara hiyo vinginevyo vita dhidi ya dawa za kulevya zitakuwa kazi
bure tu.
Kingunge aliyewahi kushika nafasi
mbalimbali za uongozi ukiwamo uwaziri katika awamu zote nne za uongozi
tangu taifa lipate uhuru, alisema pia tatizo la biashara hiyo ya dawa za
kulevya limekuwa sugu kutokana na mfumo wa maisha uliopo kwa sasa
kuanzia kwenye malezi hadi katika elimu kwa watoto na vijana
inayowafanya wakuwe wakiwa wavivu na kuthamini fedha na anasa kuliko
kufanya kazi.
"Wazazi, walezi na hata serikali imekuwa
ikikumbatia na kuthamini sana watu wenye fedha, pia jamii imekuwa
inapenda anasa na njia za mkato za maisha badala ya mfumo wa malezi na
elimu unaowafanya watu wapende kufanya kazi kama tulivyokuwa tukihimiza
miaka ya nyuma. Hili liunafanya watu watafute kila njia kupata fedha
hata kwa njia haramu," alisema.
Kuhusu wimbi la wanawake nao kujiingiza
kwenye biashara hiyo na baadhi yao kunaswa katika mataifa ya nje,
alisema wanalazimika kwa sababu nao wanatafuta fedha kw akutambua bila
ya kuwa na fedha hawathaminiki wala kuonekana ni watu.
"Upo msemo kwamba mtu kitu asiyekuwa na
kitu kinyama cha mwitu, tusiwalaumu wanawake na vijana kuingia kwenye
biashara hii, wanatafuta fedha kwa sababu wamewaona wazazi na walezi wao
na hata serikali ikithamini na kuwapa heshima watu wenye fedha,"
alisema.
Mwanasiasa huyo alisema hata hivyo kuna
tatizo la jamii ya kitanzania kuangalia matokeo ya hali ya mambo badala
ya kuangalia chanzo cha suala hilo, akidai biashara ya unga imeanza
kitambo kirefu lakini iliwahusisha watu wachache lakini kutokana na
mabadiliko ya utandawazi vijana wamekuwa wakijifunza mambo mengi ya
upuuzi kupitia runinga na mitandao na kujikuta wakizama kwenye maovu.
NA MICHARAZO
Post a Comment