Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Ngeleja alisema wajumbe hao wana jukumu kubwa la kuwapatia Watanzania katiba mpya itakayokidhi mahitaji yao.
Alisema busara, hekima na utulivu vinapaswa kuwaongoza wabunge katika vikao vyao na wapime uzito wa hoja badala ya kumuangalia mtoa hoja au itikadi yake.
“Kuna wajumbe wamekamia kujikita kwenye muundo wa serikali…, wengine wanataka tatu, mbili na moja. Ningependa zaidi tujikite kuangalia rasilimali za taifa zinawanufaisha vipi wakulima, wavuvi, wafanyabiashara ndogo ndogo na wafugaji.
“Tuangalie tunaufufuaje ushirika ambao utawasaidia wakulima wazalishe na wauze bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi…, tuisaidie mahakama iwe na mfumo wake, ili iwe huru zaidi,” alisema.
Pia Ngeleja aliwataka vijana, hususani walioingia katika Bunge Maalumu la Katiba wawe mstari wa mbele kutoa mapendekezo ya katiba wanayoitaka badala ya jukumu hilo kuliacha kwa makundi mengine.
Alisema asilimia 60 ya watu nchini ni vijana, hivyo ni vema kundi hilo likashiriki kikamilifu kuandaa maisha yao.
“Vijana wana matatizo makubwa zaidi, sasa hii ni fursa muhimu ya kushiriki kuandika katiba mpya itakayosaidia kuweka mfumo imara wa kutatua matatizo yao,” alisema.
Ngeleja pia alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kufanya uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka makundi mbalimbali ambapo anaamini walioteuliwa wataweka mbele masilahi ya taifa.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment