. Wakati Rais Jakaya Kikwete akijiandaa kwenda
London Uingereza kuhudhuria mkutano wa kuokoa viumbe vilivyo hatarini
kutoweka duniani ukianza wiki hii, tatizo la ujangili limeweka wingu
zito kwa Tanzania.
Rais Kikwete ni kati ya viongozi wa nchi 50
watakaohudhuria mkutano huo, utakaokuwa chini ya wenyeji wa mwana wa
Wales na Waziri wa Mkuu wa Uinegerza, David Cameron,
Taarifa ya gazeti la The Mail on Sunday
la Uingereza la Februari 8, limeitaja Tanzania kama kinara wa ujangili
kwa kuua zaidi ya tembo 11,000 kwa mwaka, huku Rais wake (Jakaya
Kikwete) akielezwa kufumbia macho.
Pia, gazeti hilo limemhusisha Rais Kikwete kuwa na
urafiki na wafanyabiashara ya meno ya tembo, huku likiwahusisha
wafadhili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika biashara hiyo.
“Utawala wa Rais Kikwete umetawaliwa na mauaji ya
tembo yaliyovunja rekodi katika historia ya nchi yake. Kibaya zaidi,
wahifadhi wanasisitiza kuwa, ndani ya Serikali kuna viongozi
wanaoshiriki biashara hiyo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Katika mkutano huo, viongozi wa nchi 50 na
mawaziri wataweka mikakati dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori,
yenye thamani ya pauni 6 bilioni za Uingereza kwa mwaka zinazotumika
kufadhili magaidi.
Taarifa hiyo inasema kuna wafanyabiashara wakubwa wa Dar es Salaam wanaohusika na ujangili.
“Miongoni mwao ni matajiri wakubwa nchini,
wafadhili na wanachama wa CCM na ndugu wa karibu wa Rais Kikwete. Lakini
wanao marafiki wakubwa, huku majaji, waendesha mashtaka na polisi
hurubuniwa kwa urahisi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo inadai kuwapo kwa idadi kubwa ya
Wachina wanaofanya biashara ya mafuta nchini, huku baadhi yao
wakihusika na ujangili.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva
Rweyemamu alikiri kuona taarifa hiyo na kwamba, Rais Kikwete atahudhuria
lakini aliipuuza taarifa hiyo.
“Ni kweli Rais Kikwete atahudhuria huo mkutano,
lakini taarifa ni ya None sense, crap and malicious (ya kishenzi,
kipuuzi na ovu),” alisema Rweyemamu.
Juhudi za kumpata Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita muda mrefu bila
kupokelewa
Hata Naibu wake, Mahmoud Mgimwa naye hakupokea simu alipopigiwa.
Kuhusu CCM taarifa hiyo imeitaja idara ya
wanyapori kunuka rushwa huku ikisingizia kuuzwa kwa meno ya tembo
yaliyoko ghalani kwenye soko la kimataifa wakati lengo lao ni kupata
fedha kuisaidia chama hicho uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“ Wabunge, maofisa wa juu na wafanyabiashara,
wametajwa bungeni na kwenye vyombo vya habari, lakini uchunguzi
unapotezwa,” inaongeza.
Jitihada za kupata viongozi wa CCM hazikuzaa matunda.
Post a Comment