Dar es
Salaam. Kampuni ya Equator Suma JKT yenye ubia na Shirika la Uzalishaji
mali la Jeshi la Kujenga Taifa, imesaini mkataba na kampuni ya Farmer
kutoka nchini Poland utakaowezesha uzalishaji wa matrekta Tanzania.
Akizungumza
wakati wa kusaini mkataba huo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa
Equator Suma JKT, Ramesh Patel alisema kuwa mradi huo unagharimu Dola 70
milioni (Sh112 bilioni) ambazo ni mkopo kutoka Poland.
"Kwa muda
mrefu, Serikali imekuwa ikizungumzia maendeleo ya kilimo, sisi
tumeliona hilo na tulikuwa na mazungumzo na Kampuni ya Farm ya Poland,"
alisema Patel na kuongeza:
"Leo ni
siku ya kihistoria, kwani tunatia saini mkataba huu kuonyesha kuwa tuko
tayari kuzalisha matrekta hapa nchini na yataitwa kwa jina la
Kitanzania."
Alisema mradi
huo utaanza kwa kuzalisha matrekta machache ambayo yatafanyiwa
majaribio na Kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (Carmatec)
cha Arusha ili kuyathibitisha kwa ubora wa kimataifa.
Kwa
upande wake, mwakilishi wa kampuni ya Farm kutoka Poland, Robert Parcia
alisema kuwa wameichagua Kampuni ya Equator Suma JKT kutokana na ufanisi
wake katika kilimo.
"Leo ni
siku ya furaha kwetu kwani tumeingia kwenye hatua mpya. Tunatarajia
kwanza kuunganisha matrekta 1,200 kwa mwaka na hiyo itaanza mwaka 2017.
Yatakuwa matrekta ya kiwango cha juu na ubora wake utakuwa ni kama wa
Ulaya," alisema Parcia na kuongeza: "Tunashukuru kwa kuwa Serikali ya
Poland imetupa msaada wa kifedha ndiyo maana tunapata uhakika wa
mafanikio."
Naye
Mkurugenzi wa Equator Suma JKT, Robert Ndege alisema matrekta hayo
hayatakuwa kwa soko la Tanzania tu, bali kwa Afrika nzima.
"Wameichagua
Tanzania kwa sababu ya uzuri wa eneo la kibiashara. Tutazalisha
matrekta, siyo kwa soko la Tanzania tu, bali kwa Afrika nzima. Lengo
letu ni kuhamisha teknolojia hiyo, ikiwezekana asilimia 70 itengenezwe
kwao na sisi asilimia 30," alisema.
"Matrekta
hayo yatakuwa yakitolewa kwa mkopo na tutachagua mojawapo ya benki,
ambapo watu wataomba mikopo na kuirejesha hukohuko benki."
Alisema kuwa mradi huo utakuwa endelevu na hautaishia tu kuzalisha matrekta bali utakuwa pia ukizalisha magari aina nyingine.
"Kiwanda
hiki kimeanzishwa kwa ajili ya uzalishaji wa matrekta, lakini
tutazalisha na magari mengine. Tunategemea kuendelea na uzalishaji kwa
zaidi ya miaka 200 ijayo," alisema Ndege na kuongeza:
"Hiki
kiwanda kitakuwa cha Watanzania licha ya kusaidiwa na Poland.
Tutakachokifanya ni kuwafundisha Watanzania utaalamu huu ili tuzalishe
zaidi. Hata Poland wakiondoka, bado tutajitegemea."
chanzo:Mwananchi
Post a Comment