TUCTA imekuja na pendekezo hilo huku kukiwa na taarifa kwamba serikali imepandisha kiinua mgongo kwa wabunge kutoka sh milioni 43 za awali hadi sh milioni 160, pamoja na nyongeza ya mishahara na posho zao.
Pendekezo hilo la TUCTA lilitangazwa jana na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Nicolas Mgaya, wakati wa mkutano wa viongozi wa matawi wa shirikisho hilo jijini Dar es Salaam, uliofanyika katika ukumbi wa Msimbazi Centre.
Mgaya ambaye alikiri kwamba pamoja na pendekezo lao la awali la kutaka kima chini kiwe sh 315,000 kutotekelezwa na serikali, kiasi hicho kwa sasa hakifai na kimepitwa na wakati kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.
“Ikumbukwe kwamba tumekuwa tukidai kima cha chini cha sh 315,000 kwa mwezi tangu mwaka 2006, lakini hadi leo hakijaongezwa na tangu mwaka 2010 hadi 2012 hapakuwa na kima cha chini kinachotambulika rasmi kutokana na serikali kufuta tangazo lake Na. 223 ambalo liliweka vizuri mishahara na marupurupu ya wafanyakazi.
“Kutokana na shinikizo la TUCTA na vyama shiriki, bodi za mishahara za kisekta zilifanya utafiti na kubaini kima cha chini ambacho kingeweza kulipwa kwa sekta binafsi.
“Matokeo yake mwaka 2013, kima cha mshahara kwa sekta binafsi kilifikia kati ya sh 100,000 hadi 350,000 wakati kwa utumishi wa umma kilifikia sh 240,000,” alisema Mgaya.
Kutokana na maelezo hayo, katibu huyo aliweka wazi kwamba hata kama kima cha chini mwaka huu kitafika kama walivyobainisha mwaka 2006, yaani sh 350,000, kiwango hicho sasa hakitoshi kwani kimepitwa.
Kwa mujibu wa Mgaya, kima cha chini kinachoweza kwenda na wakati kutokana na hali halisi ya kupanda kwa gharama za maisha ni sh 720,000 kwa mwezi.
Wakati kwa sekta binafsi alisema baada ya kufutwa kwa tangazo la serikali, uchunguzi umebaini kuwa wafanyakazi wengi kati ya mwaka 2011/2012 wanalipwa kati ya sh 70,000 na 100,000 kwa mwezi huku hali ikizidi kuwa mbaya katika sekta ya kilimo, mashambani, hotelini, mgahawani, majumbani, ujenzi, usafirishaji na katika kampuni ndogondogo.
Punguzo la kiwango cha kodi
Mgaya alisema serikali kwa kutambua mahali pekee inapoweza kukusanya kodi kubwa na kwa urais ni kupitia mishahara ya wafanyakazi na hadi leo imezira kupunguza kiwango cha makato ya kodi hiyo kulingana na pendekezo la TUCTA.
“Badala yake ilichofanya serikali ni kupunguza kima cha chini tu cha tozo ya kodi hiyo mwaka 2011 kutoka asilimia 15 hadi 14 kwa mshahara wa 170,000/- yaani punguzo la asilimia moja wakati kwa mishahara ya kati na juu ni kama hapakuwepo na punguzo.
“Aidha mwaka 2012 hapakuwepo na punguzo lolote mbali ya serikali kutamka kuwa wafanyakazi wanaolipwa kima cha chini kisichozidi sh 170,000 hawatakatwa kodi ya malipo ya ajira na mwaka jana 2013 likawepo punguzo la asilimia moja tena kufikia asilimia 13.
“Eneo hili bado lina matatizo makubwa kwani TUCTA tulitaka kiwango cha makato kipungue kwenda asilimia tisa pale serikali itakapokuwa imepanua wigo wa walipa kodi,” alisema.
Maboresho ya pensheni kwa wastaafu
Mgaya alisema katika malalamiko yao ya uundwaji wa Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kiasi fulani yamefanyiwa kazi kwani pamoja na mabadiliko chanya yanayotokana na marekebisho ya sheria za mifuko, tatizo linaonekana kwenye eneo hili kwa sasa ni kasi ndogo ya utekelezaji wa maboresho hayo.
Madai ya Wafanyakazi
Kwa mujibu wa Mgaya, tangu mwaka 2010, Tucta na vyama shiriki imekuwa ikifuatilia madai ya wafanyakazi kwa njia mbalimbali, huku changamoto wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na kauli ya serikali kuwa haina uwezo wa kulipa kima halisi cha mshahara na kuona kuwa kupunguza kiwango cha kodi ni pigo kwa mapato yake.
Pia alisema baadhi ya waajiri wenye uwezo wa kulipa mishahara mizuri hawana msukumo wa kufanya hivyo kwani hulinganisha kile wanacholipa na kinacholipwa na serikali kwa mfano sh 200,000 na 300,000 wanazolipa wanadai wako juu ya kile kinacholipwa na serikali.
Tatizo la ajira
Mgaya alisema ukosefu wa ajira unachangia ongezeko la ajira za muda na kibarua na kukubaliana na baadhi ya viongozi ambao waliwahi kusema ukosefu wa ajira ni bomu linalosubiri kulipuka.
“Kauli hiyo ni kweli kabisa na hii ni kutokana na ongezeko la idadi kubwa ya vijana wanaomaliza shule, vyuo na kuingia mitaani kusaka ajira kuzidi kuongezeka kila mwaka.
“Miongoni mwa wanaotafuta ajira ni watoto wa wafanyakazi ambao kwa namna moja au nyingine wanaendelea kuwa mizigo kwa mfanyakazi mwenye kipato kidogo, hata baada ya kujitahidi kujibana kumsomesha mtoto huyo.
Masuala ya Kijamii na athari kwa wafanyakazi
Kupanda kwa bei ya nishati, umeme na mafuta ya petroli, mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kitanzania, Mgaya alisema ni kati ya maeneo ambayo yanachangia sana katika kuyafanya maisha ya wafanyakazi kuwa magumu.
Hata hivyo, wakati Mgaya akiwa anapigia debe kima hicho kipya, baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo wanaonekana kuwa na wasiwasi kukubalika ukizingatia kuwa cha awali cha sh 315,000, hakijatekelezwa.
Mmoja wa wajumbe ambaye ni mwakilishi wa Chama cha Walimu, Joyce Galikika, alisema kwa muda sasa viongozi wao wamekuwa kimya kudai haki zao hali inayowapa hofu na kujiuliza maswali yasiyokuwa na majibu.
Galikika alisema alitegemea hatua ya serikali kutotekeleza pendekezo la kuongeza kima cha chini kuwa sh 315,000 viongozi hao wangekuja na msimamo, lakini alishangaa kuona wakipendekeza kima kingine cha chini kuwa sh 720,000.
Kiinua mgongo cha wabunge
Wakati kukiwa na habari za kuongezwa kwa kiinua mgongo cha wabunge kutoka sh milioni 43 za awali hadi sh milioni 160, Mgaya alisema kama habari hizo ni za kweli, ni dhuluma iliyopitiliza.
Alisema inasikitisha kuona watu waliopewa dhamana kuwatetea wanyonge, ndio wanakuwa wa kwanza kujipendelea.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment