Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bw. Adoh Mapunda (katikati)
akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu namna wilaya hiyo
inavyoendelea kuboresha huduma za jamii kwa kutumia rasilimali
mbalimbali zilizo katika wilaya hiyo.Kushoto ni diwani wa kata ya Kikole
Mwl.Haji Mulike na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo
Bw. Ali Mohamed Mtopa.
Ramani
ya hospitali ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa itakayojengwa wilayani
kilwa kwa nguvu za halmashauri na wadau wa Maendeleo. Picha na Aron
Msigwa - MAELEZO.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO,Dar es salaam.
Uongozi
wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa umesema kuwa utahakikisha
rasilimali zote zinazopatikana katika wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na
gesi asilia zinatumika kuleta maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bw. Adoh Mapunda wakati akitoa ufafanuzi
kwa waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii kwa kutumia
rasilimali mbalimbali zilizo katika wilaya hiyo.
Akiwa
ameambatana na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo akiwemo mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya hiyo, watendaji na baadhi ya Madiwani
wanaohudhuria kikao kazi jijini Dar es salaam, Bw. Mapunda amesema
kuwa halmashauri hiyo imejipanga kupunguza utegemezi wa fedha toka
serikali kuu kwa kupanua wigo wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya
vya mapato.
Amevitaja
vyanzo hivyo kuwa vyanzo hivyo vipya ni pamoja na ushuru wa zao la
Ufuta ambalo sasa mapato yake yamefikia milioni 595, mauzo ya viwanja na
ushuru wa Gesi asilia inayozalishwa katika kijiji cha Songosongo ambayo
sasa inatoa asilimia 0.3 ikiwa ni ushuru wa tozo la huduma.
Akifafanua
kuhusu mapato hayo Bw. Mapunda amesema kuwa katika zao la ufuta
asilimia 20 ya pato hilo inarudishwa vijijini na halmashauri hiyo na
kuongeza kuwa mapato ya ushuru wa huduma unaolipwa kwa halmashauri
kutokana na shughuli za gesi za kampuni ya PAN AFRICAN ENERGY katika
eneo la Songosongo huchangia 20% kwa ajili ya maendeleo ya eneo hilo.
“
Kuanzia mwezi Septemba 2012 Baraza la Madiwani lilipendekeza tuanze
kupeleka asilimia 20 kwenye kijiji cha Songosongo kutokana na malipo ya
kampuni ya PAN AFRICAN ENERGY kiasi cha shilingi milioni 811ambapo hadi
sasa tumeshapeleka jumla ya shilingi milioni 139 na tunajiandaa kupeleka
kiasi kingine kilichobaki cha shilingi 22” ameeleza Bw. Mapunda.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii mkurugenzi huyo amesema
kuwa wilaya ya kilwa inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya
Maji Safi, Umeme, Elimu, mkakati wa kukuza ajira, kuimarisha ulinzi na
usalama kwa kujenga kituo cha polisi cha kisasa kitakachogharimu
shilingi milioni 625 na uboreshaji wa huduma za afya.
Ameongeza
kuwa katika kuboresha huduma za afya wilaya hiyo imeshatenga eneo la
hekari 30 kwa ajili ujenzi wa hospitali ya kisasa yenye hadhi ya
kimataifa itakayotoa huduma ya afya kwa wakazi wa wilaya hiyo.
“Mradi
huu wa hospitali ya kisasa utaanza haraka iwezekanavyo ndani ya mwaka
huu hii ikiwa ni mchango wa rasilimali za eneo letu pia kwa kushirikiana
na kampuni inayochimba gesi, pia tunajiandaa kwa ujenzi wa ukumbi wa
kisasa wa kimataifa utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8”
Aidha
katika hatua nyingine Bw. Mapunda ameeleza kuwa halmashauri ya Kilwa
inaendelea na mikakati ya kuimarisha miundombinu ya barabara ili
kuimarisha usafiri wa ndani wa wilaya hiyo, kufanya juhudi ya
ukamilishaji wa miundombinu ya ulinzi na usalama ili kuimarisha hali ya
ulinzi na usalama wa miundombinu iliyopo.
Post a Comment