Mmoja
wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (aliyevaa fulana nyeusi)
akihoji uimara wa sehemu ya kutulia ndege wakati walipofanya ziara ya
kujionea maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Mtwara.
Timu ya Ukaguzi
wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara kwa ajili ya kujionea
maendeleo ya uwanja huo.
Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara, Mhandisi Mugasa Mlondo akitoa maelezo juu uimara na ubora wa uwanja wake wakati Timu yaUkaguzi
wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya
ziara kwa ajili ya kujionea maendeleo ya uwanja huo. Picha na Saidi Mkabakuli
************************************
Na Saidi Mkabakuli
Katika
kukabiliana na kasi ya maendeleo ya ukuaji wa uwekezaji katika maeneo
ya viwanda vikubwa na biashara za huduma mkoani Mtwara, Serikali imesema
kuwa kuna haja ya kuuimarisha Uwanja wa Ndege wa Mtwara ili kuongeza
ufanisi katika utoaji wa huduma kwa watumiaji wa uwanja huo, hasa
kufuatia kugundulika kwa gesi mkoani humo.
Hayo yamebainishwa mmoja
wa viongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati ilipofanya ziara kwa
ajili ya kujionea maendeleo ya uwanja wa huo.
Bibi Mwanri alisema kuwa Serikali
inaendelea kufanya tathmini na mikakati mbalimbali itakayopelekea
kuuimarisha uwanja wa ndege wa Mtwara ili kuweza kuhudumia uwekezaji
mkubwa unaofanywa na makampuni mbali mbali ya ndani na nje ya nchi
mkoani humo. Aliongeza:
“Tathmini
ya awali inaonesha kuwa miradi mingi ipo mkoani Mtwara kufuatia
kugundulika kwa gesi hivyo kuna haja ya dhati ya kuuimarisha uwanja wa
ndege wa Mtwara kwa lengo la kutoa huduma za uhakika wakati huu wa
mfumuko wa kiuchumi mkoani Mtwara,” alisema Bibi Mwanri.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof.
Longinus Rutasitara ambaye alikuwa kiongozi mwenza wa ukaguzi, alisema
kuwa kuna haja ya dhati ya kuwekeza katika uwanja huo ili kukabiliana na
kasi ya maendeleo ya mkoa wa Mtwara kufuatia wawekezaji wengi kuendelea
kumiminika na kuwekeza mkoani humo.
“Uwanja
wa ndege wa Mtwara una fursa za nyingi za kuhudumia wafanyabiashara wa
ndani na nje ya nchi, hakika ni lango la biashara hasa kipindi hiki cha
uchumi wa gesi mkoani Mtwara, hivyo uendelezaji wa uwanja huu ni jambo
lisilo epukika,” alisema Prof. Rutasitara.
Kwa
mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 -
2015/16), Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa
katika miundombinu ya nishati, usafirishaji (bandari, reli, barabara na
usafiri wa anga), maji (safi, taka na ya uzalishaji) na TEHAMA.
Serikali
imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa
kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni
kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji
mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi.
Mpango
wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja
wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa
utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na
tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa.
Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025
Post a Comment