**************
Wakati tukio la kupotea kwa ndege ya Shirika la Ndege la
Malaysia, MH370, linaendelea kuitikisa dunia, imebainika kuwa Tanzania
si jambo jipya kutokana na kuwapo kwa kumbukumbu ya matukio manne
tofauti kama hayo katika miongo minane iliyopita.
Ndege hiyo ya Malaysia ilipotea wiki mbili
zilizopita ikiwa na abiria 227 na wafanyakazi 12 huku juhudi za
kuitafuta zinazofanywa na nchi 26 zenye uwezo mkubwa wa kiuchunguzi
zikiwa hazijazaa matunda.
Kwa matukio ya Tanzania, Mkaguzi Mkuu wa Ajali za
Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihura amesema katika
mahojiano maalumu na mwandishi wetu kuwa Tanzania imewahi kuingia katika
kumbukumbu za ndege ndogo kupotea na baadhi hazikuonekana kabisa na
nyingine zilionekana baada ya miaka kadhaa kupita. Ndege ya kwanza
kupotea ilikuwa mwaka 1937 iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda Madagascar.
Ilikuwa na abiria wanane na haijaonekana hadi leo.
Mbali na tukio hilo ambalo limedumu kwa miaka 77
sasa, Nyamwihura alisema tukio la pili ni la mwaka 2003 wakati ndege
iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda Zambia ilipopotea ikiwa na raia wawili
wa Afrika Kusini, nayo pia haijaonekana hadi sasa.
Mkaguzi huyo alisema katika matukio mengine
mawili, ndege zilizopotea zilionekana baadaye. Mwaka 1997, ndege ndogo
iliyokuwa na abiria mmoja ilipotea katika bonde kwenye kilele cha Kibo,
Mlima Kilimanjaro baada ya kutumbukia kwenye korongo na kuganda kwenye
barafu bila kuonekana hadi baada ya miaka sita. Hata ilipoonekana
haikuwezekana kutolewa.
“Ndege ile ilikuwa ikitoka Nairobi kwenda Zanzibar ikiwa na rubani wa Kitanzania peke yake,” alisema Nyamwihura.
Ndege nyingine iliyoingia katika orodha hiyo ni
ile iliyoanguka katika Ziwa Victoria mwaka 1976 ikiwa na abiria 12
ambayo ilionekana miaka miwili baadaye.
Kwa nini ndege zinapotea?
Swali hili linajibiwa na Nyamwihura akisema sababu
kubwa ya matukio hayo ni mabadiliko ya hali ya hewa na kuharibika kwa
miundombinu, mambo ambayo husababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya
waongoza ndege na marubani.
“Matukio mengi kama haya ni kuwa ndege hugonga
milima na kuanguka. Zikianguka sehemu za milima ni vigumu kupatikana kwa
sababu wakati mwingine huganda katika barafu au kuzama kwenye
makorongo,” alisema.
Alisema hata ndege zinazoanguka kwenye maji, pia ni vigumu kuonekana kutokana na kina kirefu au barafu.
Mtaalamu huyo alisema kuna baadhi ya ndege ambazo
hupotea kutokana na rubani kukata mawasiliano kwa makusudi kwa sababu
ama za kigaidi au magendo
Kwa habari kamili tembelea http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Ndege-nne-ziliwahi-kupotea-Tanzania/-/1597296/2252502/-/4re4yt/-/index.html
MWANANCHI
Post a Comment