Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es salaam.
SERIKALI
imetoa wito kwa wananchi na vyombo vya habari kushiriki katika shughuli
na matukio mbalimbali ya maadhimisho ya Sherehe za miaka 50 ya
Muungano yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini ambayo kilele
chake kitakuwa tarehe 26,April 2014, siku ya maadhimisho ya sherehe
hizo.
Akizungumza
na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam, Msemaji wa Serikali na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene amesema kuwa
maadhimisho ya mwaka huu ambayo ni ya kipekee yanaongozwa na kauli mbiu
isemayo Utanzania wetu ni Muungano Wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na
Kuudumisha yanaambatana na matukio mbalimbali yanayozihusisha wizara na
taasisi mbalimbali za Muungano.
Amesema
wizara na taasisi hizo zitashirikiana na vyombo vya
habari kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mafanikio makubwa
yaliyopatikana katika kipindi chote cha uhai wa Muungano ikiwemo umoja,
amani na mshikamano.
“Sisi
tumeungana miaka 50 iliyopita,huu ni muungano pekee uliobaki Afrika wa
kupigiwa mfano na unaoendelea kudumu haya ni mafanikio makubwa “
amesema.
Ameeleza
kuwa katika kipindi chote cha muungano watanzania wamebaki kuwa wamoja
kwa kuhakikisha kuwa Muungano unalindwa , kuenziwa na kudumishwa na
kizazi cha sasa na vile vitakavyofuata na kuongeza kuwa mwananchi
anawajibu wa kuyalinda mafanikio hayo.
“Watanzania tuna
kitu cha kusherehekea kwa sababu miaka 50 ya Muungano kwa sababu
tumebaki kuwa wamoja. Tanzania ni nchi moja ni lazima wananchi
waliohusika kuunda Muungano huu tuendelee kuwakumbuka na ni sehemu ya
sherehe hii”
Aidha
amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana baadhi ya watu wamekuwa
wakibeza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha Muungano kwa
kulaumu na hata kutumia vyombo vya habari kuharibu taswira ya mafanikio
hayo jambo ambalo halina msingi wala ukweli wowote kutokana na
matunda yanayoonekana sasa ya kuwafanya watanzania kuendelea kuwa
wamoja.
Ameeleza
kuwa vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuendelea kueleza mambo
makubwa yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika ndani na nje ya nchi na
kufafanua kuwa Tanzania ina uzoefu mkubwa wa masuala mbalimbali katika
Nyanja ya ushirikiano.
Amesema
Tanzania imekuwa na ushirikiano na mataifa mbalimbali katika kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kushirikiana na nchi nyingine jambo
linaloonyesha ukomavu wa Muungano na utayari wa ushirikiano wa Tanzania
na mataifa mengine.
“Ukiangalia
sisi tuna miundombinu ya reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA
inayokwenda nchi ya Zambia hii yote, miradi hii ni mikubwa iliyojengwa
kwa ushirikiano hili tu linaonyesha kuwa sisi tuna uzoefu mkubwa katika
masuala ya muungano hasa kufanya kazi kwa pamoja katika masuala haya
ya Muungano”
Amesema
Tanzania inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya kiuchumi
kwa kushirikiana na mataifa jirani ikiwemo mkataba wa ujenzi wa reli
uliosainiwa hivi karibuni kati ya Tanzania na Burundi.
Kuhusu wizara
na taasisi za muungano zitakazoshirikiana na vyombo vya habari kutoa
taarifa kwa umma kuhusu masuala mbalimbali kuhusu taasisi na wizara
husika kuanzia mwezi huu amesema ni pamoja na Wizara ya Kazi na
Utumishi wa Umma na Ofsi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Tume ya uchaguzi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Nyingine
ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano
Zanzibar,Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na Bodi
ya Mikopo ya Elimu ya juu.
Wizara
na Taasisi nyingine ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar,Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Katiba na Sheria,
Taasisi za Wizara ya Fedha (Muungano) za Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Bodi ya Mikopo ya Nje, Benki Kuu ya Tanzania, Taasisi ya
Kupambana na Fedha Haramu na Mamlaka ya Bima.
Aidha
amesema kuwa kuelekea kilele cha sherehe hizo kutakuwa na fainali
tamasha kubwa linalohusisha vikundi mbalimbali vya muziki na
taarabu ambapo rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi atakuwa mgeni rasmi
katika eneo la viwanja vya Mnazi mmoja pia kutakuwa na kongamano kuhusu
Muungano wa Bara la Afrika ambalo litafanyika katika ukumbi wa Benki Kuu
ya Tanzania (BOT) ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu mstafu Dkt.
Salim Ahmed Salim.
Matukio
mengine ni pamoja na fainali za kongamano la wazi kuhusu Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar litakalofanyika Zanzibar tarehe 19 mwezi
huu,Hotuba na zoezi la utoaji wa nishani litakalofanywa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na mkesha
mkubwa wa miaka 50 ya Muungano katika viwanja vya mnazi mmoja Dar es
salaam na viwanja vya Mwaisla, Zanzibar.
Post a Comment