SERIKALI
wilayani Rungwe mkoani Mbeya imebaini mbinu mpya za usafirishaji wa pombe
haramu za viroba toka nchini Malawi inazofanywa
na wafanyabiashara wasio waaminifu ambao husafirisha viroba hivyo kutoka Malawi
kupitia njia za panya zilizopo boda ya kasumulu wilayani Kyela kwenda mikoani.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo ofisini kwake mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispin Meela
alisema kuwa mbali na kupiga marufuku uingizaji wa pombe hizo nchini lakini
bado kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakibuni mbinu mpya ya
kusafirisaha pombe hizo haramu ambazo tayari wamezibaini.
Alisema
kuwa katika uchunguzi uliofanywa na kamati yake ya ulinzi na usalama juu ya
kuzibaini njia hizo tayari walikwisha wabaini wafanyabiashara ambao walikuwa
wakisafirisha pombe hizo katika mifuko ya sarfeti na juu yake wamekuwa wakiweka
nafaka ili wasibainike na kwamba njia nyingine hutumiwa na akina mama ambao
hupakata viroba hivyo ambavyo huviviringisha kwenye vitenge mithiri ya mtoto
bila ya kugundulika.
Aliongeza
kuwa mbali na maafisa wa TFDA kuwatoza faini wamiliki wa magari yanayokamatwa
yakiwa yamebeba na kusafirisha pombe hizo pamoja na kutaifisha pombe hizo haramu kwa
wafanyabiashara ambao hukamatwa lakini haijasaidia bado pombe hizo zinazidi
kuingia nchini kupitia boda hiyo ya kasumulu iliyopo wilayani Kyela.
Kutokana
na hali hiyo mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa alikwisha keti na kamati ya
ulinzi na usalama na kujadili namna ya kukomesha na kudhibiti usafirishaji huo
kwa kutunga sheria kandamizi itakayowabana wamiliki wa magari wanaopewa tenda
ya kusafirisha bidhaa hizo haramu na wafanya biashara wenyewe kwa lengo la kuokoa
nguvu kazi ya Taifa la vijana ambao wamekuwa wakipata madhara juu ya matumizi
ya pombe hizo.
Alizitaja
sheria hizo kuwa ni kutaifisha gari au pikipiki ambayo litakamatwa ikiwa
limebeba pombe hizo ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani wafanyabiashara
watakao kamatwa wakiwa wanasafirisha au kuuza pombe hizo haramu zilizopigwa
marufuku na Serikali.
Meela
aliongeza kuwa katika jitihada zao za awali za uthibiti wa pombe hizo wamefanya utafiti wa miezi mitatu na kubaini
kuwa wamefanikiwa kwa asilimia 80 kuthibiti
matumizi ya pombe hizo kwa wilaya ya Rungwe na Kyela na kuwa tayari ajali za
barabarani zimepungua kwa madereva wa badabada waliokuwa wakitumia pombe hizo
wakiwa kazini ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya vijana waliokuwa wakitumia
vinywaji hivyo.
Alisema
kuwa katika operesheni waliyoifanya kwa miezi mitatu iliyopita tayari wamefanikiwa
kukamata katoni 3,000 ambazo zitateketezwa mwishoni mwa wiki hii na kuwafikisha
mahakamani wafanyabiashara 6 waliokamatwa wakati wakisafirisha pombe hizo na
kuwa sheria itafuata mkondo wake ili iwefundisho kwa wengine ambao watakaidi
amri ya serikali ya upigaji marufuku pombe hizo hatarishi kwa maisha ya
wanadamu.
Aliyataja
madhara wanayoyapata wanadamu pindi watumiapo pombe hizo kuwa ni kuishiwa nguvu
za kiume,kukosa hamu ya kula,tendo la ndoa,kuungua ini,kuchanganyikiwa na
kupoteza kumbukumbu na hatimae kifo,na kwamba tayari ameiagiza kampuni ya
kizalendo inayotengeneza pombe za konyagi isambaze katika wilaya hizo kwa kuwa
hazina madhara zimedhibitiwa na TBS.
Aliongeza
kuwa mpango mkakati waliupanga katika wilaya yake kwa kushirikiana na viongozi
wa wilaya ya Kyela ambayo ndiyo uchochoro wa kupitishia pombe hizo ni kuanza
operesheni ya pamoja ya duka hadi duka na kuweka maafisa wa polisi katika njia
zote za panya zilizopo kwenye kivuko cha mto songwe unaotenganisha nchi ya
Tanzania na Malawi kwa lengo la kutokomeza kabisa matumizi ya pombe hizo.
Post a Comment