Machi 23 mwaka 1995 ni siku isiyosahaulika kwa wapenzi wa
muziki wa zamani nchini. Siku hiyo ndipo tulipompoteza mwanamuziki kipenzi chetu,
Marijani Rajabu. Alizikwa kesho yake yaani Machi 24 kwenye makaburi ya Kisutu.
Historia ya gwiji huyu inaanzia Machi mwaka 1955. Mara baada ya kumaliza elimu
yake ya Sekondari, Marijani alijitosa moja kwa moja kwenye muziki licha ya kuwa
awali aliwahi kuwa Mlinda Mlango hodari kwenye timu mbalimbali ikiwemo Timu
yake ya Shule. Mwaka 1970 alikuwa miongoni mwa wanamuziki wa bendi ya STC Jazz
na kushiriki kuimba na kutunga vibao kadhaa. Ewe mwana inaweza kuwa ndio wimbo
maarufu zaidi. Mwaka 1972 alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa
wakati huo ilikuwa inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao
kiongozi wakati huo alikuwa Ali Rajabu. Kuingia kwa Marijani kukaleta mapinduzi
mapya kabisa ndani ya bendi na muziki wake. Ikiathiriwa zaidi na muziki wa
vijana wakati huo, muziki wa Soul, Trippers ambayo punde ikaongeza neno Safari
kwenye jina lake ilianza kupiga na kutunga nyimbo zake kali na ambazo hata leo
hii bado zinakumbukwa. Wimbo Georgina ni mfano tu. Marijani alishiriki kutunga,
kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga gitaa kwa baadhi ya
nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba.
|
Safari Trippers-Marijani wa pili toka kulia waliosimama. Wa kwanza mwenye kofia ndie mtunzi wa wimbo Georgina- Uvuruge |
Mwaka 1976, Marijani
na baadhi ya wanamuziki wa Trippers waliamua kuihama bendi na kwenda
baadaye
kuasisi Dar es salaam International chini ya umiliki wa Mzee Zakaria
Ndabemeye
ambaye bado yu hai hadi sasa. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Abel
Baltazar kutoka Msondo, Kassimu Mponda kutoka Trippers, Abdallah Gama,
Joseph
Mulenga, Haruna Lwali na George Kessy Omojo waliokuwa wanapiga muziki
Magot
pale, Said Mohamed kutoka Polisi Jazz, Cosmas Chidumule kutoka Urafiki,
Belesa
Kakere kutoka Biashara Jazz, Joseph Bernard kutoka Trippers, Ali Rajabu
kutoka
Trippers, na King Michael Enock kutoka Dar es salaam JazzAkiwa Dar Inter
alishiriki kutunga nyimbo mbili, Betty na Sikitiko. Hata hivyo kama
waswahili
wanavyosema mafahari wawili hawakai zizi moja ndivyo ilivyotokea kati
yake na
Abel Balthazal kiasi cha hatimaye Marijani kufukuzwa ndani ya bendi
kutokana na ubishi kuhusu wimbo aliotunga Marijani, kuna maelezo kuwa
wimbo ulionekana unafanana na wimbo fulani toka Kongo na hivyo Marijani
akatakiwa aubadilishe na ndipo ugomvi ukaanza. Hata hivyo mwishoni
mwa mwaka 1978, Marijani alirejeshwa tena kundini kutokana na rundo la
wanamuziki wa Dar Inter kuihama bendi kwa kishindo kikubwa na kwenda
kuifungua
bendi mpya kabisa ya Orchestra Mlimani Park. Aliporejeshwa Marijani
alikuja na
wanamuziki wengi wapya wakati huo kama akina Christopher Kasongo,
Mohamed
Tungwa, Mafumu Bilal, Hamis Milambo, Athuman Momba, Mzee Alex Kanyimbo
na
wengine na kuja na mtindo wa Super Bomboka. Katika kudhihirisha hasira
zake kwa
Abel, Marijani alimtungia Abel wimbo wa kumnanga ukiitwa Kidudu mtu
ambao hata
hivyo RTD waliukataa kuurekodi, jambo lililokuwa kawaida enzi hizo kwa
redio kukataa wimbo. Sifa nyingine ambayo Marijani alikuwa nayo ni
kuibua
wanamuziki chipukizi kama alivyofanya mwaka 1983 alipomuibua kutoka
Tanga
kijana Mkuu Waziri Kungugu Kitanda Milima almaaruf Fresh Jumbe ambaye
kwa
hakika kabisa Marijani hakujutia kumchukua kijana huyo. Alimuamini
kupita maelezo
kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa akimuachia bendi aongoze na yeye
anapumzika
nyumbani. Mbali na Fresh, wanamuziki wengine ni kama vile Tino Masinge,
Mohamed
Mwinyikondo, Juma Choka na wengine kibao.
|
Tanzania All Stars..Marijani wapili toka kulia |
Hata hivyo safari ya Dar Inter
ilikoma mwaka 1987 kutokana na sababu za kawaida za kufa kwa bendi
lakini kubwa
ni uchakavu wa vyombo. Hata hivyo Marijani aliendelea kufanya muziki na
kwa
kipindi kifupi amewahi kucheza na Kurugenzi ya Arusha na Mwenge Jazz
ambayo
alirekodi nayo wimbo mmoja wa Ukimwi. Mwaka huohuo wa 1987 Marijani na
Muhidin
Maalim Gurumo waliliongoza kundi la wanamuziki zaidi ya 50 kutunga
nyimbo
maalum hasa kwa maadhimisho ya miaka 10 ya CCM na 20 ya Azimio la
Arusha.
Naizungumzia Tanzania All Stars. Aidha mwaka 1994 aliwahi mkurekodi zong
zing
na marehemu Eddy Sheggy. Bendi yake ya mwisho ilikuwa ni Africulture ama
Mahepe
Ngoma ya Wajanjailiyokuwa mali ya Rogers Malila, alikokuwa na wanamuziki
kadhaa kama akina
Hassan Kunyata na wengine. Bado Marijani ataendelea kukumbukwa na
wapenda
muziki kote nchini na hata Afrika kwa ujumla kwa nyimbo zake zenye
mafundisho
na tamu huku akienzi utamaduni na ngoma za kwao Kigoma.Chini hapa ni
video ya Marijani akipiga gitaa na kuimba wimbo aliotunga enzi za Dar
International hapa alikuwa na kundi la Africulture katika ukumbi wa
Mango.
Credit Uncle Kitime
on Sunday, March 23, 2014
Post a Comment