Wafanybiashara
na Wachimbaji waliowakilisha wenzao katika Maonesho ya 53 ya Bangkok
Gems and Jewelry Fair’ wakiwasikiliza wageni waliotembelea banda la
Tanzania kuona aina mbali mbali za madini ya Vito na Usonara
yaliyowasilishwa katika maonesho hayo.
Mthamini
wa madini kutoka idara ya Uthamini wa madini ya Almas (TANSORT) Bw.
Edward Rweymamu (katikati), akiwaeleza jambo wageni waliotembelea banda
la Tanzania katika maonesho hayo. Wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni
Mratibu kutoka Kituo cha ‘Tanzania Geomological Center’ (TGC), Bw. Musa
Shanyangi na wa kwanza kulia ni Mthamini wa Madini kutoka Idara ya
uthamini madini ya almsi (TANSORT), Wizara ya Nishati na Madini Bibi.
Teddy Goliama.
Mwandishi
wa habari hii (Kushoto) Asteria Muhozya, akifanya mahojiano na
wafanyabiashara wa madini walioshiriki maonesho ya Vito na Usonara ili
kutaka kujua namna walivyofaidika na ushiriki wao katika maonesho hayo.
Anayeongea ni Bw. Jeremiah Simioni Mfanyabiashara kutoka Kampuni ya Tom
Gems na katikati ni Mfanyabiashara Mhe. Dorah Mushi kutoka Kampuni ya
H.B Mining Company.
…………………………………………………………………..
Na Asteria Muhozya, Bangkok
Wafanyabiashara
na wachimbaji wa madini Tanzania wameelezea kufurahishwa na ushiriki
wao katika maonesho ya 53 ya madini ya vito na usonara, Bangkok,
kutokana na kupata fursa ya kulifikia soko la madini kimataifa.
“Wachimbaji
wa madini ya vito na usonara, watarajie kupata masoko ya madini yao
nje. Wananunuzi wa bidhaa zetu wapo na wana imani kubwa na madini yetu.
Jambo kubwa tulilolihitaji ilikuwa kujua masoko na namna ya kupata
taarifa mbalimbali. Tunafurahi kwa hilo, tumefanikiwa. Amesema
Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Vito Tanzania, Bw. Gregory Kibusi.
Aidha,
Aliongeza kuwa, ushiriki wake katika maonesho hayo, umewawezesha kupata
sehemu ambazo zitawasaidia wachimbaji kupata taarifa mbalimbali,
ikiwemo taarifa za bei za madini hali ambayo itawawezesha kupata taarifa
sahihi tofauti na awali, ambapo walikuwa wakizipata kutoka vyanzo
visivyo rasmi. Hivyo, amewataka wachimbaji kufanya maandalizi mazuri kwa
ajili ya maonesho ya madini ya vito na usonara yanayofanyika kila mwaka
jijini Arusha.
Akizungumzia
namna alivyonufaika na maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
madini ya H.B Bw. Harry Mushi, alieleza kuwa, maonesho hayo,
yamewasaidia kujua nafasi zao kibiashara. Vilevile, ameongeza kuwa,
maonesho hayo yamewasaidia kujua aina za madini zinazotakiwa
kuwasilishwa kwenye maonesho ya kimataifa, na umuhimu wa kuzingatia
ubora wa madini.
“Tumegundua
wafanyabiashara wa madini Tanzania tunahitaji kujipanga ili kuliteka
soko la kimataifa. Tumejifunza umuhimu wa kukata madini. Madini tunayo
na ni bora sana. Wachimbaji wanatakiwa kuyaongezea thamani madini yao.
Jambo hili ni muhimu sana, tunahitaji kujipanga.” Ameongeza Mushi.
Kwa
upande wake mfanyabiashara wa madini kutoka kampuni ya H.B Mining, Mhe.
Dorah Mushi, alieleza kuwa, ipo haja kwa Watanzania kuinuka kutokana na
ukweli kwamba, Tanzania inayo hazina kubwa ya madini ya aina mbalimbali
takriban katika kila Mkoa kutokana na kwamba, maonesho ni njia mojawapo
ya kusaidia kujenga mtandao wa kibiashara.
Aidha,
ameiomba Serikali kuwasaidia wananawake walioko katika sekta ya
uzalishaji wa madini ili waweze kufahamu fursa zilizopo na kujua namna
ya kuzitumia. Ameongeza kuwa, wapo wanawake wengi katika sekta hiyo
ambao wameshindwa kufaidika na sekta hiyo kutokana na ukosefu wa elimu.
“Madini
ni maisha, ni biashara, ni ajira. Kina mama litambueni hili, jiingizeni
katika sekta hii soko la kimataifa lipo. Nimeshiriki hapa Bangkok kwa
mara ya kwanza Sitaki kukosa tena maonesho kama haya. Nimejifunza mengi
ikiwemo namna ya kuuza madini. Serikali wasaidieni wadau wa madini ,
hasa kina mama , wafumbueni macho”. Amesema Mhe. Dora Mushi.
Wakati
huo huo, mfanyabiashara wa madini na Afisa Masoko wa kampuni ya Tom
Gems, Bw. Jeremiah Simioni, aliishukuru Serikali ya Tanzania kutokana
na kuwa na uhusiano mzuri na nchi ya Thailand kutokana na kwamba,
ushiriki wao katika maonesho hayo, umewafungulia mipaka ya ufahamu
kuhusiana na biashara ya madini ya vito na usonara katika ngazi za
kimataifa.
“Nataka
kuwa balozi kwa wenzangu baada ya kushiriki maonesho haya. Nataka
kuwaambia wenzangu fursa zilizopo kimataifa na namna wanavyopaswa
kuzitumia. Naishukuru sana Wizara na idara ya uthamini wa madini ya
almas TANSORT kwa kufanikisha ushiriki wetu lakini bado naiomba
Serikali iendelee kutoa mafunzo mbalimbali kwa wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini”. Aliongeza Jeremiah.
Akizungumzia
ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo, Kamishna Msaidizi wa Madini,
Mhandisi Hamis Komba, alieleza kuwa, Serikali ina mengi iliyojifunza
kutokana na ushiriki wake katika maonesho hayo ikiwemo matumizi ya
teknolojia zinazotumika katika sekta hiyo.
Aliongeza
kuwa, watanzania wakiwemo wafanyabiashara na wachimbaji wanatakiwa kuwa
na uthubutu ili waweze kuleta mapinduzi na mabadiliko katika sekta
hiyo, hali ambayo itawasaidia kuendana na biashara za nje ikiwemo pia
ushindani wa kimataifa.
Aidha,
alieleza kuwa, uwezo wa kuibadilisha Tanzania kupitia sekta ya madini
upo hivyo, amewataka wadau wote kila mmoja atekeleze wajibu wake
kikamilifu.
“Tunatakiwa
kujipanga, kwa mfano kwenye usonara kuna mengi, tunahitaji kuufikisha
usonara katika ngazi za kimataifa kuanzia teknolojia. Kila mdau analo
jukumu, wafanyabiashara na wachimbaji kuweni na uthubutu, wataalamu
nyanyukeni muisaidie Serikali”. Amesema Komba.
Akizungumzia
kuhusu uthamini wa madini ya vito na almas katika maonesho hayo,
mthamini wa madini kutoka idara ya uthamini wa madini ya almas TANSORT
Bw. Edward Rweymamu alieleza kuwa, idara ya uthamini imeyatumia maonesho
hayo kutafiti mwenendo wa bei za madini jambo ambalo litawasaidia
kuifanyia marekebisho kanzidata ya bei ili kuhakikisha wanapata
mrahaba stahiki.
Ameongeza
kuwa, si kwa wafanyabiashara na wachimbaji pekee ambao wamenufaika na
maonesho hayo bali hata nchi ya Tanzania kutokana na idadi kubwa ya
wageni waliotembelea banda la Tanzania kutafuta madini mbalimbali
yakiwemo madini ya Tanzanite, Ruby, Saphire na Almas, yakiwemo pia
madini ya viwandani hali ambayo inaashiria kukubalika kwa madini ya
Tanzania katika soko la Kimataifa.
Katika
hatua nyingine, wafanyabiashara na wachimbaji waliipongeza Serikali na
Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kitengo cha Uthamini wa madini ya
Almas (TANSORT) kwa kuratibu na kufanikisha ushiriki wa Tanzania kwa
mara ya kwanza katika maonesho hayo ambayo yamewasaidia kufungua mipaka
ya kibiashara.
Post a Comment