Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba jana waligawanyika katika
kushangilia hotuba ya ufunguzi wa Bunge hilo iliyotolewa na Rais Jakaya
Kikwete.
Mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya wajumbe wa CCM
wakidiriki hata kusimama, huku wakipiga makofi wakati Rais Kikwete
alipokuwa akielezea upungufu aliouona katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Pia kwa upande mwingine, baadhi ya wajumbe kutoka
Zanzibar walionekana wakishangilia baadhi ya sehemu ambazo zilionyesha
kuwa na udhaifu uliopo katika muundo wa Serikali mbili.
Baadhi ya maeneo ambayo yalishangiliwa kwa kiasi
kikubwa na wajumbe kutoka CCM, ni pamoja na kuondoa jambo la mafuta
katika mambo ya Muungano.
Kadhalika, wajumbe walishangilia kwa nguvu wakati
Rais Kikwete alipowataka wasisite kuondoa mambo yasiyostahili na
yanayostahili kuboreshwa yaboreshwe na kwamba katika Serikali mbili
yanatekelezeka mambo yote ambayo yametajwa kuwa masuala ya Muungano
katika Rasimu ya Katiba.
Maeneo mengine ambayo yaliamsha hisia kwa wajumbe
wa CCM hadi kusababisha baadhi yao kusimama ni wakati aliposema; “Sisi
tulioko katika CCM tunaamini Serikali mbili, tunaamini kuwa haya yote
yanatekelezeka.”
Hotuba hiyo iliyochukua saa 2.40, upande unaounga
mkono muundo wa Serikali tatu ulionekana kushangilia wakati Rais
aliposema; “Uamuzi wako usiwe wa kuambiwa na akili za kuambiwa changanya
na zako.” Shangwe hizi ziliongozwa na mwenyekiti wa CHADEMA, mh. Freeman Mbowe
Ufunguzi huo ulipambwa na gwaride pamoja na bendi.
Baada ya kufika katika Viwanja vya Bunge, Rais Kikwete alikagua gwaride
lililoandaliwa na polisi kisha kuimbwa Wimbo wa Taifa.
Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume alikuwa
kiongozi wa kwanza kuingia ukumbini, akifuatiwa na Rais wa Awamu ya
Pili, Ali Hassan Mwinyi aliyeshangiliwa kupita kiasi.
Aliyefuatia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omari Othman Makungu na kisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Othman Chande.
Wengine waliotangulia kuingia ukumbini kabla ya
Rais Kikwete, ni Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Seif
Sharif Hamad na kisha Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein akifuatiwa na
Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano, Dk. Ghalib Bilal kisha aliingia
Rais Kikwete.
Wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni mke wa Rais,
Mama Salma Kikwete, mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Asha
Bilal, mke wa Rais wa Zanzibar, Mwanamwema Shein, mke wa Waziri Mkuu,
Mama Tunu Pinda, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mtungi, Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, Mama Maria Nyerere, mke wa Rais wa Awamu
ya Pili, Mama Sitti Mwinyi, mabalozi na wawakilishi wa taasisi za dini.
Post a Comment