MKUU
WA MKOA WA GEITA NA KAIMU MKUU WA MKOA WA MWANZA SAID MAGARULA
AKIMKARIBISHA JANA 9/3/2014 MKE WA WAZIRI MKUU MAMA TUNU PINDA MKOA WA
MWANAZA AMBAPO ALIFUNGUA TAMASHA LA WANAWAKE (WOMEN DIALOGUE FRONT 2014)
IKIWA NI SEHEMU YA MAANZIMISHO YA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI
YALIYOFANYIKA KATIKA HOTELI YA JB BELMONT YA JIJINI MWANZA. HAFLA HIYO
ILIYO ANDALIWA NA MIKAELA WOMEN EMPOWERMENT INITIATIVES.PICHA PMO
============== ========== ========
MKE WA WAZIRI MKUU, Mama Tunu Pinda amewaasa wanawake
nchini kwa kuwataka wawe na nidhamu ya matumizi ya fedha za mikopo
wanayochukua kwa ajili kuendeshea miradi kama kweli wanataka kufanikiwa
na kutimiza malengo waliyojiwekea.
Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Machi 9, 2014)
wakati akifungua Tamasha la Wanawake (Women Dialogue Front -2014) ikiwa
ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika
kwenye hoteli ya JB Belmont, jijini Mwanza.
Akizungumza na washiriki wa tamasha hilo
lililoandaliwa na asasi ya Mikaela Women Empowerment Initiatives ya
jijini Mwanza, Mama Tunu Pinda alisema: “Japokuwa kwenye ujasiriamali
kuna changamoto nyingi lakini kuna wenzenu walioweza kufanikiwa. Hivyo
nina imani kubwa kuwa nanyi mtafanikiwa, ili mradi muwe na nia ya dhati
katika kutekeleza malengo mliyojiwekea.”
Akisisisitiza haja ya kuwa na uthubutu kwenye
ujasiriamali, Mama Pinda alisema: “...Lakini niwatake wanawake wenzangu
kuwa wajasiri na wenye kuthubutu na kuwa na mipango inayotekelezeka ili
muweze kutimiza ndoto zenu.”
“Sisi wanawake tunapaswa kujitambua na kuzitumia
fursa zilizopo ambazo kama tutazizingatia ipasavyo, zitatusaidia kujenga
ustawi wa maisha yetu na jamii kwa maana kukua kwa uchumi kwa mwanamke
ni kukua kwa uchumi wa familia, kaya na jamii pia.”
Aliwataka akinamama nchini watumie vizuri fursa za
mikopo na wawe waaminifu katika kutumia na kurejesha mikopo hiyo.
“Tumieni fursa za mikopo kwa kukopa kwa uaminifu, kimkakati na kwa
malengo ili kuendeleza miradi yenu na jamii kwa ujumla,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mama Tunu Pinda alisema ana imani
kwamba taasisi za fedha zitatoa kipaumbele katika kutoa mikopo yenye
riba na masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali ili kuleta maendeleo
ya kweli miongoni mwa akinamama.
Akizungumzia kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi
(VVU) katika jiji la Mwanza, Mama Tunu Pinda aliwataka wanawake hao kuwa
makini kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa vile Jiji hilo lina
kiwango cha juu cha maambukizi ya ugonjwa huo.
“Utafiti unaonyesha kwamba Jiji la Mwanza linashika
nafasi ya 11 kati ya mikoa 30 ya Tanzania sawa na asilimia 4.2. Na kati
ya hao wanawake ndio wanaongoza kuliko wanaume. Hii inasababishwa na
wengi wao kukosa uelewa wa kutosha katika masuala ya afya ya UKIMWI
pamoja na kukosekana kwa usawa wa kijamii, kiuchumi na unyanyasaji wa
wanawake na wasichana walio ndani na nje ya mahusiano,” alisema Mama
Pinda.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha ni jinsi gani
mwanamke anaweza akuchukua tahadhari mapema na ya haraka katika
kupambana na ugonjwa huo hatari. “Lakini pia mimi niseme tu, mwanamke
una nafasi kubwa sana katika kupambana na ugonjwa huu kwa kuchukua hatua
za dhati na za makusudi katika kujikinga wewe na familia yako kama
mwanamke unayejitambua,” aliongeza.
Mapema, akisoma risala yao
mbele ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa asasi ya Mikaela Women Empowerment
Initiatives, Bibi Edith Mudogo alisema asasi hiyo inayojishughulisha na
utoaji wa mikopo midogodogo kwa akinamama, ina jumla ya wanachama 102
ambao wanajihusisha na biashara, kilimo na ufugaji.
Alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo
kunyimwa mikopo na taasisi za kifedha kutokana na masharti yasiyo rafiki
yaliyowekwa na taasisi hizo; ukosefu wa fedha unaowanyima fursa ya
kuwafikia wanawake waishio vijijini na usumbufu unaopatikana katika
kukopa na kurejesha mikopo ingawa ni kwa kiasi kidogo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMATATU, MACHI 10, 2014.
Post a Comment