Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Hebron Mwakagenda
alisema hayo wakati akitoa taarifa za matokeo ya utafiti wa usimamizi wa
deni la ndani.
Alisema deni hilo limeongezeka kutoka Sh811 bilioni mwaka 2002 hadi kufikia Sh6.8 trilioni Desemba mwaka 2013.
Alisema ingawa deni hilo ni dogo ikilinganishwa na
deni la nje, lakini madhara yake ni makubwa kwa jamii ya Watanzania.
Deni la nje kwa mujibu wa utafiti huo uliofanyika kati ya mwaka 2012-13,
limefikia Sh20.2 trilioni na kwamba jumla ya deni la taifa ni Sh27
trilioni.
“Malipo ya riba kwa madeni ya ndani yamegharimu
sehemu kubwa ya rasilimali za Serikali katika kuyalipa ikilinganishwa na
madeni ya nje,” alisema.
Mwakagenda alisema asilimia 73 ya deni la ndani
inatokana na benki ambazo zinatoza riba kubwa na kwamba dhamana za
Serikali zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa.
Alisema hicho ni kiashiria kwamba, gharama za madeni ya ndani ni kubwa kuliko madeni ya nje ambayo yana masharti nafuu.
“Ukiangalia unaona wazi kuwa hali hiyo ni ongezeko la madeni ya ndani kwa kiasi kikubwa. Deni linaongezeka kila mwaka,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema Serikali inatumia fedha
nyingi kulipa riba za madeni ya ndani na kusababisha kuzorota kwa huduma
za jamii.
“Unaweza kuona kwamba, Serikali inatumia pesa nyingi kama riba kulipa madeni yake ya ndani,” alifafanua.
Alipendekeza Serikali kuondoa misamaha ya kodi ili
fedha zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ziweze
kutumika katika uendeshaji wa Serikali.
Taasisi hiyo ilipendekeza Serikali kuomba kibali
cha Bunge kila inapotaka kukopa ili sababu za kufanya hivyo ziweze
kujulikana na kusimamia utekelezaji wa fedha zinazokopwa.
Post a Comment