KIJANA
Omar Simon (30) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa
tuhuma ya kumlawiti mwanafunzi wa darasa la pili (9), anayesoma katika
Shule ya Msingi Kitangili, Manispaa ya Shinyanga, kisha kumtoboa macho
kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kumuacha porini, akisota kwa muda
wa siku mbili.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla alisema tukio hilo
lilitokea Aprili 20, mwaka huu majira ya saa 10;00 jioni katika
kitongoji cha Bugweto, nje kidogo ya Mji. Alisema mwanafunzi huyo
aliokotwa na wanawake wawili.Kamanda
Mangalla alisema siku ya tukio, mwanafunzi huyo ambaye anaishi na bibi
yake Kata ya Ibinzamata alipewa Sh 500 na bibi huyo ili apande baiskeli
kwenda kwa mama yake mkubwa anayeishi Kata ya Ngokolo.
Mangalla alidai mwanafunzi huyo alipofika katika kituo cha baiskeli,
zinazofanya biashara ya kusafirisha abiria, maarufu kama daladala au
bodaboda, alikutana na mtuhumiwa Simon, mwendesha daladala ya baiskeli,
ambaye alimpeleka katika pori dogo lililoko katika Kitongoji cha Bugweto
na kumlawiti na kisha kumtoboa macho kwa kitu chenye ncha kali na
kumtelekeza katika eneo hilo bila ya msaada.
“Tangu mwanafunzi huyo atoweke kwao Aprili 20, alikuja kuokotwa Aprili
22, mwaka huu majira ya saa 4;00 asubuhi na wanawake wawili na kumpeleka
katika Kituo cha Polisi ambao walimpeleka Hospitali ya Mkoa hadi sasa
anaendelea kupata matibabu,“ alisema Mangalla.
Kamanda Mangalla alisema mtuhumiwa tayari amekwishakamatwa na Jeshi la
Polisi, na atafikishwa mahakamani wakati wowote kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, bibi wa mwanafunzi huyo alisema
amefungua kesi katika Kituo Kikuu cha Polisi jalada lenye kumbukumbu
Namba SHY/ RB/2098/2014 baada ya kuhisi mjukuu wake, amefanyiwa kitendo
hicho, kutokana na hali aliyonayo.
Post a Comment