*********
KUANZIA sasa, shule yoyote mpya isiyokuwa na maabara ya sayansi na
maktaba haitasajiliwa na wala kuruhusiwa kutoa huduma; Serikali
imeagiza.
Wakati agizo hilo linagusa shule za Serikali pamoja na za binafsi
zinazojengwa, kwa upande wa shule zilizopo ambazo hazina mahitaji hayo,
unaandaliwa mkakati hatimaye zote ziwe na maabara na maktaba.
Akizungumza na mwandishi katika mahojiano maalumu, Kamishna wa Elimu
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bharalusesa
alisema hakuna usajili utakaotolewa kwa shule yoyote mpya bila kutimiza
masharti hayo.
Hatua hiyo ya Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wake wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu kuwezesha upatikanaji
elimu bora na yenye viwango.
Kamishna huyo wa Elimu alisisitiza, “hii inatokana na agizo la Rais
Jakaya Kikwete kwa shule zote mpya zinazojengwa kuhakikisha masharti
haya yanatekelezwa, vinginevyo, shule husika hazitapewa usajili hata
kidogo.”
Kwa mujibu wa Profesa Bharalusesa, maabara zinapaswa ziwe
zimekamilika kwa kuwa na vifaa vyote vinavyohusu masomo ya Fizikia,
Kemia na Bayolojia.
Vile vile kwa upande wa maktaba, maelekezo ya wizara ni kwamba lazima
ziwe zimekamilika kwa ajili ya kuwezesha utoaji elimu yenye viwango.
Hivi karibuni, vyombo mbalimbali vya habari, viliripotiwa juu ya
baadhi ya shule za serikali mkoani Arusha kushindwa kuanza muhula mpya
wa masomo kutokana kutokidhi masharti ya kuwa na maabara na maktaba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni
Mchome, hivi karibuni aliliambia gazeti hili kwamba yako mabadiliko
mengi yanayotarajiwa kufanyika katika sekta ya elimu.
Alisema mipango mbalimbali pamoja na sera zitaundwa kukidhi mahitaji
hayo. Alisema mabadiliko hayo yatajitokeza kupitia Sera ya Elimu na
Mfunzo inayopitiwa.
Kwa mujibu wa Profesa Mchome, kama mambo yatakwenda vizuri, sera hiyo
itakuwa tayari mwakani na itatumika kutatua kasoro mbalimbali katika
sekta ya elimu.
>>>HABARI LEO
Post a Comment